LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 17, 2024

AMIRIJESHI MKUU RAIS DK. SAMIA AFUNGUKA, TANZANIA NI NCHI HURU INAJUA CHA KUFANYA KUHUSU MATUKIO YANAYOTOKEA NCHINI

Moshi, Septemba 17, 2024
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amejibu matamko yaliyotolewa na mabalozi wanaowakilisha mataifa mbalimbali nchini, waliyotaka uchunguzi wa haraka kufanyika kuhusiana na matukio ya utekaji na mauaji ya watu, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi huru na haipaswi kuelekezwa cha kufanya katika masuala yake ya ndani.

Baada ya Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ali Kibao, kupatikana amefariki huko Ununio, Dar es Salaam, mabalozi wa nchi mbalimbali, zikiwemo Marekani, Ufaransa, na Umoja wa Ulaya (EU), walijitokeza kulaani tukio hilo na kuitaka Serikali ya Tanzania kufanya uchunguzi wa haraka.

Akizungumza leo, Septemba 17, 2024, kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Polisi Moshi, Rais Samia alisisitiza kwamba mauaji hayo hayakubaliki kwa sababu yoyote ile.

“Natumia kofia ya Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii kusema kwamba tumeapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na tutaendelea kufanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha ya Watanzania, kwa kuwa ni jukumu letu.

“Kuhusu wajibu huu, hatuhitaji kuelekezwa na mtu yeyote nini cha kufanya kwa sababu katiba yetu inatoa maelekezo yote jinsi ya kuendesha serikali. Na hakuna mtu anayeumia zaidi ya Watanzania pale haya yanapotokea. Hatukubaliani nayo, tunaumia sana kuona haya yanatokea… Kifo chochote kinatuuma Watanzania. Hii ni damu yetu.”

Rais Samia pia aliwataka mabalozi na nchi za nje kuonesha huruma zao kwa kuzingatia makubaliano ya kidiplomasia ya kimataifa kama yalivyoainishwa kwenye “Vienna Convention on Diplomatic Relations” ya mwaka 1961.

“Tamko lililotoka likituambia tufanye moja, mbili, tatu, sisi tunajua cha kufanya kama nchi huru. Ni imani yangu kuwa tamko hilo halikutolewa na viongozi wakuu wa mataifa hayo. Kwa sababu nina njia ya kuwasiliana na marais wenzangu ili kuthibitisha kama kweli walitoa maelekezo hayo, na kama sivyo, nitawasilisha malalamiko yangu kwao.”

Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania inajiongoza kwa katiba, sheria, mila na desturi zake, na si lazima kuelekezwa nini cha kufanya.

“Mambo kama haya yanatokea kila nchi, si Tanzania pekee. Inapotokea kwetu, inauma, lakini matukio haya siyo ya kipekee kwetu. Kila mahali kuna changamoto kama hizi. Kwa mfano, utaona mtoto kachukua bunduki, kenda shuleni na kuwaua wenzake. Haya yanatokea kwa njia mbalimbali,” alihitimisha Rais Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali wa Jeshi la Polisi kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa mwaka wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi hilo uliofanyika katika Shule ya Polisi Tanzania (TPS)
Moshi Mkoani Kilimanjaro tarehe 17 Septemba, 2024.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages