Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Mhandisi, Daudi Sebyiga ameipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 15.7 kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vitongoji (HAMLET PROJECT II) kwenye vitongoji 75 vya majimbo matano (5) ya mkoa wa Rukwa ambapo Wateja wa awali wanatarajiwa kuunganishwa na huduma ya umeme watakuwa 2,475.
Akizungumza na Wanahabari ofisini kwake, Oktoba 15, 2024 wakati wa zoezi la kumtambulisha Mkandarasi anayetekeleza Mradi huo katika mkoa wa Rukwa, kampuni ya STEG International Services kutoka Tunisia; Kaimu Katibu Tawala wa mkoa, Mhandisi, Daudi Sebyiga amesema Mkoa wa Rukwa una vitongoji 1,816, kati ya hivyo vitongoji 1,175 vimepatiwa umeme katika miradi tofauti na kubakiwa na vitongoji 641 visivyo na umeme.
“Kwa sasa, Wakala wa Nishati Vijijini unatekeleza miradi ya ujazilizi katika mkoa wa Rukwa kupitia Wakandarasi wawili (2) wenye kufikisha umeme katika vitongoji 206 wilaya za Sumbawanga na Nkasi, 50 wilaya ya kalambo) kwa muda wa miaka miwili na kutegemewa kukamilika mwezi Novemba 2025 hivyo kupunguza idadi kutoka vitongoji 641 hadi vitongoji 435.” Amesema, Mhandisi, Sebyiga.
Viongozi wa REA; wakiongozwa na Msimamizi wa Miradi Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi, Dunstan Kalugira amemwambia Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa kuwa kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 75 vya mkoa huo ilianza rasmi tarehe 20 Agosti, 2024 baada ya REA kwa niaba ya Serikali kusaini mikataba na Wakandarasi kwa lengo la kusambaza umeme kwenye vitongoji zaidi ya 3,060 kote nchi ambapo kupitia Mradi huo, mkoa wa Rukwa umenufaika kwa kupata vitongji 75 ambavyo ni vitongoji 15 kwa kila Jimbo la uchaguzi la mkoa huo.
Majimbo hayo ni pamoja na Sumbawanga Mjini; Nkasi Kaskazini; NkasI Kusini; Kwela na Jimbo la Kalambo.
Mhandisi Kalugira amesema Wakala wa nishati vijijni (REA) unaendelea kutekeleza miradi mbalimbali nchi nzima pamoja na kuwasimamia kwa karibu Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza Miradi mbalimbali kuhakikisha Miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iwanufaishe Wananchi.
“Kwa sasa Wakala wa Nishati Vijijini, umeanza Mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 15 kwa kila jimbo kwa Tanzania Bara ambapo jumla ya vitongoji 3,060 vitafikishiwa nishati ya umeme; mkoa wa Rukwa, utanufaika na vitongoji 75 katika majimbo yote Matano. Mradi huu utatekelezwa na mkandarasi STEG INTERNATIONAL kwa muda wa miaka miwili kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 15.7.” Amekaririwa, Mhandisi Kalugira.
Naye Bwana Aymen Louhaichi; Meneja wa STEG International Services nchini amesema kampuni yao imekuwa ikitekeleza Miradi mbali mbali nchini na kwamba Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vitongoji vya mkoa wa Rukwa wataukeleza kwa mujibu wa mkataba na kwamba wamepanga kumaliza kabla ya kipindi cha mkataba (Miaka miwili).
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa, Mhandisi, Daudi Sebyiga (kushoto,akiishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi bilioni 15.7 kwa ajili ya kazi hiyo. Kulia ni kiongozi wa kampuni ya STEG International Services kutoka Tunisia itakayotekeleza miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇