LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 22, 2024

WAKATI TANZANIA IKIADHIMISHA SIKU YA FARU DUNIANI IDADI YA FARU WEUSI YAPAISHA ONGEZEKO LA FARU WEUSI

 Septemba 22, 2024 – Dodoma

Wakati leo Septemba 22, 2024 Tanzania inaungana na jumuiya za kimataifa kuadhimisha Siku ya Faru Duniani (World
Rhino Day), kutokana na juhudi mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi, Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi ya faru weusi kutoka 162 mwaka 2015 hadi 263 mwaka 2024.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa maadhimisho haya rasmi mwaka 2011 ni kutoa elimu na kukuza uelewa kwa
jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi faru duniani. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tujenge mazingira bora ya kuhifadhi faru
kwa wakati ujao: Siku hii inatukumbusha kuwa mipango ya pamoja, ubunifu, na uwajibikaji ni mambo muhimu katika
kuhakikisha uwepo na ustawi wa viumbe hawa adimu kwa vizazi vijavyo”

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara, Dk. Hassan Abbasi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana amesema, takwimu kutoka Shirika la Hifadhi ya Mazingira Duniani (International Union for Conservation of Nature– IUCN) na Kundi la Wataalamu wa Faru Afrika (African Rhino Specialist Group) zinaonyesha kuwa miaka ya 1960 kulikuwa na faru takribani 100,000 Barani Afrika ikijumuisha faru weupe na faru weusi.

Miaka ya 1970-1980 faru hao walipungua hadi 65,000 kutokana na ujangili. Tanzania tuna faru weusi pekee, ambapo miaka ya 1960 idadi yao ilikuwa takribani 10,000. Hata hivyo, kutokana na ujangili katika miaka 1980 na mwanzoni mwa 1990 idadi hiyo ilipungua hadi kufikia faru chini ya 100.

Chana amefafanua kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) inatekeleza Mradi wa Kupambana na Ujangili na
Biashara Haramu ya Nyara. Aidha, kupitia Mradi huu, Serikali imeandaa Mkakati wa Kupambana na Ujangili wa miaka
10 (2023-2033).

"Kuongezeka kwa faru nchini kutaiongezea Tanzania umaarufu kwa utalii wa faru. Ikumbukwe Utalii unachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato ghafi la Taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni. Aidha, utalii umetoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa watanzania zaidi ya milioni mbili. Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Tanzania (BoT) (Juni, 2024), Sekta ya Utalii imeendelea kuongoza nchini kwa kuliingizia Taifa fedha za kigeni ikifikia rekodi ya juu zaidi kuwahi kutokea ya dola bilioni 3.6. Kwa mujibu wa taarifa hiyo idadi ya watalii wa kimataifa wanaoingia nchini imefikia milioni 1.9 idadi ambayo haijawahi kufikiwa.

Hivyo, ili Tanzania iendelee kunufaika na mchango wa uhifadhi kupitia shughuli za utalii ni wajibu wa watanzania wote
kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita (6) inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu
Hassan katika kuhakikisha ujangili unatokomezwa hapa nchini. Wizara ya Maliasili na Utalii inawaasa wananchi kuwa
wazalendo na kutoa taarifa za ujangili kwa mamlaka zinazohusika pamoja vyombo vya dola.

Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania inachukua fursa hii kuwashukuru wananchi na wadau
wote wa uhifadhi nchini pamoja na jumuiya za kimataifa kwa ushirikiano wao wa dhati katika shughuli za uhifadhi wa
wanyamapori nchini Tanzania", imesema taarifa hiyo.


 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages