Mar 24, 2025

NEMC YASAJILI ZAIDI YA MIRADI 8000


Baraza limesajili jumla ya miradi 8,058, ambapo kati ya hiyo, 5,784 ni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira.


 Vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio  ya taarifa za TAM na Ukaguzi wa Miradi  na kutoa mapendekezo  ya maboresho  ya masuala ya msingi  ya kuzingatiwa  katika   taarifa  hizo. 


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira  (NEMC), Immaculate Semesi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.


Aidha amesema kuwa  Miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira. Kati ya hivyo, 3,058 ni vya TAM, 765 ni vya Ukaguzi, huku vyeti vingine vikiwemo vya kubadili masharti 169, vyeti vilivyohamishwa umiliki 552, vyeti vya muda (PEC) 53 na cheti kilichorudishwa (certificate of surrender) 1.


 "Katika kuboresha utoaji wa huduma za vibali vya TAM, Baraza lilianzisha mfumo wa kielectroniki unaotumika kusajili hadi kuidhinishwa  kwa miradi ya TAM  ambao umeongeza ufanisi.  Kabla ya mfumo Baraza lilikuwa linasajili takribani miradi 900  kwa mwaka na baada ya mfumo  Baraza linasajili  zaidi ya miradi 2,000  kwa mwaka, haya ni mageuzi makubwa ya Serikali ya   awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


....Katika kipindi cha mwaka 2020/21- 2024/25, Baraza limefanikiwa kusajili wataalam Elekezi wa Mazingira 1,023  na kutoa vyeti vya utendaji kwa Wataalam Elekezi 503 baada ya kukidhi vigezo  kwa mujibu wa Kanuni  za Usajili  na utendaji wa Wataalam Elekezi wa Mazingira za mwaka 2021. Kanuni hizi mpya zimeongeza ufanisi  kwa kuruhusu  usajili  kufanyika wakati wowote. Usajili wa Wataalam Elekezi wa Mazingira unafanyika kupitia  mfumo wa kielektroniki ambao umeongeza  ufanisi wa kushughulikia maombi," amefafanua Semesi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages