- Asema yupo tayari kuwapa somo waifahamu vyema katiba ya Chama
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mainduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliomchagua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kugombea kiti cha Urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umezingatia takwa la kikatiba na mamlaka ya Mkutano Mkuu.
Amesema baadhi ya watu wanaojiita wanaCCM wanaodai kwamba bado hawajaelewa sababu ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kupitisha uamuzi huo, atawasaidia kuelewesha kwani uwezo wa binadamu kufahamu jambo hauwezi kulingana.
Wasira aliyasema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati viongozi, wanachama, wapenzi wa CCM na wananchi kutoka maeneo mbalimbali walipojitokeza kumpokea.
"Baada ya Mkutano Mkuu kutambua kazi kubwa zilizofanywa na serikali zote mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, Mkutano Mkuu wa CCM ukasema kama hali ni hii kuna sababu gani kuchelewesha kutangaza mgombea?.
"Sasa wapo watu wanaosema wao ni wanachama wa CCM, hawakuelewa. Hilo nalo siyo jambo la ajabu. Tutawasaidia kuelewa maana siyo watu wote wanaweza kuelewa sawa. lakini tunawaambia Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CCM ndiyo kikao kikuu cha mwisho," amesema.
Wasira ameeleza kuwa Mkutano Mkuu wa Chama una mamlaka ya kubadili, kufuta na kurekebisha uamuzi wowote uliofanywa na kikao cha chini yake, kufuta maamuzi yaliyofanywa na kiongozi yeyote wa CCM.
"Mkutano Mkuu ndiyo unawakilisha wanachama na hiki chama ni chama cha wanachama, wawakilishi wenu walipokutana na kuliridhika wakatumia mamlaka ya Mkutano Mkuu wakasema tutampa Samia mitano tena. huo ni uamuzi wa Mkutano Mkuu, sasa kama wewe huelewi sijui," anabainisha.
Amesema Wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, walikutana kwa dharura baada ya kuagizwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu waondoe vikwazo vinavyozuia uamuzi wa Mkutano Mkuu kufanya uamuzi huo.
"Tukakutana tukaondoa vikwazo na Kamati Maalum ya Zanzibar ikakutana ikamkubali, Dk. Hussein Ali Mwinyi kugombea Urais upande wa Zanzibar. Wakaleta kwenye Halmashauri Kuu tukapiga kura kwa sababu Halmashauri Kuu ndiyo inamteua Rais wa Zanzibar.
"Baada ya hapo Halmashauri Kuu ikapendekeza kwenye Mkutano Mkuu kutekeleza Azimio la Mkutano Mkuu kwani hakuna sababu ya kuchelewa. Kwa mujibu wa kanuni Mkutano Mkuu unateua kwa kupiga kura, tukapiga kura ambapo Samia akachaguliwa kuwa mgombea Urais kwa asilimia 100 za kura za Mkutano Mkuu.
Amesisitiza: "Sasa aliye na mashakana katika jambo hilo kama wote hawawezi aje kwangu nitamsadia maana katiba ipo kichwani. Uamuzi tulioufanya umezingatia Katiba ya CCM ibara ya 101 inayotutaka tuchague jina moja la kuwa mgombea wa kiti cha Urais, tulitumia ibara hiyo na kwa mamlaka ya Mkutano Mkuu ameteuliwa Dk. Samia."
-
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇