Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaahidi wakazi wa Wilaya ya Serengeti kuufanya Mji wa Mugumu kuwa kitovu cha Utalii sambamba na kujenga Uwanja wa Ndege ili kuchochea shughuli za kiutalii katika mji huo.
Dkt. Samia ameeleza kuwa mji wa Mugumu ni mji wa kimkakati kwani unaumuhimu na fursa kubwa za uwejezaji wa hoteli za kitalii kwani upo katikati ya maeneo ya hifadhi, hivyo serikali yake itajenga uwanja wa ndege ili kuwezesha watalii kutua moja kwa moja katika mji wa Mugumu jambo litakalokuza uchumi wa Serengeti na kuchochea uwekezaji zaidi.
Dkt. Samia ametoa ahadi hiyo leo Oktoba 10, 2025, wakati wa kampeni zake ndani ya Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara, huku akiongeza kuwa ataendelea kuboresha huduma muhimu za Elimu na Afya na Maji katika maeneo yote ya Wilaya ya Serengeti.
Ahadi nyingine ni uboreshaji wa barabara zinazounganisha Wilaya ya Serengeti na Wilaya za jirani kwa viwango vya lami na ujenzi wa skimu za umwagiliaji ili kuwezesha wakazi kufanya shughuli za kilimo bila kutegemea mvua.
Aidha, Dkt. Samia amesisitiza mshikamano na umoja kwa watanzania na kuwataka Wanaserengeti na Mara kwa ujumla kuweka kando mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke na kuwataka kukichagua Chama Cha Mapinduzi bila kuzingatia jinsia ya mgombea kwani katika kutafuta maendeleo ubaguzi wa kijinsia hauna nafasi.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇