LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 21, 2024

MAJANGA: SIMBA YAACHILIA KWA YANGA POINTI ZOTE 6 NA MABAO 7-2

Ibrahim Bakari, CCM Blog
Makosa ya kiufundi yaliyofanywa na mabeki wa Simba jana yaliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa nje ndani wa mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyorindima kwenyedimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kufuatia matokeo hayo, Yanga imejitengenezea nafasi ya kutetea ubingwa baada ya kufikisha pointi 58 huku Simba ikisalia na pointi zake 46, huku Simba ikiendelea kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC huku Azam ikikamata nafasi ya pili ikiwa na pointi 51.

Mwendelezo huo wa Yanga, umeifanya Simba kuachilia kwa Yanga pointi zote sita na mabao 7-2 katika msimu huu, kutokana na kupigwa mabao matano (5) kwa bao moja (1) katika mchezo wa kwanza Novemba 5 mwaka jana.

Katika Mchezo wa jana, Yanga ilipata bao la kuongoza lililotokana na mkwaju wa penalti iliyofungwa na Aziz Ki baada ya kufanyiwa madhambi na Hussein Kazi aliyeingia muda mfupi tu kuchukua nafasi ya Henonga Baka aliyeumia.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Maxi Mpiya Nzengeli ambaye alitumia mwanya wa mabeki wa Simba kupanda na Yanga kufanya shambulizi la kushtukiza na mpira kumkuta mfungaji.

Kadiri muda ulivyokuwa ukisogea kila upande ulifanya mabadiliko kabla ya Simba kupata bao dakika ya 75 kwa bao la Fred Koblan baada ya kuwachekecha mabeki wa Yanga na kuukwamisha mpira wavuni.

Simba nusura ifungwe bao dakika ya 78, kama Kennedy Musonda angekuwa makini kwa kuwa alibaki na kipa Ayoub Lakred ambaye aliucheza mpira wake na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuzaa matunda.

Hadi mwisho matokeo yalibaki 2-1 kwa Simba kupoteza mchezo huo.

Wakati Yanga ikishinda mchezo huo, kile kilichokuwa kinatarajiwa, kimetokea kwa Yanga kupata ushindi katika mchezo wake dhidi ya watani wao Simba kwa kuwalaza mabao 2-1 ikiwa ni mara ya pili baada ya ushindi wa mabao 5-1 Novemba 5, mwaka jana.

Mechi ya Yanga na Simba

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages