May 29, 2025

MSAFIRI NG’AMBI WA ITIGI AMPONGEZA RAIS SAMIA, WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA CCM


Kada mkongwe wa CCM na mfanyabiashara maarufu wa matrekta kutoka Wilaya ya Itigi, Mkoa wa Singida, ndugu Msafiri Ng’ambi maarufu kwa jina la Mdau, amewapongeza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ufanisi wa Mkutano Mkuu wa Taifa unaoendelea katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.

Katika mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, pamoja na mambo mengine anasisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo ili kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi. Aidha, Rais Samia alizindua kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 isemayo "KAZI NA UTU, TUNASONGA MBELE" .

Ndugu Ng’ambi alieleza kuridhishwa kwake na maazimio yanayoendelea katika mkutano huo, akisema kuwa ni hatua muhimu katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi. Alisisitiza kuwa utekelezaji wa maazimio haya utasaidia kuboresha maisha ya wakulima na wafugaji, na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na bidhaa za mifugo.

Aidha, ndugu Ng’ambi alitumia fursa hiyo kuhimiza vijana na wanawake wa Wilaya ya Itigi na mikoa mingine kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali katika sekta ya kilimo. Alisema kuwa kupitia miradi ya kilimo cha kisasa, vijana na wanawake wanaweza kujiajiri na kuchangia katika uchumi wa taifa.

Kwa upande mwingine, wafanyabiashara mbalimbali kutoka Dodoma walieleza kuridhishwa na ujio wa mkutano huo, wakisema kuwa umeleta fursa za biashara na kuongeza mzunguko wa fedha katika mkoa huo. Mfanyabiashara wa kuku, Emmanuel Msangi, alisema kuwa wingi wa wageni umeongeza mahitaji ya vyakula, na hivyo kuongeza kipato kwao.

Kwa ujumla, Mkutano Mkuu wa CCM wa Mei 2025 umejidhihirisha kuwa ni jukwaa muhimu la kujadili masuala ya kitaifa na kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Ndugu Ng’ambi ameahidi kushirikiana na Serikali na wadau wengine wakiwamo wale walio kwenye sekta ya kilimo na masuala mengine ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Itigi na Tanzania kwa ujumla.

 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages