LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 11, 2024

BABA HALISI AACHILIA KITABU: HUDUMA YA KANISA HALISI INAVYOFANYA SAFU

 NA BASHIR NKOROMO, DAR ES SALAAM
Kanisa Halisi lilianzia Tanzania mwaka 2018, na hadi sasa limekuwa na mamilioni ya wafuasi kupitia vituo vyake zaidi ya 300 hapa Tanzania, likiwa pia na vituo katika mataifa ya Kenya, Uganda, Congo DRC, Burundi, Rwanda, Zambia, Msumbiji, Malawi na Boston nchini Marekani.

Ukweli wa Kanisa Halisi kuwa na mamilioni ya wafuasi unatokana na idadi ya Uzao wake waliopo katika vituo hivyo zaidi ya 300 hapa nchini na vile vilivyoko mataifa hayo tisa ya nje, sanjari na ambao hufuatilia Ibada za Kanisa hilo kupitia 'Online tv' hata katika mataifa ambako bado halijaweka vituo pia usisahau kuwa baadhi ya wenye dini na madhehebu tofauti nao hulifuatilia Kanisa hilo kwa sababu moja au nyingine.

Unaweza kujiuliza, ikiwa Kanisa Halisi, lina miaka ambayo siyo mingi ukilinganisha na makalisa yaliyotangulia, ni kitu gani kimelifanya kuchanua ndani na nje ya Tanzania hadi kufikia kuwa na wafuasi wengi kiasi hicho? Majibu ni mengi, lakini kwa maoni yangu limechanua na kupata wafuasi wengi kutokana na mafundisho yake ya kipekee ambayo huhubiriwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, Baba Halisi.

Katika Ibada iliyofanyika Makao Makuu ya Kanisa Halisi, Tegeta Namanga, Dar es Salaam, Kiongozi Mkuu ameachilia kitabu ambacho kinaeleza kwa kina jinsi huduma ya Kanisa Halisi inavyofanya safu (inafyofanya kazi).

Msimamizi Mkuu wa Blog hii naye alibahatika kukipata kitabu hicho ambacho Uzao waligawiwa baada ya Baba Halisi kuwafafanulia yaliyomo na kwa nini amekiandika.

Kitabu hicho chenye kurasa 16, kwa hakika ukikisoma utapata majibu halisi kuhusu Kanisa Halisi, tunakuwekea hapa kama tulivyokipokea; Tafadhali kisome👇


HUDUMA YA KANISA HALISI INAVYOFANYA SAFU

UFUNGUO
Wengi wamekuwa wepesi kudanganywa na waovu wasiopenda kweli ya MUUMBA WA KILA KITU inayofundishwa Kanisa Halisi, kwa kuwa hawaelewi vizuri Huduma ya Kanisa Halisi inavyofanya kazi. Kujua habari za waliotumwa peke yake ndiko kulikokuwa kunasababisha kutoelewa vizuri Huduma ya Kanisa Halisi. Aidha, wengi walidhani kila walichofundishwa zamani ni sahihi na hakuna zaidi ya hapo, kumbe sivyo. Sasa nafafanua ni kwa jinsi gani Huduma ya Kanisa Halisi ilivyo ili udanganyifu usiendelee tena.

1. Kanisa Halisi Linamwabudu Aliyeumba, Siyo Mwana
Katika Rumi 10:4, iliandikwa kuwa mwisho wa sheria ni Kristo. Lakini kweli ni kwamba aliye juu ya kila kitu ni CHANZO HALISI ambaye Rum 11:36, inasema kila kitu kilitoka kwake na kitarudi kwake pia. Aidha, Kolosai 1:17 a+b, inasema kuwa alikuwepo kabla ya kitu chochote na kwamba kila kitu kimeshikana katika yeye.

Huyu MUUMBA ambaye alikuwepo kabla ya kitu chochote na ambaye kila kitu kimerudi kwake, baada ya Majira kufika, ndiye anayeabudiwa maana alituumba ili tumwabudu. Kweli iliyopo ni kwamba hakuna mtume wala nabii ambaye aliumba kitu chochote. Hili ni lazima sote tulikubali. Ndiyo maana Kanisa Halisi tunamwabudu aliyeuumba. Maana mwana alisema atakuwa pamoja na Kanisa hadi ukamilifu wa dahari yake, yaani majira yake (Mathayo 28:20). Huo ukamilifu wa dahari ya mwana ulitimia Mwaka 2017.


Lakini pia, tusisahau kuwa katika Yohana 17:2-5, Mwana alikabidhi kazi baada ya kutimiza alichokuwa ametumwa na akaomba kurudi kwenye hali aliyokuwa nayo zamani kabla ya kuja kupitia kinywa cha Malaika Gabrieli (Luka 1:26-28). Kwa hiyo, kumwabudu CHANZO HALISI aliyeumba ni sahihi na ni majira yake pia. Hivyo, kwa waliokuwa wanajua na wale waliokuwa hawajui sasa ni vema sote tuelewe.

2. Kanisa Halisi linasisitiza Upendo Uliopitiliza ili kufuta mauti.

Katika 1Kor 13:13, iliandikwa kuwa kuna imani, tumaini na upendo na kwamba katika hayo matatu lililokuu ni upendo. Tatizo lilikuwa katika Wimbo Uliobora 8:6, ambayo inasema kuwa upendo una nguvu kama mauti! Hapo ni sawa na kusema kuwa upendo ni sawasawa na mauti! Ukisema upendo peke yake haitoshi maana utashindana na mauti. Na upendo wenyewe wakati wa majira saba haukuwepo maana ulichukuliwa na ufunuo, nyoka na uzao wake.

Hivyo, Kanisa Halisi lina UPENDO ULIOPITILIZA ili kuishinda mauti (IKorintho 15:26). Ndiyo maana tunainua viongozi walioko madarakani bila wao wenyewe kutuomba. Aidha, tunainua jamii na uumbaji wote bila kushawishiwa na yoyote, kwa kuwa huo ndio Upendo Uliopitiliza unaoshinda mauti. Ukiishia kwenye upendo peke yake haitoshi. Pia, hata tukishtakiwa na kuzushiwa uongo hatulalamiki wala kunung’unika kwa kuwa tuna Upendo Uliopitiliza ili kushinda mauti.

3. Kanisa Halisi lina Ufahamu na Uelewa wa Sauti ya CHANZO HALISI

Ufahamu uliokuwepo katika majira zote saba, ambao ndio unaotumiwa na ambao hawajampokea CHANZO HALISI, ni ule wa 2Korintho 4:6, yaani nuru itokayo gizani. Ufahamu huo haukubaliani na Sauti ya CHANZO HALISI kwa kuwa dunia ndio waliomvua vazi/ufahamu Adamu wa Kwanza (Mwa. 3:7-8). Nuhu (Mwa. 9:20-22); na Yesu (Yoh.19:23-24). Hivyo, walikuwa hawataki tena ufahamu wa Nuru Nuruni (Isaya 60:1-3).

 
Kanisa Halisi, tunatumia ufahamu na uelewa wa Sauti iliyosikika Tanzania ambao ndio uliohamisha ufalme kutoka Mashariki ya Kati kuja Mashariki Halisi (Isaya 41:2,4).

Katika Kutoka 19:5, iliandikwa kwamba ukiwa na ufahamu na uelewa wa Sauti unakuwa juu ya makabila yote ya dunia na baraka zinaamuriwa kukufuata (Kumb 28:1-14). Lakini ukiwa huna ufahamu na uelewa wa sauti, utakuwa na njaa, ukame na jangwa. Tukubali kuwa majira iliyoandikwa katika Ufunuo 21:9-10, ilishafika na kupita. Hivyo, sote tupokee ufahamu na uelewa wa Sauti ya CHANZO HALISI.

4.  Kanisa Halisi Linaishi Majira na Wakati kabla ya Uharibifu, Siyo Majira ya Waliotumwa

Katika 2 Sam 7:10-11, iliandikwa kuwa wakati ukifika, MUUMBA ataliweka Kanisa mahali pake ambapo wana wa uovu hawatalitesa tena kama zamani (yaani, kama kipindi cha majira saba). Katika majira saba zilizopita watendao kwa haki ilikuwa ni utumwa tu, tena walikuwa wanaenda utumwani kabla ya kuzaliwa (Mwa 15:8-15). Sasa tunaishi kwenye hii majira kabla ya uharibifu, kwa kuwa uteka wa mwenye haki umegeuzwa baada ya Kiti cha Haki na Fimbo ya CHANZO HALISI kupatikana.

5.  Kanisa Halisi Tuna Huduma ya Uhai, Siyo Mauti

Katika Hosea 13:14, kitabu kiliandika kuwa CHANZO HALISI akija, atatukomboa na nguvu za kaburi. Hii ndiyo inayoitwa Huduma ya Uhai bila mauti, kama inavyofafanua katika 1Korintho15:51, hatutalala sote bali sote tutabadilika. Katika Isaya 53:1-5, ndipo panapofafanua ni kwa jinsi gani huduma katika majira saba ilivyokuwa ya mauti (2kor 3:7). Maana kila atendaye Haki alikuwa ni fidia ya uovu. Hakutakiwa kuambiwa asante kwa kazi njema aliyofanya kwa kuwa alihesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa mchana kutwa (Rumi 8:36).

Kanisa Halisi hatusemi tena tumeokoka, bali tumekombolewa na nguvu ya mauti kwa kuwa ndicho kilichomleta CHANZO HALISI. Ukombozi ni zaidi ya wokovu, maana Ukombozi ina maana unayemtoa baharini (akiwa amezama), unamtoa akiwa hai na wewe ukiwa hai. ila kwenye kituo cha wokovu, unayemtoa baharini hatoki na wewe unayeokoa unaishia baharini pia! Hivyo, katika majira zote ambazo tulizokuwa tunasema kuwa kuna wokovu hakuna aliyevuka mto usiovukika (Ezekiel 47:1-5). Ila sasa tumevuka ule mto usiovukika (Ufunuo 22:18-19).

6. Kanisa Halisi lina Utajirisho siyo Madhabahu

Utajirisho uliishia pale alipotekwa Moyo wa Mwanzo (Ufunuo 12:1-10). Maana utajirisho ni Mema na Mazuri peke yake, wakati madhabahu ni mema na mabaya (Kumb 30:15). Katika Mith 3:16 (a), CHANZO HALISI aliweka kwenye Moyo wa Mwanzo Heshima na Utajiri siyo umaskini na aibu au fedheha ambayo mwenye haki alikuwa anaonekana anayo. Kilichosababisha aibu na fedheha katika Maisha ya mwenye haki, ni madhabahu. Msomaji aelewe vizuri kuwa madhabahu siyo ya CHANZO HALISI. CHANZO HALISI yeye ni Utajirisho peke yake. Hivyo, Kanisa Halisi limesimama kwenye Utajirisho.
 
7. Kanisa Halisi Tuna Ibada ni Uzalishaji, Siyo Kilio na Maombolezo.

 
Katika majira saba, baada ya utumishi na utumwa mgumu, ibada iligeuka kilio na maombolezo. Hii ilisabisha nabii Yeremia aandike kuwa ‘‘nitafutieni wanawake waombolezaji’’ (Yer.9:17) maana aliona mateso yamezidi baada ya kutupwa shimoni. Daudi, katika kitabu cha zaburi, alifundisha kulia na kuomboleza kuliko yeyote, maana ndiyo iliyokuwa ibada ya majira saba zilizopita. Sasa CHANZO HALISI amekuja kuishi ndani ya moyo wa kila atendaye kwa Haki ili tusilie tena wala kuomboleza (Isaya 57:15).

Kwa kuwa CHANZO HALISI ndiye aliyekuwa wa kwanza kufanya kazi kwa mujibu wa 1Korintho 12:4-7, na anaonekana kwa sura ya kila atendaye kwa haki, basi sasa Ibada ni Uzalishaji. Tunakuja kwenye nyumba ya ibada kushukuru yale tuliyotendewa kazini ili CHANZO HALISI azidi kutuzidisha na kutuongeza.

8.  Kanisa Halisi Lina Safu Siyo Cheo.

Katika Yoeli 2:6-8, kitabu kinasema Kanisa linatakiwa kujipanga kwa namna ambayo hakuna anayepotosha Safu yake aliyopewa. Kwenye safu inawezekana kuwa hivyo, ila mahali ambapo kuna cheo haiwezekani kutopotosha safu kwa kuwa cheo unafanya kazi kwa kusimamiwa na nyampara. Msimamizi asipokukagua huna sababu ya kufanya vizuri.
Kwa upande wa Safu anayefanya kazi ni CHANZO HALISI ambaye anakuwa ndani ya Moyo wako (Ufunuo 22:3-4). Kwa kuwa kiti cha Haki ni kimoja na kinakuwa ndani ya Moyo wa Uzao Halisi na Watekeleza Sauti Halisi wote, Safu inawezekana na hakuna ambaye anafanya kazi kwa kushurutishwa. Hapo ndipo huduma ya Kanisa Halisi inapofanyia kazi.

9. Kanisa Halisi Tuna Matunda, Siyo Sadaka

Katika Mwa 22:1-15, Ibrahimu alimtoa Isaka sadaka baadaye ikawa ni mila na desturi ya dunia na ulimwengu kufanya wenye haki kuwa fidia ya waovu. Jambo hilo limetesa Jamii kwa kuwa iligeuka kuwa desturi ya watu wote weupe, weusi, wekundu kila Taifa na katika kila Bara.

Kwa mantiki hiyo Kanisa Halisi hatuna sadaka, bali tuna Matunda. Maana hata waganga wana sadaka. Katika Mathayo 21:43, tunasoma kuwa CHANZO HALISI amefuata Matunda siyo sadaka. Matunda ya kwanza ni Uzao Halisi na Watekeleza Sauti Halisi. kila kinachoitwa kwa jina la uzao/ watekeleza sauti Halisi ni Matunda ya CHANZO HALISI pia (fedha, dhahabu, majumba, magari, mashamba, viwanja, na kadhalika).


10. Kanisa Halisi Tunashukuru, Siyo Kuomba

Hatuombi kwa kuwa Lugha inayoeleweka kwa CHANZO HALISI ni Shukrani. Waliotumwa hawakupata ufahamu wa kushukuru, ndipo milango ikafungwa na kongwa la chuma likakaa shingoni (Kumb 28;47-48). Yesu, katika Yoh.6:11-13 na Yoh. 11:44-45, alishukuru kidogo tu maongezeko na ufufuo wa Lazaro ukatokea! Katika Zaburi 100:4, kitabu kinasema ukishukuru milango inafunguliwa.

Maombi yalikuwa ya Ishara ya kwanza mbinguni (Ufunuo 12:1)! Huyu ndiye aliyekuwa anapokea maombi. Sasa tuna majira na wakati wa CHANZO HALISI ambaye lugha yake ni Shukrani. Hapa ndipo Huduma ya Kanisa Halisi ilipo.

11. Kanisa Halisi Tuna Msamaha Bure, Siyo Sala ya Toba

Katika Isaya 43:25, kitabu kimeweka wazi kuwa, majira na wakati wa CHANZO HALISI atatusamehe bure kwa ajili yake yeye mwenyewe. Maana kila mmoja alikuwa nje ya reli! Aidha, hakuna aliyewahi kufanya Toba Halisi, ambayo ingefuta ‘‘GAP’’ ambalo lilikuwepo katika majira zote saba kati ya CHANZO HALISI na Kanisa. Ni kweli Petro alihimiza toba ili nyakati za kuburudishwa zije (Mdo 3:19), lakini haikuwezekana.

Hii ndiyo sababu katika majira zote, tulienda mbele za CHANZO HALISI tukiwa wachafu (Zek 3:3-7). Si hivyo tu, katika Ezekieli 16:1-10, hata kwa kuzaliwa bado kila mmoja alionekana ni mchafu ingawa kusudi la CHANZO HALISI lilikuwa ni uzaliwe ukiwa umetakaswa (Yer 1:5). Zaidi, Daudi alijaribu kutubu mwenyewe katika Zab 51:1-5, lakini dhambi yake ikaendelea kuonekana mbele zake. Suluhisho ni kuupokea msamaha bure.  CHANZO HALISI amekuja na msamaha bure, tafadhali upokee huo msamaha bure.


12. Kanisa Halisi Tuna Toba ya Hiari ya Moyo, Utakaso na Haki, Siyo Kusimama Palipobomoka

Katika Ezekieli 22:30, kila mwenye upendo wa kiwango cha majira saba alitakiwa kusimama palipobomoka kwa ajili ya wengine, ili Mungu wa majira saba asiangamize. Mstari huu hauna tofauti na 2 Nyakati 7:14-16, kifungu ambacho kinasema kuwa; ikiwa walioitwa kwa jina la Mungu wa majira saba wataomba na kutubu kwa ajili ya wengine, basi atasamehe mji huo uliokuwa umekosea na macho yake yataangalia hapo daima. Shida iliyokuwa inatokea katika majira zote ni kwamba, kila aliyesimama kwa niaba ya wengine, aliangamia (wale walioombewa walipona). Hilo ndilo tatizo la kusimama palipo bomoka.

Kanisa Halisi tuna Toba ya Hiari ya Moyo, Utakaso na Haki, ikiwa na maana kuwa aliyetubu siyo wewe ambaye kinywa chako kimetumika, bali ni CHANZO HALISI aliyeko ndani yako. Kwa jinsi Kanisa Halisi tunavyoinua Jamii na walioko Madarakani kila lango, basi tungeangamia zaidi kuliko wengine wote. Hivyo, inua Toba ya Hiari ya Moyo, Utakaso na Haki kwa ajili ya mwengine, siyo kusimama palipobomoka.

13. Kanisa Halisi Tuna Lango, Siyo Siku

Katika Efeso 6:13, kuna siku ya uovu. Hata kama ni mtakatifu kiasi gani, kipindi cha majira saba, ilikuwa ni lazima ukutane na hiyo siku ya uovu (ambayo kuanzia asubuhi hadi jioni ilikuwa nikukutana na mikosi balaa na nuksi tu, hata kama uko kwenye mfungo)!

Kwenye mfumo wa Lango, ni mema na mazuri tu ambayo unatakiwa kukutana nayo. Aidha, siku zilibadilishwa, badala ya mwezi kuwa na siku 28; ukawa na siku ya 29,30 na ya 31!


14. Kanisa Halisi Tunatumia Mamlaka ya Damu Safi Nyeupe, Siyo Damu ya Mwana

Kwa mahali tulipo sasa, ukikutana na mapepo, majini, vinyamkera na kila shida ukatumia damu ya Mwana, hao maadui wanakudhihaki (kwa kuwa walikuwa wanajua mahali mwana alipo-Efeso 2:5-8).

Tunatumia mamlaka ya Damu Safi Nyeupe kwa kuwa hii ni ya CHANZO HALISI ambaye majira yake ya kuabudiwa ni sasa. Aidha, ni kile kibali tulichopewa katika Ufunuo 11:6 cha kugeuza maji kuwa Damu. Katika (Mathayo 26:29), Yesu alisema Jambo kubwa baada ya kuwapatia wanafunzi wake damu ya ukumbusho. Alisema kuwa yeye hawezi kunywa tena ile damu ya ukumbusho kwa kuwa alikuwa anajua walichomfanyia msalabani. Mamlaka aliyokuwa amekuja nayo Yesu (Efeso 1:21), walichukua katika ile damu iliyomwagika msalabani na maji yakatoka ubavuni (Yoh 19 :34). Majira hii mamlaka ya kushinda mabaya iko katika Damu Safi Nyeupe.

15. Kanisa Halisi Tunaishi Uhalisia wa Moyo, Siyo Katika Ulimwengu wa Roho

Katika Efeso 1:3, iliandikwa kuwa baraka zetu zote zilikuwa rohoni. Ni kwa kuwa katika kipindi chote cha majira saba aliyekuwa mtawala ni roho na nafsi (Rumi 8:23). Katika hali kama hiyo, tulikuwa tunahimizana kukaa rohoni ambapo kwa macho hapaonekani. Pamoja na kuhimizana kukaa rohoni, wengine hatukujua hata maana ya kukaa rohoni ni kitu gani. Waovu (wachawi, waganga, wapunga upepo na waruka kwa ungo, na kadhalika) ndio hasa walikaa rohoni! Maana mtu ulikuwa unaona mko naye kwa muonekano, lakini kumbe amehamia yuko mji mwingine kabisa anahudhuria kikao! Kanisa Halisi hatuishi kwa jinsi hiyo, bali tunaishi tukiwa Halisi kuwa ukiniona nacheka, basi hata Moyoni nacheka. Ukinona nimefurahi hata moyoni nimefurahi. Hiyo, nitofauti na wale waliokuwa wanaishi rohoni, anaweza kukulamba miguu kwa ulimi (akimaanisha anakupenda) lakini kumbe anakuchukia kuliko wote.

16. Kanisa Halisi Tunafanya Kazi na Jamii na Taifa kwa Ujumla

Wakati wa majira saba Musa, aliyekuwa nabii wa kwanza katika vizazi vinne vya Ibrahimu, hakufanya kazi na Mfalme Farao! Halikadhalika Eliya Mtishbi aliyekuwa nabii wa pili katika vizazi vinne vya Ibrahimu, hakufanya kazi na Mfalme Ahabu wa Israel. Yesu nabii wa kizazi cha tatu katika vizazi  vinne vya Ibrahimu, naye pia hakufanya kazi na Mfalme Herode. Huu ndio msingi uliokuwepo ambao Kanisa Halisi tumeukataa.

Kanisa Halisi tunafanya kazi na Jamii na Taifa kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii (Mdo 2:47). Kwa mijibu wa 1Timotheo 2:1-4, tukiwainua walioko madarakani tunaishi kwa amani na utulivu. Aidha, tukifanya kazi na Jamii, tumepata baraka za kupitiliza (Isaya 58:7-11). Hivyo, hakuna kinachotuzuia kufanya kazi na Jamii na Taifa  kwa kuwa huo ndio mwongozo wa CHANZO HALISI.

17. Kanisa Halisi Tunabatizwa kwa Sauti Halisi

Katika (Rum 6:1-4), kitabu kinaonyesha kuwa ubatizo ni kufa na kufufuka na Kristo. Zaidi, ubatizo unataka ukifufuka (yaani ukitoka kuzamishwa katika maji), ufufuke kwa upya wa uzima.

Katika majira zote zilizopita, Suleimani aliandika katika (Mhubiri 1:9) kuwa jipya halikuwahi kuwepo. Ubatizo ulianza wakati wa majira ya Yesu, ili badiliko litokee, lakini halikutokea. Halikutokea kwa kuwa tatizo halikuanzia karibu, lilianzia kwa yule wa kwanza kuachiliwa na CHANZO HALISI hata kabla ya Kerubi katika (Eze 28:15), kuwepo.

Tatizo hili ambalo mitume na manabii wa kizazi cha tatu, walidhani wengeweza kuliondoa kwa kufanya, kama Yesu alivyofanya katika (Math 3:15), halikutoka. Halikutoka kwa kuwa lilihitaji CHANZO HALISI aje mwenyewe juu ya nchi.

CHANZO HALISI ni Sauti Halisi na kwa Sauti Halisi kweli tumebadila kabisa. Ndiyo maana iliandikwa katika (1kor 2:9-19), yapo ambayo sasa yatafanyika (ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio halijawahi kuhifadhi ndani ya moyo wa yeyote). Ni hivyo, kwa kuwa sasa CHANZO HALISI ambaye alikuwepo kabla ya roho, nafsi na mauti amekuja ili aondoe hivyo ndani yetu. Kwa ubatizo wa maji, roho, nafsi, mwili, asili, mauti n.k havikutoka ndani yetu.Ndiyo maana ubatizo wa Kanisa Halisi ni kwa Sauti.

Kwa ufupi, Huduma ya Kanisa Halisi iko pale ambapo kitabu kiliandikwa katika kituo cha zaidi ya yale yaliyofanywa na mwana (Yoh 14:12). Maana ya jambo hili ni kwamba tuache kituo cha kujua ya zamani, tupokee kituo cha Uelewa wa Sauti. Hapo ndipo tutaipokea Huduma ya Kanisa Halisi na kuiona ni nzuri.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages