Na HEMEDI MUNGA, Uyui
MAKAMU Mwenyekiti wa Machifu mkoa wa Tabora ambae ni Chifu wa Himaya ya Usongo Igunga, Nshoma Haiwa amewapongeza Viongozi mbalimbali akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Selwa Abdalla Hamid kwa kazi nzuri iliyofanikisha miradi yote iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2024 kukubalika kikamilifu.
Chifu Nshoma ametoa pongezi hizo katika uwanja wa Chuo cha VETA Idete wilayani Uyui baada ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya wilaya hiyo na Igunga mkoani hapa.
Aidha, amesema uchapakazi wa watendaji wa Halmashauri hiyo unakwenda sanjari na moja ya Tafsiri ya jina la Chifu Hangaya ambalo ni jina la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiwa Chifu namba moja na mwenye falsafa ya Kazi Iendelee.
"Hangaya kwa lugha ya Kisukuma "alehangaya" inamaana ya Nyota inayongaa ambayo huonekana nyakati za alfajiri," ameeleza na kuongeza kuwa :
"Hua mnasikia Mama akisema kazi iendelee, hivyo kama mfano kwa wakulima
huondoka mapema alfajiri kwenda shamba."
Amesema halikadhalika kwa upande wa watumishi hua wanatoka mapema kwenda kazini kuendelea na shughuli mbalimbali za kuendelea kulijenga Taifa.
"Hakika ni Nyota inayongaa maana hata Watumishi Mbalimbali huamka na kujiandaa nyakati za alfajiri kwenda kazini."amesema.
Mbali na hayo, ameweka wazi kuwa alishiriki kumvika ngozi ya Chui Rais Dk. Samia ikiwa ni ishara ya kuendeleza ulinzi wa nchi yake.
Aidha, amesimulia kuwa alilifanya zoezi hilo katika Tamasha la Utamaduni lililofanyika jijini Mwanza mwaka 2021.
Katika hatua nyingine, Chifu Nshoma amebainisha furaha aliyokua nayo ya kupata picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambayo imetajwa kuwa ni ishara ya kuwapa baraka.
Amefafanua kuwa baada ya Mkuu wa wilaya hiyo, Sauda Mtondoo kuukabidhi Mwenge wa Uhuru wilayani Uyui, alikuja na Kumkumbatia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Abdalla Hamid.
"Namimi nilimkumbatia kulia na kushoto huku nikimnongoneza kuwa tumemaliza Mwenge wa Uhuru Salama," amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo inaendelea kuonesha ishara ya mshikamano, ushirikiano na upendo ambao utaendelea kuhakikisha gurudumu la maaendeleo linaendelea kupaa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇