Beijing, China
Tanzania imefanya uzinduzi rasmi wa filamu ya 'Amazing Tanzania' katika maadhimisho ya miaka 60 ya Kidiplomasia kati yake na China, yaliyofanyika leo, Mei 15, 2024 Jijini Beijing.
Katika maadhimisho hayo, sanjari na uzinduzi wa filamu hiyo, Tanzania imezidua pia mwaka wa Utalii na Utamaduni?
Katika Maadhimisho hayo Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema uhusiano kati ya China na Tanzania ulianza tangu kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Amesema mahusiano kati ya China na Tanzania ni thabiti chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.
"Tunapoadhimisha miaka 60 ya uhusiano wetu na pia tunasherehekea mwaka wa utamaduni na utalii kama ilivyotangazwa na viongozi wetu mwaka 2022 katika ziara ya Kiserikali ya Rais Samia Suluhu alipotembelea hapa nchini China" Waziri Kairuki amesisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Mwinyi na mwigizaji maarufu wa filamu kutoka China, Jin Dong kwa kushiriki katika uandaaji wa filamu hiyo.
Kufuatia uzinduzi wa filamu ya " Amazing Tanzania " Kairuki amesema kuwa filamu hiyo itaonyesha vivutio vya utalii wa Tanzania kwa soko la utalii la China na kwamba Tanzania inatarajia kupokea watalii wengi kutoka nchini China baada ya uzinduzi huo.
Naye, Waziri wa Utamaduni na Utalii wa Jamhuri ya Watu wa China, Sun Yeli amesema kuwa urafiki wa jadi kati ya China na Tanzania ulijengwa na viongozi wa kizazi cha zamani wa nchi hizo mbili na kwamba tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia miaka 60 iliyopita China na Tanzania zimestahimili jaribio la mabadiliko ya mazingira ya kimataifa na kuimarika zaidi.
"Leo tunapokutana hapa kuzindua mwaka wa Utalii na Utamaduni wa Tanzania na China natumai tutaifanya kuwa mwanzo mpya wa kuendeleza mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano wa Utalii ili kurahisisha ziara zetu za pande mbili, mabadilishano kati ya taasisi za kiutamaduni na sanaa na vile vile kampuni za utalii kuongeza usambazaji wa bidhaa za utalii." amesisitiza.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro,Waziri wa Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma na binafsi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇