LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 23, 2024

MIAKA 60 YA MUUNGANO NA RAIS DK. SAMIA ANAVYOING'ARISHA NCHI

Ibrahim Bakari, Official CCM Blog
Aprili 24, mwaka 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda kitu kimoja hivi kinachoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hiyo ni baada ya kuchanganywa udongo, ule wa Tanganyika na Zanzibar kwa ajili ya kufanya kitu kimoja, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume ndiyo waliofanya kazi hiyo hadi kuchanganywa udongo wa pande zote mbili.

Katika miaka 60 ya Muungano, yamefanyika mambo mbalimbali katika awamu tofauti, lakini awamu ya sasa chini Dk Samia Suluhu Hassan, imezidi kuung'arisha Muungano huu.

Mwaka 1995 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Kilimanjaro, Jijini Dar es Salaam. Mwalimu Nyerere alisema Muungano wetu una nyufa nyingi zinazohitaji kuzibwa.

Aliufananisha Muungano na kuta za nyumba akiongezea kuwa nyufa nyingine ziko kwenye dari. Kikubwa alionyesha wapi pana legalega na nini cha kufanya kuuimarisha Muungano.

Kero za Muungano pamoja na kuanza kushughulikiwa kwa nyakati tofauti, lakini Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuzipunguza zaidi kutoka zilizokuwa 25 hadi kubakia nne.

Katika kikao cha Machi 5, 2024 kilichofanyika Nyamanzi, Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Suleiman Jaffo amesema kero za Muungano zimetatuliwa kutoka 25 na sasa zimebaki nne.

Amesema watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wenzao wa Bara wako kwenye hatua mbalimbali kuona namna gani wanamaliza kero hizo.

Hoja au kero zilizosalia ni pamoja na suala la sukari, usajili wa vyombo vya moto na bodi ya pamoja ya mgawanyo wa mapato ya iliyokuwa sarafu moja ya Afrika Mashariki.

Ukiacha kero, Tanzania imedumu kwenye amani, umoja na utulivu ambavyo ndizo tunu tulioachiwa kutoka kwa waasisi wa taifa la Tanzania, Amani Karume na Julius Nyerere.

Kila mahali walikuwa wakihubiri amani ambayo kwa sasa kijiti amekikamata Mwanamama shupavu, Dk Samia Suluhu.

Ni dhahiri shahiri Tanzania katika miaka 60 ya Muungano, imeendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano ikilinganisha na baadhi ya mataifa na mengine jirani ambayo yamekosekana utulivu kiasi cha Umoja wa Mataifa kupeleka majeshi kwa ajili ya kulinda amani.

Amani inatuliza akili kwa mwanadamu wa kawaida kufanya kazi kwa ufanisi, kuzalisha mali na hata kuwa na fikra za utekelezaji wa majukumu ya maendeleo.

Zaidi ya hayo, katika miaka 60 ya Muungano, Rais Dk Samia amezidi kuutakasa Muungano kwa kupigania huduma muhimu za kijamii kwa wananchi.

Baadhi ya mambo anayoyapigania ni pamoja na upatikanaji wa huduma za afya ambazo amezigawanya kwa makundi.

Makundi hayo ni pamoja na wazee, mama wajawazito na wenye watoto kwamba kila mmoja ana nafasi yake kupata huduma katika vituo vya afya, zahanati na hospitali.

Rais amehakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kundi la wazee na ameelekeza huduma zitolewe bure.
Wakati akizungumza na wazee mkoa wa Dar es Salaam Mei 5, 2021 aliwasisitiza wazee kwa kuwaeleza kuwa wanapaswa kupata huduma za afya bure.

Hata hivyo kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya watekelezaji wa maagizo hayo ambao ndio hao wanaowachonganisha wananchi na Serikali yao.

Huduma nyingine muhimu anazopigania ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama na lengo ni kumtua mama ndoo katika miaka 60 ya Muungano.

Ndio maana Wizara ya Maji ikapelekewa bajeti kubwa ya Sh. Bilioni 756.2 kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama na zaidi ni kumtua ndoo mama.

Pia katika mwaka wa fedha 2023/2024 Rais Dk Samia aliridhia mpango wa ukamilishwaji wa miradi 1,546 ya maji katika mikoa 25 ya Tanzania.

Hadi kufikia Disemba 2023, jumla ya miradi 374 iliyogharimu Sh 128,177,655,882 ilikuwa imekamilika na Serikali inaendelea na ukamilishaji wa miradi mingine 1,172 kupitia Wakala wa maji na Usafi wa Mazingira ‘RUWASA’.

Fedha nyingi zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji, miundombinu yake, uchimbaji visima na uboreshwaji na ufufuaji wa DP.

Aidha, katika miaka 60 ya Muungano, Rais Samia anataka kuona hadi nyumba za tembe zinapata nishati ya umeme na ndio maana anapambana kukamilishwa kwa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere, JNHPP, ambapo mpaka sasa asilimia kubwa limefika pazuri.

Kuonyesha awamu ya sita iko imara, tayari mashine mbili zimewashwa kwa majaribio huku umeme wa megawati 235 ukiingizwa gridi ya taifa.

Kwenye elimu, katika miaka 60 ya Muungano, suala la elimu ni Watanzania wenyewe washindwe kupeleka watoto shule kwani elimu bure ni kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

 Baada ya kupata fedha za Uviko 19, alizitawanya  katika kila mikoa kujenga shule mpya ikiwa ni uimarishwaji wa miundombinu ya kusomea pamoja na madawati. Hapo hapo elimu ni bure.

Kuna maeneo mengi ambayo katika miaka 60 ya Muungano yameimarishwa zaidi katika awamu ya sita kama kilimo, maliasili, utalii, biashara na  uhusiano wa kimataifa.

Pia, uimarishwaji wa diplomasia ya uchumi ikiwemo uwekezaji, uwezeshwaji wa makundi ya kijamii, ujenzi wa miundombinu ya barabara na utoaji haki.

Pamoja na mazuri yanayofanyika awamu ya sita,  tatizo lipo kwa baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakimwangusha Rais kwa kutokuwajibika.

Mfano mdogo ambao tunauona, ni katika ziara za Waziri Mkuu mikoani amekuwa akiagiza kama si polisi kukamata basi Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa TAKUKURU kufanya uchunguzi katika jambo fulani.

Hapa ndipo tunapowaona baadhi ya watendaji kujisahau na kutotelekeza ama kufuatilia masuala muhimu ya kijamii.

Hongera Dk Samia kwa maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages