LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 26, 2024

DK. SAMIA ALIHUTUBIA TAIFA, ASEMA MUUNGANO UMELETA MAGEUZI TANZANIA, ASISITIZA ULINDWE

Na Ibrahim Bakari, Official CCM Blog

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali nchini.

Akilihutubia taifa Aprili 25, 2024, jioni, kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano ni leo Aprili 26, 2024, amesema Muungano ulikumbwa na mitikisiko, lakini leo unatimiza miaka 60 ukiwa na mafanikio.

Amesema kati ya mageuzi makubwa ya Muungano, ni pamoja na kutambuliwa kwa haki za binadamu kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Aidha amesema Muungano umerejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992 pamoja na uanzishwaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora sanjari na utekelezaji kazi wa mihimili mitatu ya dola bila kuingiliana.

Amesema ndani ya Muungano kulizaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) 1977 na kuweka msingi unaoakisi Muungano wa Tanzania kwani chama hicho ni baada ya kuunganishwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP) kilichokuwa Zanzibar.

Dk. Samia amesema kwa sasa wamekuja na falsafa ya 4R ambayo imefanya mapitio ya masuala mbalimbali ikiwemo mfumo wa Haki jinai, uhuru wa kujieleza na vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa uhuru.

Kingine ni mabadiliko katika Sheria za Uchaguzi, Vyama vya Siasa na Sheria ya Tume ya Uchaguzi.

Kwa upande wa Diplomasia, amesema Muungano umewezesha Tanzania kuwa na ushawishi kikanda na kimataifa ikiwemo kukuza diplomasia na mataifa, kushiriki harakati za ukombozi na usuluhishi wa migogoro ukanda wa Maziwa Makuu.

Kuhusu kilimo, Dk. Samia amesema wakati nchi hizi zinaungana, kiuchumi zilikuwa katika kiwango duni cha maendeleo na kilimo kilikuwa chini sanjari na huduma za kijamii kama elimu, afya, maji na umeme.

 Amesema kuondokana na uduni huo, jukumu la kwanza lilikuwa kujenga uchumi endelevu na  kuongeza kipato cha wananchi.

Aidha amesema Juhudi zimefanyika kukuza pato la taifa na kufikia sh. trilioni 170 kwa takwimu za 2022 na pato la mtu mmoja mmoja kufikia sh. Milioni 2.8 kwa mwaka.

Ameelezea kufarijika Tanzania kufikia uchumi wa kati katika ngazi ya chini na lengo ni kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu sanjari na kuongezeka kwa umri wa kuishi kutoka miaka 45 hadi 67.

Akizungumzia elimu ya juu, amesema katika miaka 60 ya Muungano, kumejengwa vyuo vya elimu ya juu 49, ikiwemo 19 vya umma na 30 vya binafsi na Zanzibar ikiwa na vyuo vikuu vitatu.

Amesema mpaka sasa Serikali imetoa sh. trilioni 6.69 ikiwa ni mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa pande zote.

Dk. Samia amesema kila penye umoja changamoto hazikosekani na katika miaka 60, Muungano ulikumbwa na changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii ambazo zilitafutiwa ufumbuzi na kuimarisha kuuimarisha.

 Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia amewataka Watabzania hususan  vijana kuulinda, kuuendeleza Muungano anbao ni  urithi ulioachwa na waasisi wa taifa hivyo kila mmoja anatakiwa kuudumisha Muungano huo.



No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages