Apr 18, 2025

KOKA : HATIMAYE WAKAZI KATA YA PANGANI KUPATA MAJI YA BOMBA

 DAWASA YAANZA RASMI MARA MOJA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI PANGANI

 

Mbunge Koka akiteta jambo na Meneja wa DAWASA Wilaya Kibaha Mjini


Na Mwandishi wetu, Pwani

MAMLAKA
ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imemkabidhi rasmi eneo la mradi Mkandarasi Shanxi Engineering  Company kuanza mara moja utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji kata ya Pangani katika Wilaya ya Kibaha Mjini.

 

Tukio hilo limeshuhudiwa na viongozi wa Mkoa wa Pwani, Viongozi wa Chama na viongozi mbalimbali wa ambapo pia walipata fursa ya kutembelea maeneo yatakayotekelezwa mradi huo ikiwemo ujenzi wa tenki la lita milioni 6 pamoja na kituo cha kusukuma maji.

 

Akizungumza katika tukio hilo, Mbunge wa Kibaha Mjini Mhe. Silvestry Koka amesema hapo awali kata ya Pangani ilikuwa na changamoto ya upatikanaji maji hivyo kwa kuanza kwa mradi wa maji Pangani ni tumaini kwa maendeleo ya Kibaha mjini na kwamba ni furaha yake kuona maji yanasambazwa kila nyumba.

 

"Katika Wilaya ya Kibaha mjini ni kata ya Pangani ndio ilikuwa ikitukwamisha kufikia asilimia 100 ya utekelezaji wa ilani ya CCM, leo tunafarijika kuona utekelezaji umeanza,"amesema. 

 

Mheshimiwa Koka ametoa rai kwa watekelezaji na wasimamizi wa mradi kukamilisha mradi kwa wakati huku pia wakiweka miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi wakati shughuli nyingine zikiendelea.

 

Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya tsh bilioni 9.8 unaanza mara moja na utatumia muda wa miezi 12 kukamilika kwake.

 

"Tayari mkandarasi yuko katika eneo la mradi akiendelea na kazi, tunategemea mradi huu utatekelezwa ndani ya miezi 12 na kuanza kunufaisha wakazi takribani 80,000 wa maeneo ya Pangani, Kibaha - Msufini, Lulanzi na TAMCO. " ameeleza.

 

Mbunge Koka na timu ya DAWASA na viongozi wa Wilaya Kibaha Mjini wakiwa kwenye eneo ambalo tayari limeanza kusafishwa kwa ajili ya kuweka matenki ya kusambaza maji katika mitaa yote ya Kata ya Pangani jana.

Mradi wa Maji Pangani unajumuisha ujenzi wa tenki la lita milioni 6, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji pamoja na   ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji na usambazaji maji kwa umbali wa kilomita 18.7.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages