Apr 13, 2025

WAZIRI DK. NDUMBARO KUZINDUA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA, KAGERA KESHO

Na Lydia Lugakila, Bukoba

Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro, kesho April 14, 2025 anatarajiwa kuzindua rasmi Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) mkoani Kagera.


Kampeni hiyo yenye lengo la kutoa elimu mbalimbali za kisheria pamoja na utatuzi wa migogoro kwa Wananchi, hasa wanyonge pamoja na makundi mbali mbali wanaokabiliwa na  migogoro ikiwemo ya ardhi na mirathi inatazinduliwa katika Uwanja wa Mashujaa  maarufu Mayunga.


Kampeni hiyo inatarajiwa kuleta faraja kwa Wananchi wa Mkoa wa Kagera ambao  watafika katika viwanja hivyo kutatuliwa changamoto walizonazo kwa muda mrefu ambapo watakutana na  jopo la wanasheria kutoka wizarani, wanasheria kutoka asasi za kiraia, pamoja na mawakili wa kiserikali.


Mkurugenzi wa Kampeni hiyo(MSLAC), Ester Msambazi akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Kagera amesema kuwa mpaka sasa kampeini hiyo imeisha tekelezwa katika mikoa 23  na mkoa wa 24 ni Tanga ambapo kampeini inaendelea na sasa ni zamu ya Mkoa wa  Kagera ambapo itadumu kwa siku 9.


Amesema kuwa kuwa kila wilaya watafikia kata 10 kwa siku na vijiji 30, tunatarajia kufikia wananchi kwa asilimia 75  wenye migogoro ya ardhi ,mirathi Mkoani Kagera huku huduma zote za kisheria zikitarajiwa kutolewa bure ikiwemo uandikishaji wa vitambulisho vya taifa NIDA isipokuwa mwananchi atachangia  kidogo katika upande wa huduma za rita zinazohusiana na usajiri wa vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo.


Msambazi amewaomba wananchi wa Mkoani humo kujitokeza kwa wingi na kuwasisitiza waitumie vyema siku hiyo muhimu kwani baadhi ya changamoto zao zitaisha pale pale.


Kwa upande wake  Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta, Samia Suluhu Hassan kwani kampeini hiyo inaenda kumuhakikishia mwananchi mnyonge haki na usawa katika kupata haki zake za msingi 


Pia ametoa wito kwa Wananchi mkoani humo kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili kueleza changamoto zao.


Aidha Rc Mwassa amesema kampeini hiyo ni kabambe hivyo Wananchi wahakikishe hawabaki nyuma kwani anatambua wanakagera wanazo changamoto nyingi hasa za migogoro ya ardhi na mirathi ambazo baadhi walijaribu kuzitatua lakini nyingine zilikuwa nje ya uwezo wao.


"Niwaombe Wananchi siku ya Jumatatu April 14 saa mbili asubuhi msikose pale uwanja wa Mayunga ili shida zenu zitatuliwe kwa muda mfupi" alisema RC Mwassa.


Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa ameziagiza halmashauri za mkoa huo baada ya kuzindua kampeini hiyo waendelee kuwa na kliniki za kusikiliza kero ambazo zitakuwa zinafanyika kila siku ya Jumanne na Alhamis ambapo Mkuu wa wilaya na wataalam wake watakuwa wanakaa kusikiliza kero mbali za Wananchi katika maeneo yao.

RC Mwasa
Ester Msambazi

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages