LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 26, 2024

CDE MBETO AMVAA JUSSA ATAKA AACHE UPOTOSHAJI MCHAKATO WA ZABUNI UINGIZAJI WA MAFUTA ZANZIBAR

NA MWANDISHI MAAALUM, ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis, amewataka viongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo kuacha upotoshaji juu ya mchakato wa zabuni za makampuni ya uingizaji wa mafuta nchini kwani kampuni iliyopewa tenda ya kuingiza mafuta ya GBP ndio iliyokubali kuingiza mafuta kwa mkopo ambapo makampuni mengine matano yalikataa kwa madai kulipwa fedha taslimu.


Kauli hiyo ameitoa leo wakati akitoa ufafanuzi juu ya upotoshaji huo uliotolewa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar Ismail Jussa wakati wa mkutano wa viongozi wakuu wa chama hicho Mkoa wa Kusini Unguja, aliyedai kuwa mikataba mingi mibovu inayogharimu nchi.


Katika madai ya Jussa, alisema katika zabuni ya kuingiza mafuta ya kampuni tano zilizoomba zabuni ya kuingiza mafuta ,iliyopendekeza zabuni kubwa ndio iliyopewa na kuachwa zilizopendekeza zabuni ndogo.


Mbeto, amefafanua kuwa kauli zilizotolewa na Jussa ni upotoshaji ukweli ni kwamba, Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein  Ali Mwinyi, imeendelea kufanya juhudi kubwa za kuhakikisha inafunga mikataba halali na yenye maslahi mapana ya nchi.


Katibu Muenezi huyo Mbeto, alisema Serikali ilifanya maamuzi ya kupendekeza zabuni ya kampuni ya GBP kwa sababu ilikuwa tayari kuingiza mafuta nchini kwa mkopo na makampuni mengine matano yalikataa kuingiza mafuta kwa mkopo zikijenga hoja ya kuwa bei ya mafuta imepanda duniani.


“ Nishati ya Mafuta ni uti wa mgongo wa nchi inapokosekana kwa dakika moja sote tunajua hali inavyokuwa Zanzibar , kwani watu wanaangaika na hawafanyi kazi kwa ufanisi  kwani wanaangaika kila kituo cha kutoa huduma hiyo  kupata mafuta kwa ajili ya matumizi ya mashine,magari, na pikipiki.


Serikali haiwezi kuacha watu wakiangaika kwa kuwaendekeza makampuni yanayojali faida na maslahi binafsi na faida badala ya maslahi ya nchini kwani kampuni ya GBP imejitolea kusambaza mafuta zaidi ya mwaka sasa wakilipwa fedha kidogo kidogo huku kampuni nyingine zikishindwa masharti ya kutoa huduma hiyo.”, alifafanua na kuwataka Viongozi wa ACT-Wazalendo kufanya utafti kabla ya kutoa kauli za upotoshaji.


Alisema Serikali imeyadhamini kampuni ya ndani yanayofanya biashara ya Mafuta ili kampuni ya GBP iendelee kuleta nishati hiyo ambapo  kwa sasa inadai zaidi ya Bilioni 200.


Alifafanua kuwa hata makampuni ya ndani uwezo wao wa mitaji umeyumba kutokana na bei ya mafuta kupanda Duniani inayosababishwa na uwepo wa vita vya Urusi na Ukraine, matatizo ya nchi za mashariki ya kati, nchi za umoja wa Opec kupunguza uzalishaji kutokana na kupanda kwa Dola ya Kimarekani.


Katibu huyo wa NEC Mbeto, alisema tenda hiyo iliitishwa wazi na kila kampuni ilikuwa huru kuomba lakini kilichojitokeza baadhi ya makampuni hayakuwa tayari kuleta mafuta bila ya kupewa fedha taslimu kutokana na uwezo wa mtaji wa makampuni hayo kuwa mdogo usioweza kukidhi masharti ya Serikali ya kuleta mafuta muda wote nchini.


Pamoja na hayo alieleza kuwa kinachofanywa na viongozi wa Chama Cha ACT- Wazalendo ni kutafuta huruma ya wananchi na kutafuta umaarufu wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 kwa kufanya uchochezi na siasa za porojo zisizokuwa na ushahidi.


Aliwasihi wananchi kuendelea kuamini na kuunga mkono serikali iliyopo madarani kwani inafanya juhudi kubwa za kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora na yenye hadhi.


Sambamba na hayo Mbeto, alisema Zanzibar inahitaji kuwa vyama vya upinzani imara vyenye viongozi wenye maono na fikra za kujenga hoja zenye mashiko, kukosoa, kufanya utafti na kusimamia dhana ya uzalendo na utaifa sio kuwa madalali wa kisiasa.



No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages