Na Mwandishi Maalum, Kibakwe
Zikiwa zimebaki siku nne, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Orodha ya Wapiga Kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji huku akiwataka vijana wawe mstari wa mbele kushiriki zoezi hilo.
Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Kijijini kwake Pwaga katika Tarafa ya Kibakwe Mkoani Dodoma mara baada kujiandikisha kwenye daftari hilo ambapo amesema uchaguzi huo ni muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya vitongoji na mitaa kwa ujumla.
Hata hivyo, Mhe.Simbachawene amewataka Wananchi kutofautisha uandikishaji wa daftari la makazi unaoratibiwa na TAMISEMI na ule wa daftari la kudumu la wapiga kura unaoratibiwa na Tume Huru ya Uchaguzj ( INEC ) kwa ajili ya uchaguzi wa Mkuu wa mwaka ujao
" Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa una orodha yake ya wapiga kura na uchaguzi ule wa kuchagua Diwani, Mbunge na Rais na wenyewe una daftari lake" amesisitiza Mhe Simbachawene
Kufuatia hatua hiyo Mhe.Simbachawene amewahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la uandikishaji linaloendelea nchi nzima huku akikisitiza kuwa yeyote ambaye hataweza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa hataweza kushiriki kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi Novemba 27 mwaka huu
Amesema uchaguzi huo ni muhimu sana kwani unawapa fursa wananchi kuchagua vuongozi wanaoishi nao kwenye mitaa na viongozi hao ndo msingi wa mchakato wa shughuli za maendeleo yanapoanzia.
" Msingi wa maendeleo ni watu, watu hao wakishirikishwa na wakiwa na viongozi wao na waliowachagua wataweza kupiga hatua za kimaendeleo kwani ndiko mawazo na ushirikishwaji wa mipango ya maendeleo yanapoanzia " amesisitiza Mhe.Simbachawene
Amewataka wananchi hao wajiandikishe ili 27 Novemba mwaka huu waweze kuchagua viongozi badala ya kuwa watazamaji na walalamikaji kwa kisingizio kuwa wao hawakuwachagua viongozi waliopo madarakani.
Zoezi hilo la kujiandikisha lilianza rasmi nchini kote kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka, huku rai kubwa ikitolewa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe akijiandikisha kwenye Daftari la Orodha ya Wapiga Kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kitongoji cha Pwaga , Kata ya Pwaga Mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇