Sehemu ya waandishi wa habari
IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Stergomena Tax ametaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu zote sita (6)
za uongozi wakati wa kuadhimisha miaka 60 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Awamu ya kwanza ilijenga nchi, umoja wa kitaifa, iliunda Jeshi,
iliandaa vijana kwa ulinzi wa nchi yao ambao walimshinda Nduli Iddi Amin
Dadaa, mafanikio haya yameendelezwa na awamu zilizofuata zote.
Waziri Tax akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma Aprili 3, 2024, amesema kuwa katika kulinda
mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru, na usalama wa nchi, wizara
kupitia JWTZ imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi
hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu. Aidha, Serikali
kupitia Wizara imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha Jeshi kwa kulipatia zana
na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu, na nyenzo za kufanyia mazoezi ili
kuwa imara wakati wote.
"Ili kuliimarisha
Jeshi, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa Wanajeshi na
Watumishi wa Umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu, kwa kuwapatia makazi
bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali, kupandisha vyeo
kulingana na sifa, vigezo na taratibu."
# Hadi sasa Serikali
imejenga nyumba za makazi katika kambi mbalimbali za Jeshi kwenye mikoa ya
Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Mwanza, Pemba, Pwani,
Rukwa, Tabora, na Tanga. Aidha, ujenzi wa nyumba hizo, kwa kiasi kikubwa
umepunguza uhaba wa nyumba pamoja na changamoto zitokanazo na wanajeshi kuishi
uraiani.
# Mchango mwingine
mkubwa wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania katika miaka 60 ya Muungano,
ni ulinzi madhubuti wa mipaka yetu, uhuru, na katiba. Nchi imeendelea kuwa
imara na yenye amani katika awamu zote.
# Mafanikio mengine ni
ushiriki wa Wizara kupitia Taasisi zake, hususan JWTZ katika kukabiliana na
majanga au maafa mbalimbali pale yanapotokea. Katika kutekeleza jukumu hilo,
JWTZ imeendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa misaada ya uokoaji na ile ya
kibinadamu kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
# Wizara kupitia JWTZ
imeendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika miradi ya kimkakati. Baadhi
ya maeneo ambayo JWTZ imeshirikiana na mamlaka za kiraia ni pamoja na kushiriki
katika kuboresha huduma katika taasisi za serikali; kushiriki katika ulinzi wa
miradi na maeneo ya kimkakati kwa nchi ikiwemo katika migodi mbalimbali, ulinzi
wa miundombinu kama reli, ikiwa ni pamoja na reli ya kisasa Standard Gauge
Railway (SGR), Mradi wa Bwawa la kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (Julius
Nyerere Hydro Power Project - JNHPP); ulinzi katika mamlaka ya usimamizi wa
bandari Tanzania (TPA), kampuni ya simu (TTCL), na maeneo ya viwanja vya ndege.
# Wizara imefanikia
pia kwenye utoaji wa huduma za afya na tiba kupitia hospitali za jeshi za kanda
ambazo ni Lugalo Dar es Salaam, MH Mwanza, Bububu Zanzibar, Mirambo Tabora, MH
Arusha, MH Mbeya ambazo hutoa huduma kwa wanajeshi, wananchi waishio maeneo
yaliyo jirani na kambi za jeshi na katika hospitali nyingine. Kwa upande wa
huduma za tiba, takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanaopata
huduma katika hospitali za Jeshi ni raia wasiyo wanajeshi.
# Ujenzi wa makao
makuu ya Ulinzi wa Taifa eneo la Kikombo jijini Dodoma. Ujenzi huu unatekelezwa
na wataalam wa ndani ya nchi, kwa gharama ya Serikali. Hili ni suala muhimu na
ni mafanikio ya kujivunia, kwani ni ishara ya uimara wa Taifa letu.
# Mafanikio mengine ni
kutungwa kwa Sheria ya JKT Na. 16 ya mwaka 1964 (The National Service Act No.
16 of 1964) ambayo iliwezesha kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Sheria hiyo imefanyiwa marekebisho mbalimbali hadi mabadiliko ya mwaka 2002.
Sheria hiyo imewezesha kuandikishwa vijana wa kujitolea, na kwa mujibu wa
sheria.
# JKT limeendelea
kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuzalisha mali, kuwapa vijana wa kitanzania
mafunzo ya awali ya kijeshi na stadi za kazi, ili kuwajengea ukakamavu,
uzalendo, umoja wa kitaifa, na uwezo wa kujitegemea. Aidha, JKT pamekuwa ni
mahali pekee nchini ambapo vijana wa makabila yote, dini zote wanapokutana,
kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa familia moja, na hivyo
kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.
# JKT limeendelea
kutoa mafunzo maalum kwa makundi mbalimbali ikiwamo ya viongozi wa serikali,
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watumishi wa serikali, ili
kuwajengea maadili mema, ukakamavu na moyo wa uzalendo.
# Pamoja na JKT
kutekeleza jukumu lake la msingi la kuwalea vijana, uzalishaji mali na ulinzi
wa Taifa, kuliundwa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa
(SUMAJKT) mnamo tarehe 01 Julai, 1981 kwa sheria ya uanzishwaji wa mashirika ya
kibiashara katika taasisi za umma. Lengo kuu la kuanzishwa kwake ni kufanya
biashara na kuzalisha faida, ili kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za
JKT, pamoja na kujenga uchumi wa Taifa.
# JKT kupitia SUMAJKT
imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na huduma kupitia
sekta za ujenzi, uhandisi na ushauri, kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda, na
huduma na biashara. Aidha, shirika hili limeshughulika na miradi ya kimkakati
kama ujenzi wa Ikulu Chamwino, na taasisi nyingine nyeti kwa taifa letu.
# Vilevile JKT kupitia
SUMAJKT imekuwa ikichangia katika pato la taifa kupitia uzalishaji mali na
kulipa kodi stahiki kupitia kampuni zake tanzu na miradi mbalimbali. Shirika
limefanikiwa pia kuongeza ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi takribani 36,479
(29,758 ajira rasmi, na 6720 ajira zisizo rasmi) kwa vijana wa kitanzania
kupitia kampuni zake tanzu, viwanda, na miradi mbalimbali.
# Kuanzishwa kwa
mafunzo ya Jeshi la Akiba. Wizara kupitia JWTZ imeendelea kutoa mafunzo ya
jeshi la akiba kwa vijana katika mikoa yote ya Tanzania bara. Jeshi hili la
Akiba limekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea wananchi uzalendo na
kuwapatia ujuzi wa kulinda maeneo mbalimbali muhimu, na hivyo kujenga
mshikamano wa kitaifa. Jeshi hili limeshiriki pia katika shughuli za majanga.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇