LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 6, 2024

BILIONI 8.482 ZA TASAF ZAWANUFAISHA WANANCHI 10,323 IGUNGA



Na HEMEDI MUNGA, Igunga 


WANUFAIKA wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu  (TASAF) wilayani Igunga mkoani Tabora wameendelea kutoa ushuhuda kuwa mpango huo umeendelea kuwakwamua kutoka kwenye hali duni za maisha.


Aidha, Wamebainisha kuwa wameweza kujiongezea kipato, kuongeza huduma za kiuchumi na kulinda rasilimali za kaya hususan zile za watoto wao.


Akizungumza mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo, Sauda Mtondoo mmoja wa wanufaika wa mpango huo katika kijiji cha Njiapanda kata ya Nkinga wilayani hapa, Magdalena Kishiwa amesema TASAF imemnufaisha kwa kuweza kulima mazao mbalimbali ikiwemo mpunga, mahindi na kufuga kuku.


"Nikiivisha mavuno nauza na mengine yanabaki yakinisaidia kwa kweli ni mfano wa chura ukimpiga teke  umemuongezea mwendo hivyo TASAF imeninyanyua ninamshukuru Rais Dk. Samia kwa kuendelea kuwezesha mpango huu," ameshukuru Magdalena.


Kwa upande wa Mkuu wa wilaya hiyo, Sauda Mtondoo ameendelea kumpongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha mpango huo.


"Kipekee tuendelee kumpongeza na kumshukuru Rais Wetu Dk. Samia Suluhu Hassan ambae ameendelea kuwezesha mpango huu hadi leo tunamadirisha ya uhawilishaji zaidi ya 20," amesema.


Ameweka wazi kuwa yapo mabadiliko makubwa kwa sababu wapo wanufaika  walioweza kuboresha nyumba zao, kupeleka watoto shule, kuhudhuria klini kila wanapopangiwa tarehe na kuwa na uhakika wa chakula.


"Ndugu zangu tujue serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ipo pamoja na sisi, hivyo nendeni mkaendelee kuzalisha kupitia ruzuku hii kwa lengo la kuendelea kujikwamua na umasikini," amesisitiza DC Sauda na kuongeza kuwa :


"Tuamini sisi sote tumenufaika na kubadilisha hali za maisha yetu kwa sababu tulivyo sasa ni tofauti na tulivyokua kabla ya mpango huu."


Katika hatua nyingine, DC Sauda amewahimiza kuwa na wivu wa kimaendeleo na kuuchukia umasikini kwa nguvu zote kwa sababu wakiyafanya hayo watakua wameutupa umasikini.


Kwa upande wa Mratibu wa TASAF wilayani hapa, Dina Madeje ameeleza kuwa wilaya hiyo imetekeleza awamu 20 za uhawilishaji na kutumia sh bilioni 8.482 huku walengwa 10,323 wafikiwa na kunufaika na mpango huo.


Pia, amebainisha  kuwa Igunga itatekeleza miradi ya ajira za muda 80 katika vijiji 72 ifikapo Novemba mwaka huu huku ikilenga kutumia sh milioni 897.271.


Amesema kaya 5,417 sawa na asilimia 92 zimeweza kumudu mahitaji ya chakula bila mashaka huku kaya 5,775 sawa na asilimia 90 zikiweza  kuwekeza katika kilimo kwa kununua mashamba, pembejeo za kilimo ikiwemo nguvu kazi.


Aidha, ameongeza  kuwa kaya 4,042 sawa na asilimia 63 zimewekeza kwenye ufugaji mdogo, kaya 770 zimewezeshwa kumudu matibabu kupitia fedha za TASAF huku kaya 5,839 sawa na asilimia 91 zimeweza kumudu gharama za masomo kwa watoto ikiwemo kununua sare za shule na vifaa vya kusomea.



Mpango wa Kunusuru Kaya masikini Awamu ya Tatu unatekelezwa katika vijiji vyote 119 ikiwemo eneo la Mamlaka ya Mji Mdogo wilayani hapa.








 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages