LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 10, 2024

PPRA YAJIVUNIA KUPATA MAFANIKIO MAKUBWA MIAKA MITATU YA RAIS SAMIA

Mkurugenzi wa Kujenga Uwezo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Amin Mcharo akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, kuhusu mafanikio makubwa waliyopata katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.


Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Zamaradi Kawawa akitoa neno la utangulizi alipokuwa akimkaribisha Mcharo kuzungumza na vyombo vya habari.

Baadhi wanahabari wakiwa makini na kazi yao.

Baadhi ya maafisa wa PPRA 

IMEANDALIWA NA RICHARD MWAIKENDA

 

TAARIFA MAFANIKIO YA MIAKA MITATU YA MHE DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA MAGEUZI MAKUBWA KATIKA UNUNUZI WA UMMA NCHINI 

 

Ndugu wanahabari,

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ina dhamana ya kusimamia  sektaya ununuzi wa umma kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa thamani ya fedha kwenye ununuzi na ugavi; kuhakikisha uzingatiaji wa haki, ushindani, uwazi na kufuatilia uzingatiaji wa sheria kwa taasisi za umma, pamoja na kujenga uwezo katika Ununuzi wa umma kwa kushirikiana na wadau..Pia,Mamlaka ina dhamana ya kuhakikisha Taasisi nunuzi zinatoa upendeleo kwa wazabuni wa ndani katika zabuni za bidhaa, kazi za ujenzi na huduma.

 

Utekelezaji wa malengo ya uanzishwaji wa PPRA umelenga katika kuchangia kikamilifu  maendeleo ya nchi kwa ujumla. Katika kufikia malengo ya uanzishwaji wake, PPRA imeendelea kuandaa mipango na bajeti zake kwa kuzingatia ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), Mpango Mkakati wa PPRA (2021/22 -2025/26) pamoja na makubaliano mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda yenye lengo la kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utoaji wa fursa za ununuzi na ugavi wa umma kwa wazabuni wote wenye nia ya kufanya biashara na Serikali. 

 

Ndugu wanahabari,

Katika kipindi cha Uongozi wa Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mamlaka imewezeshwa kutekeleza vipaumbele mbalimbali katika kusimamia ununuzi wa umma nchini, ambapo imeweza kutekeleza kwa mafanikio makubwa majukumu yake, ikijikita katika maeneo makuu mbalimbali yakiwemo; Ujenzi wa  Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma, kuimarisha Ufuatiliaji na Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, kuwajengea uwezo wadau wa Ununuzi wa Umma,kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023, kujenga jengo la Ofisi ya Makao Makuu na kuanzishwa kwa Ofisi za Kanda.

 

Ndugu wanahabari,

Mamlaka inapenda kuelezea  machache kati ya mengi yaliyofanywa na Rais wetu mwenye maono, utu na mapenzi mema ya kutaka kuona malengo ya uanzishwaji wa PPRA yanatimia kwa mustakabali wa Uchumi na maendeleo endelevu ya nchi yetu.

 

Katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya uongozi wa awamu ya sita, Serikali imetekeleza mambo mengi yanayoigusa sekta ya Ununuzi wa Umma ambayo yamekuwa na matokeo chanya kwa wadau wa sekta na kwa Watanzania kwa ujumla. 

 

1.1.         UJENZI WA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA UNUNUZI WA UMMA (NEST)

Ndugu wanahabari,

Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita (6) chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, umefanyika uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa Mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma unaojulikana kama National e-Procurement System of Tanzania (NeST). Kabla ya uwekezaji huu, ununuzi wa umma ulikuwa ukifanyika kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma uliojulikana kama Tanzania National e-Procurement System (TANePS) ambao ulijengwa na kampuni ya kigeni kutoka Ugiriki. Serikali ilibaini changamoto nyingi  kwenye ununuzi uliokuwa ukifanyika kupitia mfumo wa TANePS ikiwemo taarifa zote za Ununuzi wa umma kuwa chini ya usimamizi wa kampuni ya kigeni nje ya nchi. Changamoto hii na nyinginezo zilipelekea uamuzi wa kuanzisha Mfumo mbadala ambao utakuwa bora zaidi, wenye kuleta tija, unaojengwa na wataalam wa ndani na kusimamiwa na Serikali. 

 

Ndugu wanahabari,

Chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ujenzi wa NeST ulianza rasmi Julai 2022 ambapo kufikia Julai 2023 ulianza kutumika rasmi.

 

 

Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ilianzisha mfumo huu ili kuwezesha michakato yote ya ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya kielektroniki kwa lengo la kuongeza tija, ufanisi, uwajibikaji na uwazi  kwenye utekelezaji wa michakato hiyo.

 

Ndugu wanahabari,

Mfumo wa NeST umeunganishwa na mifumo kumi na saba (17) ya Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupunguza muda na gharama za michakato ya ununuzi, kudhibiti vitendo vya udanganyifu, rushwa na kuzuia ukosefu wa maadili.

 

Ndugu Wanahabari,

Zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali inatumika kwenye ununuzi wa umma, hivyo niwaase wananchi kujisajili katika mfumoNeST na kuomba zabuni mbalimbali zinazotangazwa na Serikali ili kuweza kujipatia kazi na kinachotakiwa ni kuhakikisha anayeomba amekidhi vigezo vinavyotakiwa katika kuomba zabuni husika na pindi wanapopata zabuni wazifanye kwa uadilifu na ufanisi ili waendelee kuaminiwa katika miradi mingine.

 

Ndugu Wanahabari,

Zaidi ya Shilingi Trioni 29 imewekwa kwenye mfumo wa NeST kwa ajili ya kufanya ununuzi wa bidhaa, hudumana kazi za ujenzi, huku hadi kufikia Aprili09, 2024 mikataba ya zaidi ya Shilingi Tilioni 5.14 imetolewa kwa wazabuni kupitia mfumo wa NeST, ambapo wazabuni 18,101 wamejisajili kwenye mfumo huo.

 

1.2.         UWEZESHAJI MAKUNDI MAALUM KATIKA JAMII

Ndugu wanahabari,

Serikali ya awamu ya sita imewekeza katika kunyanyua wananchi wake kiuchumi kwa kuhakikisha inatoa fursa kwa Makundi Maalum wakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. Ili kufikia lengo hilo, Mamlaka imewajengea uwezo Makundi Maalum na imekamilisha tafsiri ya miongozo miwili inayotumika katika ununuzi wa Umma, ambayo ni mwongozo wa ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa Umma na mwongozo wa ushirikishwaji wa jamii katika ununuzi wa Umma. Pia, imetafsiri  nyaraka sanifu tatu za zabuni za ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma, nyaraka sanifu moja ya zabuni za ushiriki wa jamii katika ununuzi wa umma.

 

Ndugu wanahabari,

Kufuatia ushiriki wa makundi maalum katika ununuzi wa umma hadi kufikia Februari 2024, jumla ya tuzo za mikataba zenye thamani ya shilingi bilioni 1.95 zimetolewa kwa makundi maalum kupitia zabuni za umma zilizotangazwa na taasisi  nunuzi kupitia mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (NeST), ambapo kundi la vijana wamepata tuzo za mikataba zenye thamani ya shilingi milioni 709 , wanawake shilingi bilioni 1.2 na wazee shilingi milioni 78.3.

 

1.3.         KUJENGA UWEZO KWA WADAU

Katika juhudi za kujenga uwezo kwa wadau wa ununuzi wa umma, PPRA imeendesha mafunzo maalum kuhusu sheria ya ununuzi wa Umma, matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma, mikataba na zana za kutekeleza ununuzi kwa Taasisi za Umma, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, makundi maalum, wazabuni na wadau mbalimbali.

 

Mafunzo haya yaliyotolewa yameongeza kwa kiasi kikubwa uelewa wa sheria ya ununuzi wa umma Sura Na. 410 na matumizi ya mfumo wa kielektroniki.

 

Ndugu wanahabari,

Serikali imeweka kipaumbele katika utafiti wenye lengo la kubaini changamoto zinazoikabili sekta ya ununuzi na kutafuta suluhisho la namna ya kukabiliana nazo. Katika utekelezaji wa lengo hilo, Serikali imeiwezesha Mamlaka kuandaa sera ya tafiti na agenda iliyoainisha maeneo muhimu ya kufanya utafiti katika ununuzi wa umma. Baadhi ya tafiti zilizofanywa na Mamlaka na kukamilika ni pamoja na: i)Tafiti kuhusu changamoto na fursa katika ununuzi wa umma ili kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya ununuzi wa umma; ii)  Ushiriki wa Kampuni za biashara zinazoongozwa na wanawake katika zabuni za Umma, ambapo ilibainika kuwa moja ya vikwazo vikubwa vinavyozuia ushiriki wa kampuni hizi za wanawake ni kushindwa kupata dhamana ya zabuni inayotakiwa. Sheria mpya imeweka mazingira ya upendeleo maalum ya kampuni hizi. Aidha, Mamlaka imekamilisha tafiti ndogondogo (Surveys) katika matumizi ya taratibu ya ununuzi kwa njia ya Force Account ambapo ilibainika kuwa kuna matumizi ya njia hii yasiyoendana na Sheria na Kanuni inavyoelekeza. Sheria mpya ya Ununuzi ya Mwaka 2023 imeboresha matumizi ya utaratibu huu.

 

1.4.         KUONGEZEKA KWA KAGUZI NA UOKOAJI WA FEDHA ZA UMMA

Mamlaka imekuwa ikifanya Kaguzi na uchunguzi mbalimbali na mapambano dhidi ya rushwa kwenye taasisi nunuzi. Lengo la kazi hii ni pamoja na kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka na viashiria vya rushwa. Mara baada ya uchunguzi kukamilika, Mamlaka hutoa taarifa zake kwa taasisi nunuzi na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa.

 

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (6), Mamlaka ilifanya uchunguzi kwa zabuni zilizotekelezwa katika mwaka wa fedha 2021/22 na 2022/23, na kufanikiwa kuokoa jumla ya fedha za umma kiasi cha Shilingi Bilioni 16.27.Kati ya fedha hizo,  kiasi cha Shilingi Bilioni 13.83 ilitokana na kuingilia kati kwa Mamlaka kwenye mikataba ambayo ilitolewa kwa wazabuni wenye bei ya juu wakati wenye bei ya chini wakitolewa kwenye mchakato (disqualified) na kiasi cha Shilingi Bilioni 2.44 ni kiasi kilichorudishwa na wasambazaji wa bidhaa (suppliers) na wakandarasi kwa malipo ya ziada yaliyofanywa na Taasisi Nunuzi.

 

1.5.         KUTUNGWA SHERIA MPYA (SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA NA. 10 YA MWAKA 2023)

 

Ndugu Wanahabari

Wote tunafahamu dhamira ya Mhe. Rais kuhusu kuhakikisha matumizi mazuri na sahihi ya fedha za umma kwa manufaa mapana ya Taifa na Watanzania wote kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo miradi ya ujenzi wa hospitali, shule na barabara. Hivyo, katika kuhakikisha hilo na kwakuzingatia kwamba zaidi ya asilimia 70 ya fedha za bajeti ya Serikali kwa mwaka hutumika kupitia ununuzi wa umma, Mamlaka kama taasisi yenye jukumu la udhibiti wa ununuzi wa umma nchini, ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki katika kufanya mapitio ya Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 chini ya Wizara ya Fedha na hivyo kupelekea kutungwa kwa Sheria mpya ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023. Sheria mpya iliidhinishwa na Mhe. Rais kuwa Sheria rasmi tarehe 29 Septemba 2023 na kutangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 40 Vol.104 la tarehe 6 Oktoba 2023. Sheria hiyo mpya itaanza kutumika rasmi tarehe itakayotangazwa rasmi na Waziri wa Fedha kupitia Tangazo la Serikali.

 

Kufuatia kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ambayo bado haijaanza kutumika rasmi, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) inaendelea kukamilisha uandaaji wa Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024 ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria hiyo mpya. Pamoja na mambo mengine, Sheria mpya imetungwa kwa lugha ya kiswahili kwa urahisi wa uelewa na tafsiri kwa lugha mama ingawa pia itatafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza. Zaidi, Sheria hiyo imeweka mazingira rafiki zaidi yanayolenga kuhakikisha upatikananji wa thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa ununuzi wa umma nchini ikiwemo: kupunguza muda wa mchakato wa zabuni; kuondoa sharti la nyongeza ya adhabu kwa kampuni zilizofungiwa nje ya nchi; kuweka mazigira rafiki zaidi kwa makundi maalumu, vijana, wanawake na wazee katika kushiriki kwenye zabuni za umma; kuongeza fursa za upendeleo kwa watu na kampuni za ndani; kufungamanisha mnyororo mzima wa ununuzi na ugavi; matumizi ya bei kikomo kwa bidhaa na huduma zenye bei kikomo; kupunguza mlolongo wa uidhinishaji katika michakato ya zabuni; undaaji na uwasilishaji wa taarifa ya tathimini ya ununuzi wa umma kwa Mhe. Rais; kuweka sharti la lazima kuchakata zabuni za umma kupitia mfumo wa ununuzi kielektroniki lengo ikiwa kuongeza uwazi, ufanisi na kupunguza uwezekano wa rushwa katika zabuni za umma. Zaidi, Sheria imeweka ukomo wa utekelezaji miradi ya kazi za ujenzi kwa matumizi ya rasilimali za ndani (Force Account).

 

Ndugu Wanahabari

Kipekee, Sheria hii imeweka masharti muhimu yatakayohakikisha uwepo wa upendeleo wa bidhaa na wazabuni wa ndani, ambapo inatarajiwa kuwa zabuni zote zilizo chini ya Bilioni 50 zitafanywa na wazawa. Hatua hii italeta mageuzi makubwa kwa wakandarasi, watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa wazawa ambapo sehemu kubwa ya bajeti ya Serikali katika ununuzi wa umma itaenda kwako. Aidha, Sheria hiyo imeweka masharti yanayoruhusu Kampuni za wazawa kuungana ili kufikia mahitaji ya zabuni husika. Pamoja na hayo, Sheria imeweka masharti kuwa endapo kampuni ya mzawa imeungana na Kampuni ya kigeni, Kampuni ya Mzawa itakuwa ndiyo Kampuni Kiongozi (Leading Company) katika ubia tofauti na hali ilivyo sasa.

 

1.6.         UWEZO WA KUCHUKUA HATUA KWA WANAKAOKIUKA SHERIA YA UNUNUZI

 

Ndugu Wanahabari,

Kutokana na umuhimu wa kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake katika ununuzi wa umma, Mamlaka ilifanikiwa kupata kibali cha  kuendesha mashataka yanayotokana na ukiukwaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma kupitia Wanasheria wake. Hii ni katika kuhakikisha kwamba, Mamlaka inasamia ipasavyo utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma na kuhakikisha kwamba hatua stahiki za kisheria zinachukuliwa haraka dhidi ya ubadhirifu utakaofanyika kupitia ununuzi wa umma.

 

1.7.         KUIMARISHAUSHIRIKIANO NA TAASISI NYINGINE KATIKA UDHIBITI  UNUNUZI WA UMMA

Kwa kuzingatia umuhimu wa taasisi za umma kubadilishana uzoefu na pia kushirikiana katika kutekeleza malengo ya Mhe. Rais hususani suala la kufanya kazi kupitia kaulimbiu yake ya “KaziIendelee”, Mamlaka, kwa kupitia vikao vya pamoja na kusaini Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding – MoU) imeweza kuongeza ushirikiano baina yake na taasisi nyingine kwa lengo la kubadilishana uzoefu, ushirikiano na kuongeza ufanisi katika kazi. Kwa mfano, Mamlaka imefanikiwa kufanya kikao cha pamoja na Mamlaka ya Uendelezaji Ununuzi wa Umma Zanzibar (ZPPDA) kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili kupitia MoU ambayo itasainiwa siku za usoni. Pia, Mamlaka ilifanikiwa kusaini MoU na NEEC kwa lengo la kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu katika kushiriki fursa zinazotokana na ununuzi wa umma. Aidha, Mamlaka na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) zilisaini MoU kwa lengo la kuongeza ushirikiano katika kupambana na rushwa kwenye ununuzi wa umma.

 

1.8.         UJENZI WA JENGO JIPYA LA MAMLAKA

Ndugu wanahabari,

Serikali ya awamu ya sita imeiwezesha Mamlaka kujenga jengo la ofisi za Makao Makuu jijini Dodoma lilipo Barabara ya Ununuzi, Eneo la NCC, Mtaa wa Tambukareli. Jengo hilo limekamilika na tayari Mamlaka imehamishia shughuli zake katika jengo hilo  kutoka katika Jengo la Kambarage Tower ambapo ilikuwa imepanga kwa muda mrefu.

 

1.9.         KUANZISHWA KWA OFISI MPYA ZA KANDA

Ndugu wanahabari,

Katika kuhakikisha kwamba Mamlaka inaboresha na kusogeza huduma zake kwa wadau wa Sekta ya Ununuzi, Serikali ya awamu ya sita imewezesha uanzishwaji wa ofisi mpya za Kanda tano na hivyo kufanya Mamlaka kuwa na ofisi sita za Kanda ambazo ni Kanda ya Pwani inayojumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro. Makao Makuu ya Kanda hii yapo Dar es Salaam; Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga. Makao Makuu ya Kanda hii yapo Arusha; Kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Makao Makuu ya Kanda hii yapo Mtwara; Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa. Makao Makuu ya Kanda hii yapo Mbeya; Kanda ya Kati na Magharibi inayojumuisha mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga, Katavi na Kigoma. Makao Makuu ya Kanda hii yapo Tabora; Kanda ya Ziwa inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera na Mara. Makao Makuu ya Kanda hii yapo Mwanza. Aidha, Mkoa wa Dodoma haupo katika orodha ya Kanda kwa kuwa utahudumiwa na Ofisi za Makao Makuu. 

 

Ndugu wanahabari,

Hivi ndivyo PPRA imekuwa ikitekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwahudumia wananchi ili kutimiza lengo la Serikali iliyopo madarakani  ya kupeleka huduma kwa wananchi na kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi na teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo, kama inavyoonyesha katika Sura ya kwanza,Kipengele cha 8(e) ya Ilani hiyo wakati sura hiyohiyo kipengele cha 8 (f) ikielezea kujikita katika  kutengeneza ajira zisizopungua milioni 8 katika sekta rasmi na zisizo rasmi kwa ajili ya vijana.

 

Kazi Iendelee.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages