Na Richard Mwaikenda, Serengeti
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasihi Watanzania kuachana na imani, tamaduni na mila potofu ambazo zimekuwa zikiwakandamiza wanawake na kuamini kuwa hawafai katika uongozi, bali amewataka kudumisha mshikamano na umoja.
Ametoa tamko hilo leo Oktoba 10, 2025 katika mkutano wa kampeni za CCM Mugumu wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara alipokuwa akijinadi yeye , wabunge na madiwani wa chama hicho kwa kuwaomba wananchi kuwapigia kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu.
Dkt. Samia amesikitishwa na baadhi ya watu wanaotoa maneno ya kibaguzi dhidi ya wagombea ubunge wanawake wa majimbo ya mkoa huo, wakidai kuwa hawawezi kuongozwa na wanawake. Mara ina wagombea ubunge wanawake wanne katika majimbo ya Tarime Mjini, Musoma Mjini, Bunda Mjini na Serengeti.
Dkt. Samia amesisitiza kuwa kwenye maendeleo hakuna suala la jinsia na kwamba Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla itajengwa na watu wote, la muhimu ni Utanzania wa kila mmoja kushikamana kama ambavyo waasisi wa Taifa la Tanzania walivyohimiza muda wote kutaka jamii ishikamane.
Amesema kuwa Yeye akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka minne amefanya makubwa na kwamba ingekuwa mwanamke hawezi asingeweza kuyafanya. "Mungu alituumba wote na akili sawa, akatupa na uwezo wa kufikiri, tena ukiwa mwanamke mwaminifu zaidi na mtendaji zaidi kwa sababu ya uoga kuliko mwanaume," Amesisitiza Dkt. Samia huku akishangiliwa.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇