LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 6, 2024

JUMUIYA KUU YA WABAPTIST TANZANIA YAIOMBA SERIKALI KUWASHULIKIA MATAPELI WANAOGUSHI NYARAKA FEKI

 Na Lydia Lugakila, 

Mwanza


Jumuiya ya wabaptist Tanzania yaiomba Serikali kuwashughulikia mara moja wasambazaji vyeti feki na nyaraka feki.


Jumuiya kuu ya Wabaptist Tanzania imeendelea kukerwa na tabia ya baadhi ya watu kutoka kundi ambalo limeendelea kukiuka maadili ya ki Mungu kwa kueneza uongo kwa waumini ikiwemo kugushi nyaraka zilizogunduliwa  kupitia mitandaoni ambazo ni feki jambo lililoendelea kuleta taharuki kwa waumini wa dhehebu hilo na kuleta uchonganisha kati ya jumuiya kuu ya Wabaptist Tanzania, Serikali na jamii kwa ujumla.


Hayo yalielezwa katika kikao cha Kamati kuu ya Wabaptist Tanzania kilichofanyika April 04, 2024 Nyamanoro Mkoani Mwanza ambacho kililenga kujadili mambo mbali mbali ikiwemo kuona namna ya watumishi wa Mungu watakavyotunza Kanisa na kuendelea kufanya kazi ambayo Yesu Kristo aliwaachia ya kupanda Makanisa na kuwafanya wengine kuwa Wanafunzi wake Yesu.


Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Jumuiya kuu ya Wabaptist Tanzania mchungaji Barnabas Michael Ngusa alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya uwepo wa nyaraka ambazo zinatoka na kuonekana kama ni za kiserikali ambapo nyaraka nyingi walizojaribu kufuatilia Serikalini zimegundulika kuwa feki.


"Sisi hatujui kiundani nyaraka hizi zinatoka wapi lakini tunajaribu kutoa taarifa kwenye Ofisi za Serikali husika lakini hatujaona hatua yoyote iliyochukuliwa licha ya kuwa tunajua na kuamini Serikali ipo inafanya kazi"alisema Mchungaji Barnabas.


Mwenyekiti huyo wa Jumuiya kuu ya wabaptist Tanzania aliongeza kuwa muhusika huyo ameendelea kuwarubuni watu kuwa ana cheti kipya huku akiwachangisha pesa kwa ajili ya kununua cheti ambacho wao wanamini sio cheti killichotolewa na Ofisi ya msajili.


"Taarifa za vyeti vinavyosambaa  mtandaoni tutazipeleka moja kwa moja kwenye ofisi za Serikali ili tujue kama Serikali imezitoa kweli" alisema mtumishi huyo wa Mungu.


Mchungaji Ngusa Alisema anaamini Serikali ya Rais Samia ipo kazini licha ya uwepo wa baadhi ya watu wasio waaminifu (Matapeli) huku akitoa wito kwa wasambazaji wa nyaraka feki na vyeti bandia kuacha tabia hiyo mara moja kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa maadali na misingi ya madhehebu ambapo pia aliwaomba watumishi wa Mungu kutoyumbishwa na upepo wa aina yoyote bali wasimame imara katika kazi ya Mungu kwani yote hayo ni mapito.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya kuu ya Wabaptist Tanzania mchungaji Elias Kashambagani alisema kwa miaka 50 sasa wamekuwa na Jumuiya kuu ya Wabaptist iliyo nzuri lakini kwa miaka minne hadi mitano imetokea vurugu kutokana Msajili kutoa cheti kwa shirika jingine la Baptist kwa Kutumia namba zile zile wanazotumia wao huku akidai jambo bado lipo kwenye Ofisi  ya katibu Mkuu Wizara ya mambo ya ndani hivyo wanasubiri majibu.


Mchungaji Kashambagani aliongeza kuwa watu hao wamekuwa wakifanya vikao wakiisaliti Jumuiya kuu ya wabaptist Tanzania na  kuichonganisha Serikali huku akisisitiza  kuwa Serikali inatakiwa kuwa  macho katika kuwazuia watu hao ili waache tabia hiyo ambapo pia aliwahimiza watumishi wa Mungu kuwa wavumilivu, kutokakata tamaa ikiwemo pia kuwaelimisha vyema Waumini wa Jumuiya kuu ya Baptist Tanzania kuendelea kuwasikiliza na kuwaamini Viongozi wao waliochaguliwa ki halali na Jumuiya kuu ya Wabaptist Tanzania na sio kuwasiliza watu wasio waaminifu katika kazi ya Mungu.


Hata hivyo baadhi ya watumishi wa Mungu akiwemo mchungaji Zephania Nasal kutoka Kanda ya Kaskazini, mchungaji Dioniz Karwani kutoka Kanda ya ziwa Mchungaji Boniphace Kidede kutoka Kanda ya Magharibi, Mchungaji Oscar John kutoka Kanda ya ziwa na mchungaji Philmon Rushona wamelaani na kukerwa na matukio ya namna hiyo ya watu wanaosambaza nyaraka feki na kudai kuwa Hali hiyo imekuwa yenye  usumbufu kwa waumini wao kwani watu hao wamejitafutia pesa kwa kuyaibia Makanisa huku wakijua ni kinyume na sheria na miongozo ya madhehebu.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages