Na Dkt. Dismas LYASSA,
(PhD in Leadership and Strategic Management)
Katika tafiti nilizozifanya hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, nikitumia mbinu za kisayansi za ukusanyaji wa taarifa na uchambuzi wa mitazamo ya wananchi kuhusu vyama vya siasa, nimebaini jambo la msingi na lenye uzito wa kitaifa: Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado kinaendelea kuaminiwa, kupendwa na kutegemewa na Watanzania walio wengi, licha ya kuwepo kwa vyama vya upinzani nchini.
UTAFITI ULIVYOFANYIKA
Nikiwa mtaalamu (PhD in Leadership and Strategic Management), kupitia taasisi yangu ya Tuwainue Foundation/Dr Lyassa Foundation, nilifanya utafiti wa kina kwa kipindi cha miezi mitatu, nikihoji wananchi kutoka mikoa 21 ya Tanzania Bara pamoja na mikoa yote mitano ya Zanzibar. Nilitumia njia mbalimbali kama mahojiano ya ana kwa ana, vikundi vya majadiliano (focus groups), pamoja na dodoso za mitazamo ya kisiasa na kijamii.
Lengo kuu lilikuwa ni kubaini mtazamo wa wananchi kuhusu vyama vya siasa, uongozi uliopo madarakani, na nafasi ya vyama vya upinzani katika maendeleo ya taifa.
Matokeo ya Utafiti: Imani ya Wananchi kwa CCM Ni ya Kweli na Ya Kudumu
1. CCM ni Chama Chenye Mwelekeo na Dira ya Maendeleo
Washiriki wengi wa utafiti wangu walieleza kuwa CCM imejikita katika kutekeleza ahadi na mipango ya maendeleo kwa vitendo. Tofauti na vyama vingine vya siasa, CCM haionekani tu wakati wa uchaguzi, bali huwa karibu na wananchi muda wote kupitia viongozi wake wa ngazi zote.
2. Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Wasifiwa kwa Mageuzi na Maendeleo
Katika Tanzania Bara, wananchi wengi walionyesha imani kubwa kwa Rais Samia, wakimtaja kama kiongozi wa mageuzi, mwenye maono ya kitaifa na anayesikiliza wananchi. Sera zake za kufungua uchumi, diplomasia ya uchumi, na usimamizi wa miradi ya kimkakati zimeleta matumaini makubwa kwa Watanzania.
3. Zanzibar Yashuhudia Mageuzi Makubwa Chini ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi
Katika upande wa Zanzibar, utafiti wangu umeonesha kuwa Rais Dkt. Mwinyi amefanikiwa kuimarisha amani, kukuza sekta ya uwekezaji, na kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya afya, elimu, na miundombinu. Wananchi wameeleza kuwa kuna mabadiliko makubwa yanayoonekana kwa macho.
Vyama vya Upinzani: Vinaonekana Tu Kipindi cha Uchaguzi
Utafiti pia umeonesha kuwa vyama vya upinzani vimekosa mwelekeo wa dhati wa kisiasa. Maoni ya wengi ni kuwa:
Vyama hivyo hujikita zaidi katika maneno na si utekelezaji wa sera mbadala.
Viongozi wa upinzani huonekana sana wakati wa kampeni, lakini hupotea mara tu baada ya uchaguzi.
Kuna migogoro ya ndani ya vyama, ukosefu wa umoja na ukosefu wa mikakati madhubuti ya kushindana kisera na CCM.
Wananchi walitamka wazi kuwa vyama vya upinzani kwa sasa haviwezi kuwa mbadala thabiti wa CCM kwa sababu havioneshi uongozi wa vitendo, wala kushughulikia matatizo ya wananchi kwa ukaribu.
Kwa Nini Wananchi Wanaendelea Kuiamini CCM
Sababu kuu zilizotajwa na wananchi ni pamoja na:
Uwepo wa chama katika maisha ya wananchi kila siku, si kwa msimu wa uchaguzi pekee.
Sera zinazoeleweka na kutekelezeka, kama vile afya kwa wote, elimu bure, ujenzi wa barabara na miradi mikubwa ya kimkakati kama SGR na Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Uongozi wa kitaifa wenye dira, unaoongozwa na viongozi makini na waadilifu.
Dhamira ya kweli ya kujenga taifa na kulinda amani, ambayo imekuwa msingi wa mafanikio ya muda mrefu ya Tanzania.
Kwa mtazamo wa kitaalamu wa uongozi na usimamizi wa mikakati, CCM imejidhihirisha kuwa ni chama chenye uwezo wa kukabiliana na changamoto, kujifunza kutokana na mazingira, na kuendelea kuwa karibu na wananchi. Sifa hii ni nadra katika vyama vya siasa barani Afrika.
Kauli yangu ya kitaalamu:
“Katika mazingira ya sasa ya kisiasa Tanzania, CCM si tu chama kilichoasisiwa na waasisi wa taifa, bali ni taasisi yenye mfumo imara, viongozi wa maono, na mkakati thabiti wa maendeleo unaoungwa mkono na Watanzania walio wengi.”
Dismas Lyassa ni Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya TuwainueFoundation/DrLyassaFoundation
0754498972
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇