Kikundi cha Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Vyombo Vya Usalama na Taasisi za Kiraia za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimeshiriki katika ufunguzi rasmi wa Zoezi la 13 la Medani la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki "FTX Ushirikiano Imara 2024" linalofanyika katika Chuo cha Kijeshi cha Maafisa Gako Nchini Rwanda tarehe 13 Juni 2024.
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu Meja Jenerali Fadhil Omary Nondo ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali John Jacob Mkunda amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa zoezi hilo kumekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Vyombo Vya Ulinzi, Usalama na Taasisi za Kiraia kutoka nchi wanachama wa EAC vimekuwa vikifanya mafunzo na mazoezi ya pamoja katika nyanja mbalimbali ikiwemo Ulinzi wa Amani, kukabiliana na Majanga ya kibinadamu,ugaidi na uharamia wa kwenye maziwa na baharini ili kujiweka tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali pindi zitakapojitokeza.
Kikundi kutoka Tanzania kimeundwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania,Polisi,Uhamiaji,Zimamoto na Uokozi pamoja na Taasisi mbalimbali za Kiraia chini ya uongozi wa Brigedia Jenerali Said Hamis Said ambaye pia ndiye Kamanda wa Vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vinavyoshiriki zoezi hilo.
Zoezi Ushirikiano Imara 2024 limefunguliwa rasmi na Waziri wa Ulinzi wa Rwanda Mheshimiwa Juvenal Marizamunda.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇