LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 8, 2024

MAKALLA: CCM TUTAWASHINDA CHADEMA KWA KISHINDO, KATIBA MPYA SIO SAWA NA KUSONGA UGALI

Ibrahim Bakari, CCM official Blog
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, CPA Amos Makalla amesema CCM imejipanga na itashinda kwa kishindo uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Akizungumza leo Mei 8, 2024 kupitia Wasafi FM, amesema kama chama wamejipanga kila eneo na Chadema wataangushwa hadi watajishangaa kwa kipigo.

Amesema wamefanya utafiti ndani ya CCM  kwamba ushindi wa kishindo hauna mjadala na wameangalia maandalizi yaliyofanyika yanawapa nguvu kufanya vizuri.

Makalla amesema silaha kubwa ya ushindi katika uchaguzi wa mitaa,  ni utekelezaji wa ilani na Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ikiwemo kupeleka fedha nyingi katika miradi mbalimbali mikubwa na midogo na kila mahali kuna alama.

Ameyataja baadhi ya maeneo yaliyoshughulikiwa kuwa ni eneo la umeme, maji, elimu, huduma za afya na kwamba kupitia utekelezaji wa ilani hiyo, CCM ina uhakika wa ushindi wa kishindo.

Aidha amesema ushindi mwingine watakaoupata utatokana na udhaifu unaoendelea sasa ndani ya Chadema kwani CCM ilidhani walikuwa wapinzani wa kweli, lakini wamebaini ni chama kinachokwenda kuporomoka.

Amesema kuporomoka kwa Chadema kunatokana na mgogoro mkubwa ulioko ndani ya chama hicho ikiwemo madai ya kukinzana; uenyekiti, urais, fedha chafu na hoja mbalimbali ambazo viongozi wakuu wanavutana na ndizo dalili mbaya.

Mbali na hayo amesema Chadema hawatakuwa na cha kuwaeleza wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa zaidi ya kuwaambia wamefanya maandamano.

Akikizungumzia chama chake, Makalla amesema wao wanawapa wananchi; matumani; wanawaandaa watu na kwamba Chadema hawajaonyesha nia ya dhati kushiriki uchaguzi wa mitaa kwa kuwa hawana cha kuwaambia wananchi.

Akisisitiza ushindi huo wa kishindo kwamba ni ushindi wa haki na kama chama kina kiongozi makini na ndiyo maana anakubalika.

Kitu kingine amesema CCM kufanya harakati kwa kuandaa watu na kuwaelezea kile kilichofanyika ikiwemo kujitathmini.

Makalla ameyasema hayo leo Mei 8, 2024 kwamba kila mara wapinzani hasa Chadema wamekuwa wakitaka Katiba mpya, na kwamba suala la Katiba ni mchakato.

Kuhusu Katiba Mpya. CPA Makalla, amesema Katiba Mpya si sawa na kusonga ugali kwamba unabandika maji, mara yamechemka, unaweka unga, unasonga na ugali tayari.

Makalla amesema Chadema wanapigia kelele Katiba Mpya wakati ndani ya chama chao hakuna demokrasia, na kwamba wangerekebisha katiba yao kwanza ndipo watoke kuzungumzia hili.

Itakumbukwa, Serikali ilitangaza miaka mitatu ya kutoa elimu ya Katiba kabla shughuli ya Katiba haijaanza.
Hata hivyo, Makalla amesema Chadema wangejiangalia kabla ya kudai Katiba kwani hata Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe amevunja katiba yao kwa kukaa muda mrefu kama kiongozi wa chama.

Kuhusu nafasi ya CCM, anasema wamejipanga na safari za mikoani wanakwenda kuangalia uhai wa chama.


Aidha amesema maandalizi ya uchaguzi na utekelezaji wa Ilani na kusikiliza kero ni kazi inayofanyika sasa.


 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages