LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 21, 2024

WAKILI MKUU WA SERIKALI DK. POSSI AKABIDHIWA OFISI

Dar es Salaam
Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi amekabidhiwa Ofisi na mtangulizi wake aliyeshika nafasi hiyo, Dk. Boniphace Luhende, juzi Agosti 19, 2024 Makao Makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.

Dk. Possi aliteuliwa  na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan Agosti 14, 2024 kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na kuapishwa Agosti 15, 2024.

“Wewe ni mtangulizi wangu, uliwahi kuongoza Ofisi hii kipindi kilichopita ukiwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na sasa umerejea kuongoza Ofisi hii ukiwa Wakili Mkuu wa Serikali, hapa ni nyumbani, ofisi hii unaifahamu.

Nakupongeza kwa kuteuliwa na kuaminiwa na Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hii, nami niko tayari kukupa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yako,” amesema Dk. Luhende.

Katika makabidhiano hayo, Dk. Luhende alimkabidhi Dk. Possi nyaraka mbali mbali za uendeshaji wa Ofisi ikiwemo Katiba ya Tanzania ambayo ni sheria mama ya nchi na taarifa ya mashauri yanayoendeshwa na Ofisi hii ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo ya uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi ya ndani na nje ya nchi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake.

Akipokea nyaraka hizo, Dk. Possi alimshukuru Dk. Luhende kwa makabidhiano ya Ofisi ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa mujibu wa dhamana waliyokasimiwa na Serikali na amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kumuamini na kumteua kushika nafasi hiyo na yuko tayari kushirikiana na Menejimenti ya Ofisi hiyo, watumishi na wadau kutekeleza majukumu ya Ofisi kwa niaba ya Serikali katika kuhudumia wananchi.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo ambaye amewapongeza viongozi hao na kuwatakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu kwa kila mmoja kwa nafasi yake katika kuendeleza gurudumu la maendeleo.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi (kushoto) akipokea nyaraka za makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Boniphace Luhende, baada ya kukabidhiwa Ofisi kwenye hafla iliyofanyika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam, juzi.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi (kushoto) akizungumza na aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Boniphace Luhende, kabla ya kukabidhiwa Ofisi kwenye hafla iliyofanyika kwenye Ofisi hiyo Jijini Dar es Salaam, juzi.

Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi (katikati) akiwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Alice Mtulo, baada ya kukabidhiwa Ofisi na aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Boniphace Luhende. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages