Na HEMEDI MUNGA, Igunga
MBUNGE wa Jimbo la Manonga wilayani Igunga mkoani Tabora, Seif Gulamali amempongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulipa jimbo hilo fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aidha, amewapongeza Mkuu wa wilaya hiyo, Sauda Mtondoo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Selwa Abdalla Hamid kwa namna wanavyoendelea kusimamia miradi ya maendeleo kwa ukamilifu ikiwemo kutoa wataalam kushiriki katika ziara yake.
Akizungumza mbele ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wajumbe wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo na wataalam wa Halmashauri hiyo, Gulamali amemshukuru Rais Dk. Samia kwa sababu amendelea kulithamini na kulijali jimbo hilo.
Shukran hizo amezitoa wakati wa kikao cha majumuisho katika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa wilaya hiyo, baada ya kutembelea kata 19 za jimbo hilo lenye vijiji 63 na vitongoji 440.
Aidha, ameweka wazi kuwa Rais Dk. Samia aliwasamehe wakulima wa zao la pamba nchi nzima wakiwemo wa Igunga gharama ambazo walizitumia kwenye mbegu na viwatilifu.
"Ndugu na viongozi wenzangu kipekee ninamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, tumesamehewa deni la sh bilioni 5.3," ameshukuru Gulamali.
Akizungumzia kuhusu elimu, Gulamali amefafanua kuwa hivi sasa jimbo hilo linashule za kidato cha tano na sita tatu ukilinganisha na wakati anaomba ridhaa ya kuwa mbunge hakukua na shule ya daraja hilo hata moja.
Amesema ni mafanikio makubwa wameyapata huku akiweka wazi kuwa wamepokea fedha nyingine za kujenga mabweni katika shule ya Seif Gulamali kwa lengo la kuipandisha hadhi kuwa na kitado cha tano na sita.
Mbali na hayo, Gulamali amedokeza wanatarajia kupokea takriban sh bilioni tatu kwa lengo la kujenga shule ya amali.
Pia, amesema Rais Dk. Samia aliwapatia gari jipya la wagonjwa lenye thamani ya takribani sh milioni 200 ambalo lipo katika kituo cha Afya Choma.
Kwa upande wa nishati ya umeme, Gulamali ameendelea kuishukuru serikali ya Rais Dk. Samia kwa sababu aliwapatia sh bilioni 15 kufikisha nishati hiyo katika vijiji vyote.
Katika hatua nyingine, Gulamali ameeleza Rais Dk. Samia aliisharidhia waanze ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Choma kuja Ziba, Ziba kwenda Nkinga hadi Puge.
Amebainisha kuwa kazi ya usanifu imeishakamilika na hivi sasa wapo katika hatua ya kutangaza kazi kwa lengo la kupata mkandarasi atakayejenga barabara hiyo.
"Ninampongeza sana Rais Dk. Samia ametupa fedha takribani sh bilioni nne na sio tu katika jimbo langu mabadiliko haya yamefanyika nchi nzima katika kila jimbo," amethibitisha.
Amebainisha kuwa jimbo hilo, awali walikua wanapokea sh milioni 300 katika sekta ya barabara lakini leo hii wanapokea sh bilioni mbili.
Kwa upande wa Mwanyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mafunda Temanya amewataka wataalam hao kuendelea kuwa wakweli na kufanya kazi vizuri.
Amesema wanataka viongozi waendelee kuwa mstari wa mbele kuonesha imani na uadilifu kwa wananchi.
"Tutende haki, tufanye vizuri na hakika Rais wetu anafanya mambo mazuri, hivyo niwaombe tufuate mfumo wake namna anavyofanya," ameshauri Temanya.
Ziara ya Mbunge katika jimbo hilo ilichukua siku takribani 20 ambapo ilianza mwezi Julai 08 na kuhitimishwa mwezi Julai, 27 mwaka huu.




No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇