Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi leo anafanya mkutano mkubwa wa hadhara Uwanja wa Mayunga Bukoba Mjini ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya siku 6 mkoani Kagera.
Jana DK. Nchimbi amefanya mkutano wenye mafanikio katika Wilaya ya Misenyi na kusalimia wananchi eneo la Katoma Jimbo la Bukoba Vijijini ambapo alipata wasaa wa kutatua kero mbalimbali za wananchi zilizowasilishwa kwake na Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Jasson Rweikiza.
Katika mkutano wa Misenyi uliofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Kyaka aliagiza serikali kuwasaka na kuwakamata watu wote wanaoratibu na kudhuru watu wenye ualbino na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha, ameendelea kutoa agizo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuongeza kasi ya kuwapatia wananchi vitambulisho vya Taifa (Kadi za NIDA) hasa baada ya changamoto hiyo kujitokeza karibu katika mikutano yote aliyoifanya tangu aanze ziara mkoani Kigoma.
Ameeleza kuwa malengo ya ziara hiyo ni; Kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, kuhuisha uhai wa chama, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhakiki taarifa zao na kujiandikisha katika Kitabu cha Kudumu cha Wapiga kura, kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇