Mar 3, 2025

KANISA HALISI LA MUNGU BABA SASA NI KANISA HALISI LA MUUMBA, SHEREHE KUFANAYIKA JUMAPILI, LANGO LA 12 ZIVU 1 MH (MACHI 9, 2025)

Tegeta, Namanga, Dar es Salaam
Lango la 12 zivu, 1 Majira Halisi (Machi 9, 2025) Itafanyika sherehe kubwa ya kushuhudia Badiliko la Uhalisia wa Kanisa Halisi ambapo limetoka kuitwa KANISA HALISI LA MUNGU BABA na kuitwa KANISA HALISI LA MUUMBA.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo BABA HALISI, amesema leo kuwa Sherehe hiyo itafanyika kwenye viwanja vya Makao Makuu ya Kanisa, Tegeta Namanga jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana na itahudhuiriwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kanisa hilo, Uzao na Watekeleza Sauti kutoka mikoa yote na ndani na nje ya Tanzania.

Amesema wamealikwa pia viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Naibu Meya wa Kinondoni, Wenyeviti na Watendaji wa Serikali za Mitaa Kata ya Kunduchi, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wa dini, na majirani wote na Vijana (Wazee) wa mkoa wa Dar es Salaam.

Katika kusherehesha undani wa kufanyika kwa sherehe hiyo, na undani wa Kanisa Halisi la Mungu Baba kubadilika na kuwa Kanisa Halisi la Muumba, Baba Halisi ametoa andiko linalofafanua hayo kwa kina tangu Kanisa kuanzishwa hadi kufikia lilipo sasa. Tafadhali lisome kwa makini hapo chini upate uelewa.

BABA HALISI;
Kanisa Halisi lilianzia Tanzania baada ya majira za waliotumwa wote kufikia ukomo. Waliotumwa ni: Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1/Mith.3:16); Kerubi (Eze.28:15); Adamu wa kwanza (Mwa.2:15); Musa (Kut.3:10); Eliya Mtishbi (I Fal.17:1); Yesu (Mdo.10:38); Adamu wa Pili (I Kor.15: 44:49); Miaka 1000 (Isa.33:6) na Nafsi ya Kwanza (I Yoh. 5:8), ambao ukomo wao ulikuwa ni Mwaka 2017.

Ufahamu unaofundishwa Kanisa Halisi unatokana na Sauti iliyosikika Tanzania Mwaka 2015 (Sauti ya Saba); Mwaka 2019 (Sauti Mpya); Mwaka 2020 (Sauti ya Moyo); na Mwaka 2023 (Sauti ya Uhai) . Mwaka 2024 ilikuja tena Sauti Kuu ya Umilele. Ufahamu huo umeshaandikwa na kitabu chake kimeshazinduliwa kwa faida ya jamii nzima. Wengi hufananisha Kanisa Halisi na Siloamu, bila kujua kuwa Waliotumwa wote ambao nimewaorodhesha pale juu, ndio waliokuwa Siloamu (Yohana 9:7). Ni Kanisa Halisi peke yake ambalo siyo Siloamu, kwa kuwa limeanza baada ya Majira ya Waliotumwa kufika ukomo, yaani baada ya Mwaka 2017.
 
Wakati Kanisa Halisi linaanza Mwaka 2018, liliitwa Kanisa Halisi la MUNGU BABA kwa kuwa lilimilikiwa na Nafsi ya Kwanza, yaani MUNGU BABA. Sasa tumesafiri na baada ya Miaka Saba, tumefika kwenye kituo cha Limbuko Halisi, mahali ambapo mmiliki wa Kanisa ni CHANZO HALISI, yaani MUUMBA Mwenyewe. Hapa ilikuwa ni lazima Uhalisia wa Kanisa ubadilike kuwa KANISA HALISI LA MUUMBA. Ili uelewe vizuri, ni vema ufahamu kwa nini tunamwabudu CHANZO HALISI na siyo miungu ambayo katika Yeremia 10:11 iliambiwa itaangamia kwa kuwa haikuumba chochote.


KWA NINI TUNAMWABUDU CHANZO HALISI NA SIYO MIUNGU?
Ukisoma kitabu, utagundua kuwa kulikuwepo  miungu mingi; mingine ni watu na mingine ni vitu. Aidha, aliyeweza kutimiza kusudi, ni CHANZO HALISI, sio waliotumwa. Pia, kumbuka iliandikwa katika Yeremia 10:11, kwamba miungu isiyoumba mbingu wala nchi lazima iangamie. Hivyo, Kanisa Halisi tunamwabudu aliyeumba kwa kuwa ni Majira ya MUUMBA WA VYOTE kuabudiwa.
 
CHANZO HALISI TUNAYEMWABUDU
Kabla ya kuja kwa CHANZO HALISI juu ya nchi, kulikuwepo na miungu mingi. Miungu mingine ilikuwa ni watu (Kutoka 7:1; Yoshua 4:14) na miungu mingine ilikuwa ni mizimu (1Sam 28 :5-11) na miungu mingine ilikuwa ni vitu (1Sam 5:15) licha ya miungu hiyo ya watu, mizimu, vitu, na kadhalika, kulikuwepo na miungu tisa (9) mitakatifu iliyotokana na Moyo wa Mwanzo kubadilika badilika majira zote saba: Mwenyenzi Mungu (Kutoka 6:2-3); Yehova (Kutoka 6:2-3); Mungu wa Daudi (Isaya 38:5); Mungu wa Majeshi (Hagai 2:7-9); Mungu wa Danieli (Danieli 6:25-28); Mungu wa Eliya (2Fal 2:9-15); Mola (Mdo 4:23-31); Mungu wa Roho za manabii (Ufu. 22:6); na Aliyetuma Wote (Eze. 28:14).
                              
Miungu yote hii haikuumba bali aliyeumba ni CHANZO HALISI ambaye alikuwepo kabla ya chochote (Kol 1:17 a+b).  Aliyeumba ni CHANZO HALISI kwa kuwa kitabu kinasema kuwa vitu vyote vilitokana na yeye na vitarejea kwake (Rum. 11:36). Huyu ndiye Mungu wa kweli ambaye sote tunapaswa kuapa kwake ili tufanikiwe (Isaya 65:16). Pia, huyu ndiye tuliyekuwa tunamngoja na sasa tufurahie ukombozi wake (Isaya 25:9), maana amekuja.

Kwa Nini CHANZO HALISI Amekuja?
1.Katika Zab 98:1-8, ilisikika sifa katika Moyo wake vitu vyote vilikuwa vinamsifu yeye, akataka hiyo sifa iwe halisi. Tunasoma katika Methali 3:16, kuwa alipoengua Moyo wake upande wa kushoto aliweka utajiri na heshima na kulia akaweka siku nyingi na sio umilele. Kwa mujibu wa Mwanzo 1:1, Moyo wa Mwanzo, alipewa safu ya kusimamia uumbaji lakini tunasoma katika Ufunuo 12:1-9, kuwa Ishara ya 1,2,3 walivamia kusudi hilo nalo halikutimia.

2.Baada ya kusudi la uumbaji kutotimia kwa upande wa Moyo wa Mwanzo, CHANZO HALISI aliumba Bustani nyingine inayojulikana kama Adeni katika (Ezekiel 28:13-15). Hapa CHANZO HALISI alitaka Sifa na Kuabudu vitokee, lakini havikutokea. Tunasoma katika (Ezekiel 28:16-19) kuwa kusudi halikutimia. Maana ile miduara 3 katika Ufunuo 12:1-9, ilimdanganya Kerubi akashindana na Muumba wake (Isaya 14:13). Kusudi halikutimia kwa Kerubi akatupwa chini.

3.Baada ya kusudi kutotimia kwa Kerubi, ilibidi Muumba aumbe Bustani nyingine tena inayoitwa Edeni (Mwanzo 2:7-15), akakabidhiwa Adamu wa Kwanza ikiwa na kila kitu kizuri kinachofaa kwa maisha yaliyokusudiwa kwa kila atendaye kwa haki. Kwa kuwa waliochafua kusudi wakati wa Moyo wa Mwanzo na wakati wa Kerubi walikuwepo hapo pembeni wakati Adamu wa Kwanza anaumbwa, basi walichafua kusudi hata kwa Adamu (Mwanzo 3:1-16). Baada ya uchafuzi huo ilibidi Adamu wa Kwanza atupwe nje ya Bustani ya Edeni na bustani ile ikabaki mikononi mwa nyoka na uzao wake (Mwanzo 3:22-24). Kusudi kwa Adamu halikutimia kama ilivyotokea kwa waliomtangulia.
 
4.Baada ya kusudi kutotimia kwa Adamu wa Kwanza, ilibidi Muumba amwinue Musa (Kutoka 3:3-10). Hapo ni baada ya Nuhu (Mwanzo 9:20-22) na Ibrahimu (Mwanzo 12:1-4), kutofanikiwa kufanya walichokuwa wameagizwa kufanya. Musa baada ya kuchoshwa na lawama na manung’uniko ya wale aliokuwa anawaongoza, naye pia kusudi alilopewa kuwatoa Wenye Haki utumwani kuwapeleka nchi ya maziwa na asali, halikutimia (Hesabu 20:8-11).

5.Baada ya kusudi kutotimia kwa Musa, ilibidi MUUMBA aje na uumbaji mwingine kwa mara ya tano kupitia Eliya Mtishbi (1Wafalme 17:1, 1Wafalme 18:30-40). Ishara ya kwanza (Ufunuo 12:1), alikuja kinyume na Eliya Mtishbi kwa uso wa Yezebeli ikasababisha kusudi ndani ya Eliya Mtishbi lisitimie (1Wafalme 19:1-14).
 
6.Baada ya kusudi kutotimia kwa Eliya Mtishbi, ilibidi MUUMBA aje na uumbaji mwingine kwa mara ya sita kupitia Yesu (Mathayo 2:1-14, Mdo 10:38). Kilichosababisha kusudi kutotimia kwa upande wa Yesu, ni maumivu aliyokutana nayo msalabani yakasabisha amlaumu Baba yake (Math.27:45-47). Kusudi la kuwasaidia wanaonewa na ibilisi na kuwapatia vitu vizuri (Efeso 1:21), halikuwezekana tena kutimia. Hiki ndicho kilisababisha Yesu aseme kuwa Ufalme utatoka Mashariki ya kati na kuhamia taifa lingine (Mathayo 21:43). Baada ya sauti kuu kusikika mara kadhaa Tanzania, sasa tumeelewa kuwa taifa alilomaanisha Yesu ni Tanzania.
 
7.Baada ya kusudi kutotimia kwa Yesu, ilibidi Sauti iliyokuja na uumbaji kwa mara ya Saba ipitie kwa Eliya Adamu wa Pili (1Wakorintho 15:44-49), wa Tanzania Mwaka 2003, akiwa mjini Kigoma. Kutokana na mnyama asiyeleweka (Daniel 7:7), kusudi halikutimia tena kwa Eliya Adamu wa Pili.
 
8.Baada ya kusudi kutotimia kwa Eliya Adamu wa Pili, MUUMBA aliinua uumbaji mwingine kwa mara ya Nane (8) kupitia Sauti Kuu aliyoipokea Miaka 1000, Mwaka 2015, naye pia akiwa mjini Kigoma. Sauti hii ililenga kuleta majira imara, ukombozi tele na kumcha MUUMBA (Isaya 33:6). Kwa sababu ya mashtaka mengi ya uongo (Daniel 12:7-11), Miaka 1000 naye pia kusudi halikutimia.

9.Baada ya kusudi kutotimia kwa Miaka 1000, MUUMBA aliinua Sauti Mpya, Mwaka 2019 kwenye Hija ya Viumbe Vyote, iliyokuja na uumbaji wa Moyo Mpya wa (Ezekeli 36:26), ili Kanisa livuke Korongo la Giza katika (2Wakorintho 4:6). Dunia baada ya kuona Moyo Mpya umesimama ilikuja kuupima huo moyo kupitia janga la korona, hapo ilibidi CHANZO HALISI aje mwenyewe kupitia Sauti ya Moyo mwaka uliofuata wa 2020.

10.Baada ya Moyo Mpya wa Ezekiel 36:26 kutolifikisha kanisa kwenye uumbaji ulio kusudiwa ilibidi CHANZO HALISI aje mwenyewe kupitia Sauti ya Moyo Mwaka 2020 ili kuzima mwenyewe janga la korona ambalo lililenga kufuta Bara la Nuru (Afrika) lote. Kuanzia Mwaka 2020 hadi kitabu hiki kinaandikwa 2 Zivu,1 Majira Halisi (2025), ndipo sasa kusudi la uumbaji la tangu Chanzo limetimia kwa sababu ya kufika kwenye LIMBUKO HALISI.
 
Hii ina maana kwamba kama CHANZO HALISI asingekuja mwenyewe hakuna ambaye angeweza kutimiza kusudi la uumbaji. Hivyo sifa, heshima na utukufu vina mrudia mwenyewe CHANZO HALISI aliyeweza kutimiza kusudi lake maana wote aliowatuma hawakuweza.
 
KWA NINI UHALISIA WA KANISA HALISI [JINA] UMEBADILIKA?
Uhalisia (ikiwa na maana ya jina la Kanisa), umebadilika kwa kuwa tulikuwa tunasafiri ili kufika kwenye kituo kikuu cha LIMBUKO HALISI ambako sasa tumefika. Hilo Limbuko Halisi ni Moyo. Tangu Chanzo, kilichokusudiwa ni Moyo (Methali 4:23). Ingawa iliandikwa katika Yohana 4:23, kuwa Mungu ni roho, lakini ijulikane kuwa MUUMBA siyo roho bali ni Moyo. Hii ni kwa sababu chemchemi ya Uzima ni Moyo. Baada ya uvamizi wa Moyo wa Mwanzo, ndipo ikaandikwa katika Rumi 8:23, kuwa sote tulikuwa malimbuko ya roho na nafsi. Pamoja na kuandikwa hivyo, Limbuko Halisi ni Moyo kwa kuwa ndio uliokuwepo kabla ya uvamizi wa ishara ya kwanza hadi ya tatu (Ufunuo 12:1-9). Hata mwili, ambao katika Rumi 8:4-7, ni uadui na CHANZO HALISI, sio kusudi la tangu Chanzo. Pia, asili ambaye ameandikwa katika Rumi 8:29, kuwa kila kitu kilijulikana kutoka kwake, bado kweli ipo pale pale sio kusudi. Maana roho, nafsi, mwili, asili wote ni wavamizi kinyume na Moyo na ndio walisababisha mauti iwepo.

CHANZO HALISI akiwa hajaumba chochote alikuwa Moyo, hadi sasa ni Moyo. Baada ya uvamizi ndipo sasa ikatokea mioyo mingi. Hii ni kwa sababu nafsi ya mvamizi katika Mwanzo 3:20, alidai kuwa yeye ni mama wa wote wenye uhai. Kila mmoja akajikuta ana moyo wake peke yake kutokana na aina mbalimbali za roho, nafsi, asili na mauti ndani yake. Hapakuwahi kuwepo na Moyo Mmoja katika majira zote saba. Baada ya CHANZO HALISI kuja juu ya nchi ndipo sasa amekomesha watangulizi wote wabaya ambao anawaita wezi na wanyang’anyi (Yohana 10:8). Watangulizi hao wabaya ndani ya kila mmoja walikuwa ni roho, nafsi, mwili, asili, mauti, na kadhalika. Ila sasa kila aliyeumbwa amekuwa Uhalisia wa Moyo. Hii ndiyo sababu ya Uhalisia wa Kanisa Halisi kubadilika na kuitwa KANISA HALISI LA MUUMBA.

KUZALIWA KWA KANISA HALISI LA MUUMBA
Waliotumwa wote, walikuwa ni Kanisa, ila Kanisa la kipindi hicho lilitekwa nyara na miduara mitatu ya Ufunuo 12:1-10, ikawaficha gizani kama tusomavyo katika Isaya 45:2-3. Kanisa lina Baba na Kanisa lina Mama, ila limezaliwa kwa Sauti ya CHANZO HALISI, siyo roho, nafsi wala mwili kama ilivyokuwa katika Majira Saba zilizopita. Hivyo, Sauti inayotolewa na CHANZO HALISI, kupitia kinywa cha Baba Halisi kila lango (siku), ndiyo imezaa KANISA HALISI LA MUUMBA.

KANISA HALISI LA MUUMBA lina Uzao Halisi badala ya waumini/washirika, ambao wamekuwa Limbuko Halisi, ili wote wawe na haki sawa mbele za CHANZO HALISI, aliyetoka mahali pake kuja kulitafuta Kanisa (Isaya 52:4-6/Mika 1:2-6). Kwa hiyo, Kanisa halijazaliwa na mtu, wala ukoo au kabila fulani. Maana Sauti ya CHANZO HALISI ambayo imezaa KANISA HALISI LA MUUMBA, siyo ya ukoo wala kabila fulani.

Licha ya KANISA HALISI LA MUUMBA kuwa na Baba Halisi na Mama Halisi, pia lina Mnara Moja Halisi, ambao huishi sehemu moja na Baba Halisi na Mama Halisi. Safu kubwa ya Mnara Mmoja Halisi ni kusababisha Sauti ya kila lango (siku) kuwa na nguvu ya: Kuhudumia uzao; Kudhihirika kwa yote yaliyotamkwa kwa uzao; Kutimia kwa yote yaliyotamkwa kwa uzao; na Uzao kuuona Uaminifu wa CHANZO HALISI katika safu mbalimbali walizonazo.

MTIZAMO WA KANISA HALISI LA MUUMBA
Msisitizo wa Kanisa Halisi siyo kwa walioko ndani ya jengo la Ibada peke yake, bali ni kila mmoja kumjua ALIYEUMBA KILA KITU. Kwa mfano, Jengo la Kao Kuu wakijaa, wanakuwa Elfu sita (6) lakini katika taifa la Tanzania, wanaosikiliza Sauti kila lango ni zaidi ya Milioni moja na nusu; Kenya wanaosikiliza Sauti ya kila lango ni zaidi ya elfu thelethini; Marekani (USA), wanaosikiliza Sauti ya kila lango ni zaidi ya Elfu kumi; na kadhalika. Msisitizo siyo kuta Nne za jengo la ibada kwa sababu ya kuongozwa na Sauti. Hivyo, msisitizo wa KANISA HALISI LA MUUMBA ni kila mmoja amfahamu na kumwelewa ALIYEUMBA KILA KITU.

Tunafanya hivyo kwa kuwa Msingi uliokuwepo katika majira saba ilikuwa ni Kanisa na Taifa kutofanya kazi pamoja. Musa hakufanya kazi na Mfalme Farao. Eliya Mtishbi hakufanya kazi na Mfalme Ahabu wa Israeli. Hata Yesu hakufanya kazi na Mfalme Herode. KANISA HALISI LA MUUMBA, kwa kufahamu kwamba kila aliyeko madarakani amepata kibali cha MUUMBA, tunainua wote kila alfajiri, hasa walioko madarakani.

MSIMAMO WA KANISA HALISI LA MUUMBA
KANISA HALISI LA MUUMBA halijishughulishi na Siasa kwa namna yoyote (ikiwa na maana na kukosoa na kulaumu au kunung’unikia viongozi wa nchi), ila linainua viongozi wote walioko madarakani bila ubaguzi wa kidini au kiitikadi kila alfajiri na mapema kama tusomavyo katika 1Timotheo 2:1-4. Hili linasababisha tuishi kwa amani na utulivu. Huu pia ni utimilifu wa Efeso 3:10, ambayo inasisitiza kuwa Hekima iliyo ya namna nyingi itajulikana kwa falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho (waanzilishi wa majanga mbalimbali katika jamii) kupitia Kanisa.

KANISA HALISI LA MUUMBA NA NIDHAMU YA TENDO MOJA HALISI
Hapa tunacholenga ni kutokuwa na urasimu wa Majira Saba zilizopita (bureaucracy) ndani ya KANISA HALISI LA MUUMBA. Wengi wanatamani KANISA HALISI LA MUUMBA lingekuwa na urasimu kama ule wa taasisi za kidunia, katika hali kama hiyo kusingekuwepo  Haja ya CHANZO HALISI kuachilia Sauti ya Uzima kila lango (siku). Tatizo ni kwamba, tulikuwa hatufahamu wala kuelewa kuwa kuna NG’AMBO ya Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1 na Mith.3:16). Ila Wanaokosoa uongozi wa Sauti, ni wale waliokuwa wanajua siri ya Moyo wa Mwanzo, ingawa  walikuwa hawafahamu kuwa kuna Ng’ambo ya Moyo wa Mwanzo. Kwa mantiki hiyo, KANISA HALISI LA MUUMBA lina nidhamu ya Tendo Moja Halisi, badala ya urasimu (bureaucracy) wa Majira Saba.
 
Hicho ndicho kinachosababisha KANISA HALISI LA MUUMBA kukua haraka. Mtekeleza Sauti kwa Tendo Moja Halisi, akiwa Mkoa wa Katavi, atafanya kitu ambacho, hata Baba Halisi kama angekuwa Mkoa wa Katavi angefanya hicho hicho, kwa kuwa CHANZO HALISI ni Moja akiwa ndani ya Moyo wa Kila Mmoja.

MAJIRA YA KANISA HALISI LA MUUMBA
Kwa mujibu wa Esta 3:7, mwaka halisi una miezi 12 peke yake. Aidha, sote tunajua kuwa wiki ina malango (siku) 7 na mwezi una wiki 4, ikiwa na maana ya mwezi kuwa na malango 28 peke yake na hivyo mwaka kuwa na malango 336.

Kuanzia mwaka 1582, dunia iligeuza mwezi ukawa na siku 29, 30 na 31; kwa maana ya kuongeza siku moja, mbili, tatu katika mwezi. Hii ilisababisha mwaka uwe na siku 365¼ ikiwa na maana ya miezi 13 kwa mwaka. Baada ya jambo hili, mfumo wa kila kitu kila mahali ulibadilika, si kwa mema bali kwa mabaya. Kila mmoja alilazimika kuwa na nyakati za mabaya katika maisha yake hata kama ni mtakatifu kiasi gani, maana waliokuzaa wanavinasaba ndani yako vyenye nyakati za mabaya. Ndipo ikaandikwa katika Efeso 6:13, kuwa kuna siku ya uovu.

KANISA HALISI LA MUUMBA lina MWAKA HALISI ambao una malango (Siku) 336 peke yake kwa mwaka (yaani miezi 12 na malango 28 kwa kila mwezi). Kwa kuwa Majira ni CHOMBO kinachobeba maisha ya kila mmoja, KANISA HALISI LA MUUMBA tuna CHOMBO KIMOJA HALISI ambacho ni MAJIRA NA WAKATI KABLA YA UHARIBIFU.

FUNDISHO LA KANISA HALISI LA MUUMBA
KANISA HALISI LA MUUMBA, kwa kila anayesimama mbele ya wengine, linasisitiza:
A) Utawala wa Amani kwa Wote, Kila unayekutana naye uwe na Amani naye hata kwa gharama ya kunyenyekea. Kwa sababu hiyo, KANISA HALISI LA MUUMBA tunainua watu wote kwa shukrani kila alfajiri hasa walioko madarakani (ITimotheo 2:1-4).

B) Upendo Usiobagua yeyote
KANISA HALISI LA MUUMBA hatubagui Mkristo wala Muislamu wakati wa Ibada kwa kuwa tunaelewa kuwa CHANZO HALISI hana dini wala dhehebu. Katika I Kor.13:13, kuna matatu: Imani, Tumaini na Upendo, na lililo kuu ni Upendo. Imani na Tumaini vilikuwa vinatubagua, lakini Upendo haubagui yeyote. KANISA HALISI LA MUUMBA tumechagua Upendo Usiobagua. Huu ndio mlango unaotuwezesha kufanya kazi na jamii na Taifa.

C) Ibada ni Uzalishaji
Kwa upande wa KANISA HALISI LA MUUMBA Ibada ni Uzalishaji, siyo kulia wala kuomboleza kama ilivyokuwa wakati wa majira zilizopita. Tunaelewa kuwa Daudi amefundisha sana kulia katika kitabu cha zaburi, lakini majira hii MUUMBA ameshakuja kuishi nasi kama alivyoahidi katika maeneo mbalimbali: Mdo 2:34-35; Ikor.15:24,28; Ufu.21:3; Zek.15:9; na Mathayo 21:41. Kwa hiyo kwa KANISA HALISI LA MUUMBA ibada ni uzalishaji, siyo tena maombolezo kama ilivyozoeleka.

UFAHAMU WA KANISA HALISI LA MUUMBA
Kwa mujibu wa Mithali 8:14-30, ufahamu una kila kitu ambacho kila mmoja anahitaji. Katika majira saba zilizopita, wote tulitegemea ufahamu ulioanzia Mashariki ya Kati ndiyo maana tunasoma katika Mdo.8:27- na kuendelea, habari za Waziri wa fedha wa Kushi wakati ule akiwa anaenda Yerusalemu kuangalia mahali ufahamu uliokuwepo wakati huo, ulipoanzia. Kanisa Halisi tunategemea ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda mataifa mengine yote (Mathayo 21:43). Hii ni baada ya Sauti ya CHANZO HALISI kusikika Tanzania. Maana Sauti ndiyo Chanzo cha ufahamu.

HITIMISHO
Kupitia haya machache niliyoandika, kilichobadilika ni Uhalisia wa KANISA, ikiwa na maana ya kutoka MLIMA WA NAFSI/ROHO (Rum.8:23) na kuhamia MLIMA WA MOYO HALISI (Mithali 4:23). Huu pia ni utimilifu wa Isaya 2:2. Hivyo, KANISA HALISI LA MUNGU BABA SASA LINAITWA KANISA HALISI LA MUUMBA.
Baba Halisi akiwa na Mama Halisi wakati wa moja ya Ibada za Kanisa Halisi. (Picha na Maktaba ya CCM Blog).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages