Na HEMEDI MUNGA, Singida
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida kimempongeza Mkurugenzi wa Kiwanda cha Pamba cha Biosustain (T) LTD kilichopo Manispaa ya Singida, Sajjad Haider kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika kuzalisha ajira ikiwemo kujenga baadhi ya miradi ya maendeleo.
Pongezi hizo, amezitoa Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama hicho wa Mkoa huo, Elphas Lwanji, wakati alipoambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo walipofanya ziara katika kiwanda hicho.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Lwanji amesema CCM inampongeza kiongozi huyo kwa sababu wameona namna kiwanda hicho kinavyofanya kazi na kutoa ajira kwa wananchi hususan wale walipo vijijini.
Amesema wanawapa wakulima fedha za pamba kwa wakati na kujenga mradi mkubwa wa bweni kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanakaa bweni.
"Hakika hatua hii inaendelea kusaidia
watoto wetu huko Iramba kuweza kufikia malengo yao kupitia elimu," amesema.
Ameeleza kiwanda hicho, kimewezesha ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari ya Mtekente iliyopo wilayani Iramba mkoani hapa lenye thamani ya sh milioni 180.
Aidha, amebainisha bweni hilo lina uwezo wa kupokea wanafunzi 80, jiko ikiwemo ujenzi wa kisima.
"Sisi CCM kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama chetu mkoani hapa, Martha Mlata tunakupongeza Mkurugenzi kwa ushirikiano mkubwa unaotoa kwa chama," amesema na kuongeza kuwa:
"Mheshimiwa Waziri hawa Biosustain ni wadau wetu wakubwa kwenye chama chetu, tunapokuwa na mambo mbalimbali ya kufanya wanatusaidia."
Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema serikali inafurahishwa na uwekezaji unaofanyika katika kiwanda hicho kwa sababu fedha zinazokopwa zinaingia kwenye mzunguko wa uchumi wa mkoa huo.
"Umuhimu wa viwanda ni kusaidia kunyanyua pato la Mkoa wa Singida, sasa nyie mnapokopa fedha sisi hilo ndio muhimu maana tunahesabu thamani 'value' ya kuingia kwenye uchumi wa mkoa wetu wa Singida," amedokeza Prof. Mkumbo.
Aidha, ameweka wazi serikali inahamasisha uchakataji wa mazao ya wakulima ya nafaka na chakula hususani katika zao la Pamba ambalo linalimwa katika mikoa 17.
"Karibu nusu ya idadi ya wakulima wanategemea zao la pamba lakini changamoto iliyopo ni kwamba asilimia 80 ya pamba inayozalishwa Tanzania inauzwa kama malighafi kabla haijachakatwa," ameongeza.
Pia, amesema nia ya Rais na serikali kwa ujumla ni kuona angalau kiwango cha kuchakata pamba kinafikia hadhi ya kati, hivyo kiwanda cha Biosustain kiwe ndio mfano kwa lengo la pamba isiwe inauzwa kama malighafi hali ambayo inasababisha watu kukosa ajira.
"Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kwa lengo la kupunguza usafirishaji wa pamba nje ya nchi ikiwa katika hali ambayo ni ghafi, kuchakata pamba nchini kuna uwezekano mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi," amebainisha Prof.Mkumbo.
Mbali na hayo, Prof. Mkumbo amesema serikali ipo katika hatua za kushughulikia changamoto za EFD ambapo inapitia upya mfumo wa kodi nchini huku eneo linaloangaliwa likiwa ni la EFD.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho, Sajjad Haider, amesema mwaka huu kiwanda kimechukua mkopo wa takribani Dola za Kimarekani milioni 14 kwa lengo la kuendelea na uzalishaji.
Kiwanda cha Pamba cha Biosustain kinaendelea na uzalishaji na kinamilikiwa na Wazawa.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa Singida, Elphas Lwanji akieleza namna CCM inavyoridhishwa na Biosustain inavyozalisha ajira, wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo katika kiwanda cha Pamba cha Biosustain kilichopo Manispaa ya Singida (Picha kwa msaada wa Ofisi ya Uenezi)
aziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, wakati wa ziara katika kiwanda cha Pamba cha Biosustain kilichopo Manispaa ya Singida (Picha kwa msaada wa Ofisi ya Uenezi)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇