LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 22, 2024

MBEZI DARAJANI WAGOMA KUCHIMBWA MCHANGA MPAKA WAJENGEWE KINGO KUZUIA MMOMONYOKO PEMBEZONI MWA MTO, WAUKATAA MKATABA WA MKANDARASI WASEMA NI 'FEKI'

Na CCM's Official Blog, Kawe
Wananchi wa Mtaa wa Mbezi Beach A, eneo la Darajani, wamesisitiza msimamo wao wa kuitaka Kampuni ya  MEG Business Solution Ltd, inayotaka kuchimba mchanga katika mto Mbezi, eneo darajani kutoanza kufanya kazi hiyo hadi itimize takwa lao la kujengewa kingo imara itakayozuia mmomonyoko wa ardhi baada ya mchanga kuchibwa na hivyo kusababisa mafuriko kwenye makazi yao nyakati za mvua.

Msimamo wa wananchi hao, wameutoa leo, Septemba 22, 2024, wakati Kamati yao ya kuwawakilisha, ilipofanya kikao na Mkurugenzi Kampuni hiyo Emmanuel Lyimo, kikao ambacho kilifanyika kikiwa ni sehemu ya kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule aliyoyatoa  Agosti 14, 2024, ambapo aliitaka kampuni hiyo kusimamisha mara moja uchimbaji mchanga ambao ilikuwa imeuanza, kisha mchakato wa vibali urudi kwa wananchi.

DC Mtambule alilazimika kufika eneo Mbezi Darajani, baada ya Wananchi kuchachamaa na kuzuia uchimbaji  baada ya kuona kwa kustukizwa tingatinga likiwa mtoni kuandaa miundombinu ya kuchimba mchanga ikiwemo barabara ya muda iliyotemgenezwa kupitia eneo la JWTZ Lugalo hadi mtoni, na Agosti 2, 2024 uchimbaji ukaanza.

Hoja ya wananchi kupinga uchimbaji huo, mbali na kulalamikia kutoshirikishwa walisema wanahofia ungeathiri kingo za mto hivyo kusababisha mafuriko nyakati za mvua ambayo wanahofu yataweza kuwa makubwa zaidi kuliko yaliyowafika wakati wa mvua zilizopita.

DC Mtambule akiwa na maafisa mbalimbali wakiwemo wa TANROADS, NEMC, Idara ya Mazingira Manispaa ya Kinondoni na Mamlaka ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, pamoja na mambo mengine alitaka kujua kutoka kwa wananchi kwa nini wanazuia uchimbaji huo.

Kwa nyakati tofauti, wananchi walimueleza DC, hawapingi kufanyika uchimbaji, lakini hawaafiki uchimbaji huo kufanyika kwa kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato katika hatua za mwanzo kama inayopaswa kufanyika wakati inapofanyika miradi inayowagusa wananchi.

Walisema, hatua ya kutoshirikishwa katika hatua za awali kunawafanya wajawe na shaka kwamba uchimbaji mchanga mtoni utafanywa bila kuzingatia hatma ya mazingira ya eneo lao na makazi yao hasa kuhusu mafuriko.

Baada ya kusikiliza pande zote kwa takriban saa 2,  DC Mtambule, akasema, amebaini changamoto iliyokuwepo kubwa ni wananchi hao kutoshirikishwa, hivyo akaamuru mkandarasi kusimamisha kazi na kuondoa vifaa vyote mtoni ikiwemo tingatinga ili kuruhsu mchakato uanze upya kwa kurejeshwa kwa wananchi.

Kikao cha leo kinafuatia kile kilichoafnyika jana, Septemba 21, 2024 ambacho kiliitishwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kawe Husna Nondo ambaye alieleza kilikuwa cha kumtambulisha mkandarasi huyo, lakini kikaisha bila maelewano, hivyo akaelekeza Kamati ya Wananchi kukutana na kuzungumza na mkandarasi huyo.

Katika mazungumzo hayo ya leo, Lyimo alithibitisha kwamba Kampuni yake haiwezi kumudu sharti la kujenga kingo ya kiwango cha mawe wananchotaka wananchi hao akidai gharama ya ujenzi huo ni kubwa. "Mkataba tuliopewa ni wa kushughulikia eneo la mita 50, sasa mahitaji yenu ni makubwa kuliko mradi wenyewe", akasema Lyimo.

Wakati Lyimo akisisitiza Kampuni yake kuwa ina Mkataba wa Mamlaka ya Bonde la Wami/Ruvu (WRBWB) baadhi ya Wajumbe walisema wananchi hawawezi kuutambua mkataba huo kwa kuwa uliingiwa wakati ambao mchakato ulikuwa haujapitia kwa wananchi hivyo wakasema ikiwa maafikiano yatafikiwa itabidi uingiwe mkataba mpya.

Kwa mujibu wa mkataba ambao Lyimo alisema kampuni yake inao, ulionyesha kuanza kusainiwa Agosti 2, 2024 na kutakiwa kuanza kutumika hiyohiyo Agosti 2, 2024 na kudumu hadi  Novemba 2, 2024.

Hata hivyo licha ya mkataba huo kuonyesha kuanza Agosti 2, 2024, siku uliposainiwa, unaoyesha kuwa ulisainiwa kwa nyakati tofauti, kwa kuwa wakati Mkurugenzi wa Wami/Ruvu Adria Massawe alisaini Agosti 2, 2024, Mkurugenzi wa MEG Bussiness Solution Ltd alisaini kesho yake, Agosti 3, 2024'

Halikadhalika, wakati Mwenyekiti wa Kamati Kamati ya Mazingira Mtaa wa Ukwamani Farasi Mng'ndilo akisaini siku ya tatu (Agosti 4, 2024) naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Mtaa wa Mbezi Beach A, Caroline Mgoda akisaini siku ya nne (Agosti 5, 2024).

Mkurugenzi wa Kampuni ya MEG Business Solution Ltd Emmanuel Lyimo (kulia) akizungumza na Kamati ya Wananchi wa Mbezi Beachi A, Darajani.

Mjumbe akimuuliza hoja, mkandarasi huyo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages