LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 19, 2024

SERIKALI SINGIDA KUWASAKA ZAIDI YA 800 WALIOACHA KUTUMIA DAWA ZA KUFUBAZA VIRUSI VYA UKIMWI

Na Ofisi ya RC Singida
Serikali mkoani Singida imeaagiza Waganga Wakuu wa wilaya na wadau wengine wa Afya kuwatafuta na kuwarejesha katika matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi watu 857 wanaoishi navirusi vya ugonjwa huo ambao wameacha kutumia dawa hizo katika Halmashauri za Itigi, Ikungi na Singida.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Tawala wa mkoa huo Dk. Fatma Mganga wakati anafungua kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi wa USAID AFYA YANGU ambao unatekelezwa Singida.

Katibu Tawala huyo amesisitiza kuwekwa kwa mikakati na mipango madhubuti itakayosaidia kurejesha kundi hilo katika matumizi ya dawa hizo haraka iwezekanavyo.

Amesema kuna umuhimu wa kutengeneza mahusiano mazuri kati na Watoa Huduma na Wateja wao ikiwemo kuwapigia simu pindi wanaoona mteja wao hafiki kuchukua dawa ili kujua sababu ambazo zinamfanya asiende kuchukua dawa hizo ili kuona namna bora ya kumsaidia.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa mkoa Dk. Victoria Ludovick ametaja sababu zinazofanya idadi kubwa ya Watu wanaoishi na virusi vya ukimwi mkoani humo kuacha kutumia dawa za kufubaza virusi vya ukimwi kuwa ni pamoja na kuhama na kwenda maeneo mengine na umbali kutoka kwenye makazi yao hadi kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.

Dk. Ludovick amesema mpango uliopo kwa sasa ni kuhakikisha watumiaji hao wanatafutwa popote walipo na kuwapa ushauri nasaha kuhusu umuhimu wa matumizi ya dawa hizo kwa ajili ya afya zao.

Naye, Meneja Mradi wa USAID AFYA YANGU Singida Saidi Mgeleka amesema mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa katika mkoa huo, umeweza kusaidia kuibua watu 700 walioathirika na virusi vya ukimwi kila baada ya miezi mitatu na kuwaazishia dawa haraka. Mradi huo unatekelezwa pia katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dk. Fatuma Mganga, akizungumza kwenye mkutano wa kutathimini maendeleo ya mradi wa USADS AFYA YANGU Mkoani Singida

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages