Mbunge wa
Mbeya Vijijini, Oran Njeza anaendelea na ziara yake katika kata mbalimbali
jimboni humo kwa kutoa michango mbalimbali pamoja na kukagua miradi mbalimbali
ya maendeleo.
Mbunge huyo
katika ziara yake ya jana ametoa sh. 400,000 kwa ajili ya kusaidia chakula cha
wanafunzi wawapo shuleni, ambapo sh. 200,000 imepewa Shule ya Msingi Chang'ombe
na sh. 200,000 nyingine ameipatia Shule ya Msingi Itega.
Hata hivyo,
amewaomba wananchi nao kuendelea kuwa na moyo wa kujitolea katika ujenzi wa
miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo, bila kusahau kutoa michango kwa
ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni.
Aidha, akiwa
katika Kijiji cha Chang’ombe alitatua changamoto ya muda mrefu ya maji kiasi
cha kupata pongezi kutoka kwa wananchi kwa kuwajali.
Mbunge huyo
ametoa ahadi kuanzia mwaka huu, kutoa zawadi ya sh. 100,000 kwa kila mwanafunzi
wa darasa la saba jimboni humo atakayepata ufaulu wa daraja A kwa lengo la
kuhamasisha ufaulu.
Njeza ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, amewaeleza wananchi
wa Kata ya Mjele, kwamba serikali
imetenga sh. milioni 50 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Msingi Itega, jambo
ambalo lilipokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wa eneo hilo.
Pamoja na mambo mengine, lengo la ziara hiyo ni; kukagua miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuhuisha uhai wa chama pamoja na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhakiki taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, zoezi litakapoanza jimboni humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇