Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM, Dodoma
Mkutano Mkuu maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ulioanza leo Januari 18, 2025, katika Ukumbi wa jakaya Kikwete jijini Dodoma umemchagua kwa kishindo mwanasiasa mkongwe Stephen Masato Wasira, kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara kwa kupata zaidi ya kura 99% za wajumbe kutokana na kura 1921 zilipigwa, ambapo kura halali zilikuwa 1917 za hapana zikiwa 7 tu.
Kufuatia kushinda kiti hicho Wasira anakuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara wa tano, akichukua nafasi iliyoachwa na Abdulrahman Kinana ambaye mwaka jana aliomba kupumzika. Wengine waliopata kushika wadhifa huo ni Mzee John Malecela, Pius Msekwa na Philip Mangula.
Wasira ni nani?
Alizaliwa mwaka 1945 katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara (ana miaka 70). Alisoma katika shule tatu tofauti, ya kwanza ni Shule ya Msingi Bariri 1956-1959, ya pili ni Shule ya Msingi Nyambitilwa 1960–1961 na kisha akamalizia Shule ya Msingi Kisangwa mwaka 1962 - 1963.
Kati ya mwaka 1964–1967, Wasira alisoma elimu ya Sekondari katika Chuo cha Ukufunzi Uingereza (British Tutorial College) na kuhitimu kidato cha nne na wakati anasoma sekondari (1965–1967), pia alifanya kazi akiwa msaidizi wa masuala ya maendeleo ya jamii na alipohitimu kidato cha nne alianza kuitumikia chama cha tanganyica African Nationalo Union (TANU) akiwa Katibu wa wilaya mwaka 1967-1973.
Mwaka 1975–1982 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na mwaka 1982 akateuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington, D.C. Alipokuwa huko alisoma na kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Uchumi na Uhusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Amerika (American University) kilichopo Washington DC mwaka 1982–1985.
Wasira alianza utumishi wa ubunge akiwa na miaka 25, hii ilikuwa mwaka 1970 aliposhinda ubunge wa Jimbo la Mwibara na akaongoza hadi mwaka 1975 huku Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere akimteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Mwaka 1985, Wasira aligombea na kushinda ubunge wa Jimbo la Bunda (wakati huo likiwa limemeguliwa kutoka lililokuwa Jimbo la Mwibara. Katika kipindi hiki aliteuliwa na Rais Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo mwaka 1989 hadi 1990.
Wasira alisoma Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Umma kati ya mwaka 1985–1986 na aliporejea nchini kuendelea na utumishi wa uwakilishi wa wananchi, aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990-1991.
Kati ya mwaka 1993–1995 alisoma tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Amerika.
Ndani ya CCM, amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) tangu mwaka 2007 na mwaka 2012 akachaguliwa katika wadhifa huo tena kwa kura nyingi kuwashinda wajumbe wote wa Tanzania Bara. Lakini pia amekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM tangu mwaka 2011 na tena 2013 hadi sasa.
tukirejea nyuma, kipenga cha vyama vingi kilipopulizwa mwaka 1995, Wasira alihitaji kuwaongoza wana Bunda lakini akaangushwa kwenye kura za maoni za ndani ya CCM, aliyemwangusha ni Jaji Joseph Warioba (Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu).
Wasira hakuridhishwa na ushindi wa Warioba na aliamua kuihama CCM na kwenda NCCR Mageuzi wakati huo ikiwika, akachaguliwa kwa kura 18,815 dhidi ya 17,527 za Warioba na hivyo akawa mbunge kupitia NCCR.
Warioba alikata rufaa Mahakama Kuu nayo ikatengua ubunge wa Wasira mwaka 1996 baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na rafu zilizofanyika ikiwamo kudaiwa matumizi ya rushwa na ikampiga marufuku kugombea kwa miaka kadhaa. Wasira alikata rufaa mara kadhaa na kushindwa. Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu.
Uchaguzi wa marudio ulipofanyika mwaka 1999 Wasira alikuwa amekwishatangaza kuihama NCCR kutokana na siasa za ugomvi na mara hii alimuunga mkono mgombea wa UDP, Victor Kubini lakini mara baada ya uchaguzi huo aliamua kurejea CCM. Miaka mitano iliyofuatia (2000 – 2005) na hata minne iliyopita (1996 – 2000), Wasira alijielekeza katika biashara ya kusafirisha mazao ya bahari nje ya nchi.
Alirejea katika ulingo wa siasa mwaka 2005 na kushinda kura za maoni ndani ya CCM na akapitishwa kugombea ubunge wa Bunda na akapita bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Maji Januari 2006- Oktoba 2006.
Kati ya Novemba 2006 – Novemba 2010 alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, lakini Februari–Mei 2008 aliwahi kutumikia kwa muda Ofisi ya Waziri Mkuu akiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Katika uchaguzi wa mwaka 2010, Wasira aligombea tena ubunge wa Bunda na kushinda kwa asilimia 66.1 na Rais Kikwete akamteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu kabla ya mwaka huu kurudishwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Nguvu yake
Wasiria alikuwa na rekodi nzuri ya kiutendaji katika awamu zote alizopitia. Uchapakazi, ufuatiliaji na usimamizi ni moja ya sifa kubwa za Wasira kwa watu waliofanya naye kazi. Rekodi hii pia inamuongezea alama muhimu.
Alikonekana kwa mhimili muhimu katika Serikali ya Kikwete na ndiyo maana ili kujipunguzia mzigo wa kazi na kuhitaji mtu mwenye uwezo wa kufanya uamuzi katika Ofisi ya Rais, Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uhusiano na Uratibu. Hivyo Wasira akawa mmoja wa watu walio karibu sana na Rais Kikwete kushinda watu wanavyofikiria.
Mwisho Wasira ni mcheshi na ni mtu wa kawaida sana. Kwa wanaomfahamu wanajua kuwa hajajitengenezea “himaya binafsi”, uwezo wa kifedha wenye kuibua shaka na mambo mengine kama hayo. Maisha haya ya kawaida yanamfanya awe mmoja wa viongozi wa kawaida. Lakini zaidi ya yote, anapenda mijadala, kubishana na kushindanisha hoja na ni rahisi hata kuwamudu vijana.
Your Ad Spot
Jan 18, 2025
Home
featured
siasa
MJUE WASIRA MAKAMU MWENYEKITI WA CCM BARA, WAZIRI CHINI YA NYERERE, MWINYI NA KIKWETE
MJUE WASIRA MAKAMU MWENYEKITI WA CCM BARA, WAZIRI CHINI YA NYERERE, MWINYI NA KIKWETE
Tags
featured#
siasa#
Share This
About Bashir Nkoromo
siasa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇