LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 14, 2024

KUNG'ARA RAIS DK. SAMIA MAGEUZI YA UENDESHAJI MASHIRIKA YA UMMA

Na Derek Murusuri, Dar es Salaam
UWEKEZAJI kwenye mashirika, duniani kote umekuwa msingi imara wa kuzisaidia Serikali za nchi malimbali kupata raslimali fedha, zinazotumika kuchochea ukuaji na maendeleo ya uchumi.

Tanzania imefanya uwekezaji wa takriban trilioni 76 katika mashirika. Huu ni uwekezaji mkubwa sana kiasi cha kuifanya Tanzania kuwa mojawapo ya mataifa yenye uchumi mkubwa barani Afrika, sasa hii ni dhahiri.

Ndio maana uanzishwaji wa Mamlaka ya Uwezekazi wa Umma, ni mageuzi makubwa yanayoweza kuupa tija kubwa uwekezaji wa umma nchini.

Huu ni ushahidi wa wazi kuwa mageuzi makubwa ya kiuchumi, yanayoongozwa na 4R za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanakwenda kuibadilisha Tanzania ndani ya miaka michache ijayo kuongoza uchumi wa Afrika Mashariki na baadaye Afrika.

Gawio na michango ya bilioni 850 ni ushahidi, Ufanisi
Ushahidi wa kihisitoria wa gawio la shilingi bilioni 637 na baadaye mwezi huu kufikia shilingi bilioni 850, ni habari mbaya sana kwa wanaobeza mageuzi ya kiuchumi ya Rais Dkt. Samia. Kila mwenye macho ameanza kuona.

Kuona ni kuamini. Mzee John Samwel Malecela, alizoea kusema wapo watu wanaotaka kuchuna ngozi ya kiroboto. Wale wanaojitia upofu hali wanaona. Hakika mageuzi ya kiuchumi ya Dkt. Samia yameanza kuzaa matunda.

“Mheshimiwa Rais kuna mambo mengi ambayo yamefanyika katika kuitikia wito wako na kutekeleza maono yako ya kuleta mageuzi katika utendaji kazi mahali popote penye uwekezaji wa Umma, lakini itoshe kusema kuwa leo sio siku yetu ya kuzungumzia tuliyoyafanya kwakuwa leo ni siku maalam ya kupokea gawio (Tanzania Dividend Day),” anabainisha Bw. Nehemiah Mchechu, Mrajisi wa Hazina.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mashirika ya umma na yale ambayo Serikali ilikuwa na hisa kidogo, kujumuika pamaoja na kutoa gawio na michango kwa Serikali ya Tanzania. Huu ni ushahidi wa kufanikiwa kwa falsafa ya 4R ya Dkt. Samia na kuongezeka kwa tija kutokana na ufanisi katika usimamizi bora wa mashirika. Hongera Bw. Mchechu na timu yako.

Mashirika yachangia baada ya miaka 10
Yapo mashirika mengine kama MCC, ambayo kwa miaka 10 yalikuwa hayajatoa gawio. Leo imewezekana. Hii ni kutokana na uongozi wa mabadililo na ufanisi, ndio uliowezesha mashirika 145 kuchangia. Idadi hii ni ongezeko la mashirika 36 kutoka mashirika 109 ambayo yalichangia mwaka 2023.

Hamna jinsi mashirika mengine 159 ambayo hayakuchangia safari hii, yashindwe kuchangia mwakani. Dhana ya mabadiliko italeta tija katika kubuni, kuongeza bidii na ufanisi ili kuendelea kuaminiwa. Ndio maana uamuzi wa kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma ni muhimu sana kwa ajili ya kuleta tija katika uendeshaji wa mashirika ili kuleta faida.

4R na Shareholder Wealth Maximization (Kuongeza Faida kwa Mwenyehisa)
Hii ni dhana ya kawaida katika biashara. Ipo hata katika biblia. Inahusu aliyepata talanta moja hadi tano. Mashirika yanajukumu la kupata faida na kuongeza faida kwa mwenye hisa. Yanapaswa kurudisha sehemu ya faida.

“Huu ni ushahidi kuwa 4R za Dkt. Samia tayari zimeanza kuonesha mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuteua viongozi wazuri wenye sifa ya utendaji wenye matokeo kama Bw Mchechu, toka akiwa Benki ya CBA na baadaye NHC,” alisema Profesa Jonathan Stephen.

Bw. Mchechu ameweza kuongeza hisa za Serikali kwenye baadhi ya mashirika, kutoka 15 hadi 20, hivyo kuiongezea Serikali faida. Mashirika 304 ambayo yako chini ya uongozi mahiri wa Wizara na Msajili wa Hazina, yanatarajia kufikia asilimia 10 ya mapato ya kikodi. Gawio na mageuzi yanadhihirisha kuwa mapato yanaweza kuwa makubwa zaidi.

Mashirika haya yanachangia katika bajeti ya taifa kwa mapato yasiyo ya kikodi kwa asilimia 3. Wastani wa changizo katika Afrika ni asilimia 6, lakini Bw Mchechu anaona inawezekana yakachangia hadi asilimia 10, ikiwezekana hata zaidi ya hapo.

Mchango wa Mashirika kwenye Uchumi wa Nchi
India ni mojawapo ya mataifa ambayo mashirika yake ya umma yana mchango mkubwa katika kuipatia Serikali yao raslimali fedha pamoja na ajira kwa wananchi wake. Hii ni pamoja na kuweka msingi mzuri wa viwanda nchini mwao. Ndio maana uchumi wa India sasa unaelekea kuwa uchumi mkubwa wa tatu duniani, kutoka wa tano sasa, baada ya miaka michache.

Ilichukua takribani miaka thelathini baada ya uhuru kwa nchi yetu kufanya mageuzi ya uendeshaji wa Mashirika ya umma chini ya usimamizi wa IMF na WB. Mageuzi ya “SAP,” ndiyo yaliyo ufungua uchumi wa Tanzania baada ya vita vya Kagera.

“Sasa tunashukuru kuwa miaka thelathini baadaye Mheshimiwa Rais, umeanzisha mageuzi kwa awamu ya pili, bila kusubiri kuambiwa ama kusurutishwa na mabwana wakubwa hawa…[WB na IMF], alisema Bw. Mchechu.

Siku ya Gawio Tanzania
Dkt. Samia aliridhia ombi la Msajili wa Hazina kuwepo na Siku ya Gawio nchini, katika miezi ya Mei mwishoni au Juni mwanzoni kila mwaka.

Mageuzi yataleta Mafanikio makubwa
Mageuzi na kujenga upya chini ya 4R za Dkt. Samia, yanakwenda kuupaisha uchumi wa Tanzania. Bwawa la Julius Nyerere likiwa tayari limeanza kuzalisha umeme na treni ya umeme ikiwa imeanza safari zake kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, hakika miradi hii mikubwa ya kimkakati ni hamasa kuwa makubwa zaidi yanawezekana.

SGR ya Tanzania ambayo, ikikamilika, itakuwa reli ndefu ya kuliko zote barani Afrika. Pia, itakuwa ya tano kwa urefu duniani.

“Serikali katika kujenga uchumi na maendeleo endelevu ya nchi, basi mabadiliko ya kiusimamizi, kiutendaji na kiuendeshaji hayaepukiki,” anatanabaisha guru wa mabadiliko, Bw Nehemiah Mchechu.

Mamlaka ya uwekezaji ya umma
Muswada wa sheria ya Mamlaka ya uwekezaji wa mashirika ya umma utakapokuwa sheria, Tanzania itafurahia uwekezaji wa matrilioni ya shilingi katika mashirika yake. Haya ni maono ya Dkt. Samia, akisaidiwa na Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Dkt. Mchechu.

Tahtimu
Mageuzi haya ni ya ndani. Yanafanyika miaka zaidi ya 30 baada ya mageuzi yaliyoletwa na Benki ya Dunia (WB) pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Miaka mitatu tu ya Dkt. Samia, mageuzi makubwa ya kiuchumi yanafanyika. Matunda yanapatikana. Utegemezi unaendelea kupungua.

Mamlaka ya uwekezaji wa umma itakapoanza kazi, mapato ya nchi yatazidi kupaa. Ustawi na maendeleo ya uchumi wa Tanzania utashamiri. Tija itaonekana zaidi.

Hii ina maana gani? Wasomi na viongozi wazalendo wanaoweza kusimamia ustawi na maendeleo ya uchumi wetu wako kazini. Kwamba, bila ushawishi wa mabwana wakubwa, Tanzania inaweza ikaasisi mageuzi yake, ikayafanyia kazi na kuwatoa wananchi wake katika umasikini.

Maana yake ni kwamba, mageuzi na kujenga upya vimejaribiwa na kuzaa matunda. Kupitia hizi 4R, Tanzania inaweza kuibuka Taifa lenye uchumi mkubwa zaidi katika Afrika. KAZI IENDELEE.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages