WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka vijana wachangamkie fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia katika kujipatia kipato na kushiriki kukuza Uchumi wa Taifa.
Amesema kuwa vijana wanapaswa kutumia mitandao ya kidijitali kutafuta fursa za masoko na upatikanaji wa bidhaa ili kufanikisha malengo ya kuifanya Tanzania kuwa Taifa lenye maendeleo endelevu kupitia nguvu ya vijana na teknolojia.
Amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa uliyofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
“Dunia nzima ya leo inazungumzia matumizi ya kidijitali na matumizi haya ya kidigitali yanaenda kukabiliana na changamoto za karne ya 21, pamoja na kasi kubwa ya maendeleo duniani. Leo hii tunafanya manunuzi mtandaoni na hata fursa za biashara zinafanyika kidijitali. ”
Amesema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo katika sekta ya dijitali yanatoa fursa nyingi kwa vijana ambao wana nafasi kubwa ya kujiendeleza na kuleta maendeleo ya Taifa kwa kutumia kikamilifu ubunifu wao kupitia matumizi ya teknolojia mpya.
Ameongeza kuwa ili kufanikisha lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo na Malengo ya Maendeleo Endelevu, teknolojia za kidijitali zina nafasi muhimu ambazo kila mmoja anapaswa kuzichangamkia. “Teknolojia hizi siyo tu zinarahisha shughuli mbalimbali za kila siku katika maisha yetu, bali pia zinasaidia katika kufanya maamuzi yenye tija kwa kutumia mifumo mbalimbali ya kidijitali. ”
Pia, Waziri Mkuu amewataka vijana waendelee kuwa na matumaini na Serikali kwa kuwa imejipanga kuhakikisha inawafungulia fursa. “Endeleeni kuiunga mkono Serikali yenu kwa namna ambavyo imekuwa ikifungua milango ya fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya vijana, endeleeni kuhakikisha mnakuwa karibu na Serikali ili uweze kufikia ndoto yako kwenye maisha . ”
Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amewataka vijana watumie vizuri mifumo ya kidijitali. “Tutumie kwa matumizi mazuri yasiwe yanayoelekeza chuki, mgawanyo au mpasuko mkubwa katika nchi yetu, tuitumie ili ituwezeshe kufikia malengo makubwa tuliyonayo”.
Amesema kuwa dunia ya sasa ni ya Kidijitali ambayo inaitaka jamii kujua kwamba ili uweze kufanya jambo linalokwenda na kasi ya dunia ya leo ni lazima ujikite katika matumizi ya kidijitali.
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Mwita Maulid amesema kuwa wataendelea kusimamia maelekezo ya viongozi wa kitaifa ili vijana wawe mstari wa mbele katika kujiajiri na kuajiriwa na waweze kuchangia pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Lengo letu ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na vijana productive Barani Afrika na duniani kwa ujumla, kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamuunga mkono Rais Dkt. Samia ya kuendelea kuijenga Tanzania”.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa uliyofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Majaliwa akipata maelezo katika moja ya mabanda ya maonesho ya vijana.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇