Na HEMEDI MUNGA, Iramba
MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida ambae ni Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego amewafunda Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) wa mkoa huo kuelewa kuwa wao ndio tanuri linalopika viongozi makini ambao wameendelea kuongoza katika nyazifa tofauti nchini.
Aidha, amewataka kuwepo popote pale ikiwemo aridhini, angani na kwenye mitandao ya kijamii kueleza utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho huku wakitoa ufafanuzi dhidi ya wale wanaopotosha mambo makubwa yaliofanywa na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika Baraza hilo, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani hapa, RC Halima amesema Umoja wa Vijana ni tanuri na darasa la kupika raia wema wa nchi hii na kuhakikisha inapata viongozi bora.
"Hakika UVCCM inapika na kupata viongozi bora, wote waliopita katika tanuri hili wanaonekana wanaposimama na haitaji kuuliza, kwa sababu wameandaliwa vema kwa kujua Itikadi, historia ya nchi yao walikotoka, walipo na wanakokwenda," amesema.
Aidha, amewafahamisha kuwa katika umoja huo, unahitaji utashi binafsi, kujitoa, uzalendo na kujiamini kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu.
Ameeleza kuwa wakati wao, wakiwa katika Umoja huo na kwingineko, walikipigania chama hicho kwa kutembea kwa miguu, bila ya kujua nani atawapa fedha na wakati mwingine kushinda na njaa.
"Tulikua tunafia Mama Tanzania, kwa kuamini usalama wa Tanzania upo mikononi mwa CCM," amesema.
Hivyo, amewataka kuacha tabia ya kujiamini, kujivuta na kuwa na matamanio binafsi kwa sababu kuacha hayo ndio wataweza kukiokoa Chama na Jumuiya zake.
"Sisi tulitumika pasina kujua siku wala saa nitakua nani, nilipiga kampeni, nilitembea mikoa yote bila ya kujua nitapata nini," amesisitiza.
Aidha, amewataka kuendelea kuhamasisha vijana wengine kwa lengo la kuendelea kuwa wengi ikiwemo wasomi kwa sababu wao ni wasomi tena ngazi ya shahada.
Katika hatua nyingine, Halima amesema serikali yao inafanya makubwa kwa sababu ya kuongozwa na Rais Dk. Samia mwenye mapenzi na mzalendo wa kweli kwa Taifa.
"Wajibu wetu vijana, alipo Mama na sisi tupo, aridhini, angani na mitandaoni tuwe wafafanuzi wakubwa kukanusha upotoshaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM," ametoa wito.
Ameweka wazi kuwa vijana ndio chem chem ya fikra mpya, hivyo serikali imewekeza kwa vijana wapate elimu kwa lengo la kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo nchini.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amewakumbusha vijana hao wajibu wao wa msingi kuhangaika na wapinzani hata kabla ya Chama kufungua mdomo.
Aidha, amewataka kuwa na moyo wa kujitolea na kufanya hivyo bila ya kutegemea fursa, utaratibu wa kuishi, cheo wanachokitegemea au mpango walioutega.
"Nilazima niwakumbushe wajibu wetu wa msingi kwamba, moja ya jukumu letu ni kujitolea kwa ajili ya Chama chetu," amesisitiza.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) anayeuwakilisha mkoa huo, Yohana Msita amesema CCM inaitegemea Jumuiya hiyo kwa sababu ndio inayopika viongozi wa leo na kesho wa Taifa hili.
"Viongozi wengi wa Taifa hili tunaowaona leo, wemetokana na Umoja wa Vijana wa CCM, hivyo nyinyi ni viongozi wa nchi hii, lazima tuthubutu na kuacha uoga katika kukabiliana na mambo ambayo yanahitaji tukabiliane nayo ndani ya chama, serikali na katika jamii tunayoishi nayo," amesema na kuongeza kuwa:
"Nilazima wabadilishe mitazamo yao na kuhakikisha kuwa wanafanya kitu kwa ajili ya chama na sio chama kiwafanyie kitu, hivyo wasikae kimkakati kwa kutaka chama kiwafanyie kitu."
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida ambae ni Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendego akiwataka Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) wa mkoa huo kueleza sera na mafanikio ya CCM, wakati wa kikao cha Baraza hilo, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani hapa. (Picha na Hemedi Munga)
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mkoa wa Singida, Lucy Shee akifikisha salam za Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa huo, Martha Mlata, wakati wa kikao cha Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama hicho, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani hapa. (Picha na Hemedi Munga)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇