Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) Bw. Hamad Abdallah, akipata taarifa ya ushiriki wa NHC katika maonesho ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam 2024.
Bw. Hamad, ameambatana na menejimenti ya Shirika hilo kujionea nini Shirika limefanikiwa katika huduma na bidhaa inazotoa katika maonesho hayo.
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewataka Watanzania kufika katika banda lao kwenye maonyesho ya Kimataifa ya bishara ya Dar Salaam, maarufu kama Sabasaba ili kujua fursa mbalimbali za upangaji na ununuzi wa nyumba aidha NHC imesema imeandaa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha makazi na maisha ya Watanzania.
Akizungumza katika banda la maonyesho la Shirika hilo, Hamad Abdallah amewakaribisha Watanzania kushiriki katika miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa 711, Samia Housing Kawe, na Medeli II. Miradi hii inatoa fursa za kipekee kwa wananchi kupata makazi bora kwa bei nafuu.
Aidha, alibainisha kuwa NHC imeanza ujenzi wa miradi mipya ya makazi katika maeneo ya Kijichi, Njedengwa, pamoja na miradi ya biashara katika Mtanda Lindi na Kashozi Bukoba. Miradi hii inalenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuongeza idadi ya nyumba za makazi na biashara.
Pia, Hamad Abdallah alisema kuwa, katika kutekeleza sera ya ubia, Shirika limeanza ujenzi wa majengo 16 yaliyokuwa yakikaliwa na familia 200 na sasa yatatumika na familia zaidi ya 2,000. Hii inaonyesha dhamira ya NHC katika kuboresha hali ya makazi na maisha ya Watanzania kwa ujumla.
Katika maonyesho hayo, Shirika la Nyumba la Taifa limetenga dawati maalumu kwa ajili ya kushughulikia masuala ya upangaji na utekelezaji wa sera ya ubia, ambayo inashirikisha sekta binafsi. Hii ni fursa nzuri kwa wawekezaji na wananchi kushirikiana na NHC katika kuboresha miundombinu ya makazi nchini.
Watanzania wanahimizwa kufika katika banda la NHC kwenye viwanja vya maonyesho ya Sabasaba ili kupata maelezo zaidi na kuchangamkia fursa hizi za kipekee zinazotolewa na Shirika la Nyumba la Taifa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇