Mar 20, 2025

WASIRA KUFANYA ZIARA YA SIKU TATU KAGERA.

Lengo ni Kusikiliza na Kutatua Kero za Wananchi


Na Lydia Lugakila, Bukoba

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Mhe. Stephen Masato Wasira, anatarajiwa kutekeleza ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Kagera kuanzia Machi 22 hadi Machi 25, 2025. 


Lengo kuu la ziara hii ni kufuatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.


Akizungumza na waandishi wa habari Machi 19, 2025, katika ofisi za CCM zilizopo Manispaa ya Bukoba, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa huo, Hamimu Mahmudu Omary, amewasihi Wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea Mhe. Wasira, ambaye hii ni ziara yake ya kwanza mkoani Kagera katika wadhifa wake mpya.


Hamimu alifafanua kuwa Mhe,Wasira atawasili Kagera Machi 22, 2025, kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba majira ya saa tano asubuhi. 


Mara baada ya kuwasili, atasaini vitabu katika ofisi za chama hicho kabla ya kuelekea Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, katika kata ya Kemondo, kwa mkutano mkubwa wa hadhara na wananchi wa Halmashauri hiyo pamoja na wakazi wa Kagera kwa ujumla.


"Ni muhimu wananchi wajitokeze kwa wingi kumpokea kiongozi wetu mkubwa," alisema Hamimu.


Aidha, Hamimu amefafanua ratiba ya ziara hiyo,akisema kuwa machi 23, 2025, Mhe.Wasira ataelekea Wilaya ya Karagwe kwa mkutano mkubwa wa ndani ambapo atazungumza na wananchi, wanachama, na viongozi wa CCM.


 Siku inayofuata, Machi 24, atafanya mkutano wa ndani katika Wilaya ya Ngara, akizungumza na wananchi na viongozi wa chama.


Aidha Ziara hiyo itahitimishwa Machi 25, 2025, mjini Bukoba, ambapo Mhe. Wasira atafanya muhtasari wa ziara hiyo, akilenga kuimarisha chama na kujenga mahusiano mazuri na wanachama wa CCM.


Kufuatia ziara hiyo matumaini ni makubwa kwamba itatoa fursa kwa wananchi wa Kagera kueleza kero zao na kupata majibu ambayo yanaweza kuboresha hali zao za kiuchumi na kijamii.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa huo, Hamimu Mahmudu Omary

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages