LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 20, 2024

NEHEMIAH MCHECHU ACHANGISHA SH. MILIONI 117.8 UJENZI WA KANISA NAIBILI, SAME

Na MWandishi Maalum. Siha

Kiongozi Nehemiah Mchechu ambaye anajulikana kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya nyumba, benki na biashara, leo Jumapili Oktoba 20, 2024, ameendesha harambe iliyowezesha kupatikana Sh. milioni 117.8 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.

Kati ya fedha hizo kwa ajili ya jengo hilo mpya la ibada ambalo ujenzi wake ulianza miaka sita iliyopita, Sh milioni 50.2 ni taslimu, ahadi Sh milini 66.5 na Sh. milioni 1.1 zilipatikana kwa njia ya mnada na pia  katika harambee hiyo ilipatikana mifuko 118 ya saruji.

Kwa mujibu wa , Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT Dk. Fredrick Shoo fedha zilizochangwa pamoja na saruji ni kwa ajili ya upauzi wa jengo hilo la ibada na kazi ya plasta, ambavyo amesema  vinatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh. milioni 150.

Akizungumza na viongozi wa kidini, serikali na kijamii, pamoja na waumini wa Naibili, Mchechu alieleza haja ya kuendelea kuwa na moyo wa kutoa na kushirikiana mpaka ujenzi wa nyumba hiyo ya ibada utakapokamilika. Kwa sasa tayari jiwe la pembe limewekwa katika Kanisa hilo.

Mchechu aliwataka Wakristo kutoishia kwenye hatua hiyo ya kuweka Jiwe la Pembe tu.  “Tunapoendelea na ujenzi huu, nataka niwaombe ninyi wapendwa msiishie hapa. Tuendelee kufanya kazi kwa pamoja mpaka ujenzi utakapokamilika,” alisema na kuongeza;

“Kanisa bado linahitaji michango yenu, maombi yenu, na utayari wenu wa kujitoa. Kila mmoja wetu anaweza kutoa kitu, iwe ni fedha, muda, au huduma kwa namna yoyote ile.”

Alisema ikiwa watatoa kwa moyo wa upendo, Mungu atarudisha zaidi na zaidi na vikombe vyao vitafurika. Mchechu alisisitiza kwa kunukuu Biblia katika Luka 6:38: "Wapeni watu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa, cha kusukwasukwa, na kushindiliwa, na kufurika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu."


Aliongeza: “Kama vile Nehemia alivyowaongoza watu wa Yerusalemu kujenga tena ukuta wa mji baada ya kuharibiwa, ninyi pia muendelee kujitoa kwa uaminifu na bidii katika ujenzi wa nyumba ya Mungu.”

Kwa upande wa Dr. Shoo, alisema matamanio yao ni kuona wanakamilisha plasta, kuweka madirisha, milango na madhabahu, kupaka rangi na kuanza maandalizi ya kutengeneza samani, ifikapo mwaka 2026.

Mpaka kufikia hatua ya kabla ya upauzi, jumla ya kiasi cha Sh229.8 milioni kimetumika, shukrani kwa watu wenye mapenzi mema na Mungu kwa michango yao.

Askofu Shoo alisema baada ya upauzi na plasta, awamu ya pili ni kujenga madhabahu na madirisha na milango ya mbao.

Baada ya hapo awamu inayofuata itakuwa kuweka tarazo, bodi ya dari, kusuka umeme na rangi, huku awamu ya nne ikiwa ni kuweka viti na kumalizia madhabahu kwa kutumia mbao.

Awamu ya mwisho itakuwa ni kufunga vifaa  vya muziki, mifumo ya CCTV Kamera, kiyoyozi na mfumo wa TEHAMA. “Ni wakati mwafaka wa kushirikiana kufanya kazi hii ya baraka iliyopo mbele yetu. Mungu atutie nguvu” alihitimisha Askofu Shoo.

Mchechu akijadili jambo na Askofu Dk. Shoo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Mchechu akisalimiana na Askofu Dk. Shoo wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Mchechu akienesha habarambee katika hafla hiyo iliyofanyika leo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
Mchechu akipongezwa na familia baada ya hafla hiyo iliyofanyika leo, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.
 Ujenzi unaoendelea wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Naibili, Siha, Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages