Dk Samia anaposubiriwa kumaliza mizozo Afrika
Ibrahim Bakari, Official CCM Blog
Mwaka 1961
baada ya Tanganyika kupata uhuru, Rais wa kwanza wa Tanganyika huru, Mwalimu Julius
Nyerere aliwahi kusema, Tanzania haiwezi kuwa huru mpaka Afrika yote iwe huru.
Huyo
alikuwa hayati Baba wa Taifa. Aliangalia mbali kwamba Watanzania hawawezi
kujidai, hawawezi kula matunda ya uhuru kwa raha zao ilhali nyumba ya jirani mitutu inalia kila kukicha.
Hakuishia
kwenye matamshi ya jukwaani, alivaa viatu akaingia uwanjani.
Kutokana na
shauku yake kutaka kuona Afrika inakuwa huru, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika.
Wakati huo lengo
kuu ni kuhakikisha mataifa ya Afrika yanapata
uhuru ikiwemo; Angola, Afrika Kusini,
Zimbabwe, Namibia, Msumbiji na mengine yanakuwa huru kutoka mikononi mwa
walowezi wachache.
Mapambano yakatimia.
Afrika imekuwa huru.
Pamoja na
hayo, ndani ya Afrika kumekuwa na
chokochoko za makundi ya waasi ambayo hadi leo yanaisumbua Afrika.
Itakumbukwa
kulikuwa na watu kama; Jonas Savimbi ambaye aliuawa Februari 22, 2002 na vikosi
vya Serikali ya Angola.
Kwa
Savimbi, ilikuwa kila kukicha mitutu inasikika, lakini sasa Angola iko vizuri
tofauti na wakati huo.
Mfano
mwingine ni Taifa la Msumbiji likiongozwa na Chama cha Frelimo, lakini bado ilisumbuliwa
na Waasi wa Renamo walioongozwa na Alphonso Dhlakama ambaye naye alifariki Mei
4, 2018.
Kufariki
ama kuuawa kwa viongozi wa waasi, kwa njia moja na nyingine imesaidia angalau
kutuliza mfululizo wa milio ya risasi na mabomu.
Hawa na
wengine, ni mifano ya wavuruga amani ya
Afrika kwa uchu wa madaraka. Wengi wa waasi waliishia kuuawa.
Pamoja na
hayo, waasi katika baadhi ya mataifa ya Afrika, bado ni tatizo, mfano mzuri
inaonekana nchini Nigeria, makundi ya Boko Haram, nchini DR Congo makundi ya
M23 yanavyoendelea kusumbua.
Tatizo
lingine ambalo bado linasumbua Afrika ni mapinduzi ya kijeshi, ambayo mara zote
hufanyika kwa kuondoa utawala halali na jeshi kuchukua madaraka kwa sababu
mbalimbali na baadaye kukosekana amani na utulivu kutokana na mapinduzi hayo.
Kwa sasa,
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, AU lina kazi moja ya
kumaliza mizozo ya mataifa kama ilivyo DR Congo uliodumu kwa zaidi ya
nusu karne sasa, ambayo imesababisha hadi uingiliaji kati wa majeshi ya kigeni.
Itakumbukwa, Aprili 19, 2024, ujumbe wa amani wa Umoja wa
Mataifa katika DR Congo (MONUSCO) ulikabidhi kambi ya Bunyakiri kwa majeshi ya
Serikali (FARDC).
Kaimu kamanda wa kikosi cha MONUSCO, Meja Jenerali Khar
Diouf, amesema hatua hiyo ni nzuri kwani na ni mwanzo mzuri wa kudhoofisha
nguvu za M23 na tayari Baraza la Amani na Usalama chini ya Mwenyekiti wake; Rais
Samia Suluhu wa Tanzania, limesema halitaki kusikia milio ya mitutu
ikitamalaki.
Bunyakiri ni kambi ya pili ambayo MONUSCO iliikomboa nchini
humo, baada ya kujiondoa, kwa wanajeshi wa uasi waliokuwa wamekaa katika kituo
cha Kamanyola hadi Februari 28, 2000 walipoondoka katika jimbo hilo la
mashariki mwa DRC la Kivu Kusini.
Makabidhiano haya mawili ya kambi, kipekee yanaashiria kuanza kwa operesheni ambayo italazimu
kuondoka kwa walinda amani wote wa UN wapatao 13,500, kabla ya Desemba 31, 2024.
Wote hao chini ya Umoja wa Mataifa waliokuwepo nchini humo tangu mwaka 1999.
Mataifa mengine yenye mizozo ya kisiasa ni pamoja na yale ya
pembe ya Afrika, ikiwemo Somalia ambayo hata hivyo inaelezwa mizozo imemalizwa na
baraza hilo.
Aidha mpaka sasa, inaelezwa mizozo imetatuliwa katika mataifa
ya Comoro, Sudan, Somalia na Ethiopia pamoja na baadhi ya mataifa ya Afrika
Magharibi ikiwemo Mali.
Akizungumza katika maadhimisho ya Baraza hilo tangu
lianzishwe Mei 25, 2004, Mwenyekiti wake, Dk. Samia amesema Baraza limekuwa na nafasi muhimu katika kukuza amani,
usalama na utulivu wa Afrika.
Amesema Tanzania itahakikisha Baraza la Amani na Usalama wa
Afrika, unakuwa madhubuti ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kutoa
hamasa ya kulinda amani na kuhakikisha
ustawi wa watu.
Dk. Samia amesema ni muhimu kwa baraza kuwashirikisha vijana
na wanawake katika kuimarisha na kuleta maendeleo ya kiusalama ili kuleta
mabadiliko chanya pamoja na maendeleo kijamii na kiuchumi.
Amesema jitihada za pamoja ni muhimu katika kuimarisha
usalama, hivyo ni muhimu kwa wanachama na baraza ambao ni mataifa ya Afrika kwa ujumla kuongeza ushirikiano na wadau wa
makundi mbalimbali.
“Leo ni miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Baraza hili lina jukumu
la kuzuia, kudhibiti na kutatua migogoro katika bara letu la Afrika hivyo
niwapongeze viongozi wote kwa hatua tuliyofikia,” amesema na kuzipongeza nchi
wanachama wapya waliojiunga na baraza hilo kuanzia Aprili, mwaka huu.
Dk Samia amewaahidi ushirikiano katika mambo yote ambapo nchi
wanachama wa AU 53 kati ya 55 zimeridhia itifaki ya uanzishwaji wa baraza hilo
ambalo bado linaendelea na jitihada za kutokomeza mitutu Afrika.
Mbali na mitutu, kubwa ni kuimarisha mifumo ya utambuzi wa
migogoro, kuzuia masula ya ugaidi na kuimarisha demokrasia na utawala bora.
Dk. Samia amesema baraza la Amani na usalama Afrika
limetembelea na kufanya ziara katika nchi ambazo zina migogoro na kuelewa vyema
changamoto za nchi hizo, hivyo limeonesha mshikamano na wahusika wa migogoro
kwa nia ya kuzuia na kuitokomeza kabisa.
Akizungumzia mafanikio Rais Dk. Samia ameainisha mafanikio ya
baraza kuwa ni kuanzishwa kwa majadiliano baada ya vita, kukabiliana na
migogoro na ugaidi, kujidhatiti kusimamia misingi ya haki za binadamu na
ushirikiano wa taasisi.
Amesema ili kuimarisha amani na usalama Afrika, baraza
linapaswa kuongeza uwezo wa kuzuia migogoro kwa kutumia nyenzo zilizopo, kuzuia
migogoro isiwe endelevu kupitia mifumo ya utambuzi wa mapema, kuwepo kwa
majadiliano na kuimarisha michakato ya maridhiano.
“Ipo mifumo ambayo haitumiki vizuri hivyo ni muhimu
kuimarisha amani kutumia jeshi la Afrika, utekelezaji madhubuti wa nyenzo hii
itasaidia kudhibiti mitutu,” amesema.
Ameainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili baraza hilo
kuwa ni uhitaji wa haraka wa kufanya tathmini ya uhuru kwa bara hilo,
mabadiliko yasiyozingatia Katiba kwa sababu hayavumiliki.
Kwa hali hiyo, ni busara za Mwenyekiti zinasubiriwa kumaliza
mizozo ndani ya Afrika kupitia vikao maalumu.
Kimsingi, kuundwa kwa baraza hilo, ni wazi Waafrika wanataka
kumaliza matatizo yao kwa maana ya kwamba matatizo ya Afrika yatamalizwa na
Waafrika wenyewe.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇