LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 6, 2024

BALOZI DK. NCHIMBI AELEZA MSIMAMO WA CCM KWENYE DIPLOMASIA YA UCHUMI NA SIASA TANZANIA, NI ALIPOZUNGUMZA NA MABALOZI NA MKURUGENZI MKAZI FES

Lumumba, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema CCM, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutoa uongozi na kusimamia ili kuhakikisha diplomasia ya uchumi na siasa inaendelea kuiwezesha Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana ndani na nje ya nchi.

Balozi Dk. Nchimbi amesema, mabadiliko mbalimbali ya kisera na mwelekeo, chini ya Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Dk. Samia, yameendelea kuwa sehemu ya dira ya Tanzania katika kutafuta matokeo chanya ya haraka yanayolenga kuhakikisha Tanzania inakuwa mnufaikaji sawa katika uhusiano unohusisha pande mbili, kila wakati, iwe kati ya nchi na nchi au nchi na taasisi za kimataifa.

Ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wanaoziwakilisha Nchi zao hapa nchini, Balozi wa Misri
Balozi Sherif Abdelhanid Ismail na Balozi Kim Yong Su wa Korea Kaskazini, na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Friedrich-Ebert-Stiftng (FES), nchini, Bi. Elisabeth Bollrich, Ijumaa, Aprili 5, 2024, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Balozi Sherif Abdelhanid Ismail amemhakikishia Balozi Dk. Nchimbi kuwa Nchi ya Misri, chini ya uongozi wa Rais Abd el-Fattah Saeed Hussein Khalil el-Sisi, inaichukulia Tanzania kuwa mmojawapo wa washirika wake wa karibu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ikizingatiwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na ushirikiano katika miradi mikubwa yenye athari chanya kwa uchumi wa pande zote mbili.

Naye Balozi Kim Yong Su katika mazungumzo yake na Balozi Dk. Nchimbi alisema kuwa Nchi ya Korea Kaskazini, chini ya Rais Kim Jong Un, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea (WPK), kinachoongoza nchi hiyo, ambacho ni chama rafiki na CCM, siku zote imekuwa tayari kudumisha na kuenzi urafiki na uhusiano wa nchi hizo mbili na vyama hivyo viwili, uliowekewa misingi imara tangu wakati wa Kiongozi wa Kwanza wa Korea Kaskazini, Komredi Kim Il Sung na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.  

Aidha, Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya FES, Bi. Elisabeth Bollrich, pamoja na masuala mengine alimwelezea Balozi Dk. Nchimbi jinsi ambavyo FES imekuwa ikifanya kazi nchini, ambapo Katibu Mkuu huyo wa CCM alimhakikishia ushirikiano kwa masuala yenye maslahi kwa Tanzania.

Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na Balozi wa Misri hapa Nchini Sherif Abdelhanid Ismail, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam, jana.
Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akiagana na Balozi wa Misri hapa Nchini Sherif Abdelhanid Ismail, baada ya mazungumzo yao, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam, jana. 


Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza Balozi wa Korea Kaskazini Kim Yong Su, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam, jana,

Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Friedrich-Ebert-Stiftng (FES), Elisabeth Bollrich, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, jana.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages