Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Yessaya Mwakifulefule akimkabidhi Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda tuzo ya mshindi wa pili wa kutoa huduma kwa jamii ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo (Corporate Social Responsibility) iliyotolewa na Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST).
Washindi wa tuzo za heshima za uhusiano na mawasiliano zilizotolewa na Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania.(PRST) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeshinda tuzo mbili za heshima za uhusiano na mawasiliano katika kutoa elimu kwa umma kuhusu magonjwa ya moyo (Public Services Campaign) na kutoa huduma kwa jamii ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo (Corporate Social Responsibility) zilizotolewa na Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST).
Tuzo hizo zimetolewa jana jijini Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa St.Peter’s na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imeshinda tuzo hizo kupitia huduma za tiba mkoba zinazojulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inazozifanya kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo. Hadi sasa Taasisi hii imeshaifikia mikoa 13 ya Tanzania bara na visiwani na kufanya upimaji kwa watu 11,254.
Upimaji huo unakwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa umma kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo na matumizi sahihi ya dawa za moyo, kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa jinsi ya kuwatambua wagonjwa wa moyo na kufanya utafiti wa magonjwa ya moyo.
Ushindi huo pia umetokana na mchango mkubwa unaotolewa na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano katika kuuhabarisha umma kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi pamoja na kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇