Ibrahim Bakari, CCM Blog
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema uadilifu kwa baadhi ya watu umetoweka ndio maana wanaoongelea nafasi za uongozi leo, akili zao zinawapeleka kwenye kwenda kupiga dili.
Dk. Nchimbi ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 102 ya kuzaliwa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere leo Aprili 9, 2024, kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kivukoni Dar es Salaam.
Amesema robo tatu ya watu wanawaza kupiga dili kwenye uongozi na kusahau uadilifu na kuweka wazi kuwa uadilifu kwa waliowengi umepotea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujisahaulisha misingi ya uadilifu iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere kuwa kazi ni kipimo cha utu.
Balozi Dk. Nchimbi amesema Mwalimu aliliona na kuanzisha chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyarere (Chuo cha Kivukoni wakati huo) kwa ajili ya kuwapika viongozi wa kuwatumikia Watanzania. Alikisifu chuo hicho pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa, (JKT) kwa kutengeneza Watanzania waadilifu.
Akimmwagia sifa Baba wa Taifa, Balozi Dk. Nchimbi amesema hata wakati anaachia madaraka mwaka 1985, alimtafuta mtu mwadilifu, eneo ambalo hakuwa na mashaka nalo.
Amesema alimteua Edward Sokoine ambaye alikuwa mwadilifu na alimpeleka shule ya uadilifu kuongeza ustadi na aliporejea alipewa Uwaziri Mkuu, akatingisha mabepari na wahujumu uchumi. Sokoine alifariki kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984 eneo la Dumila mkoani Morogoro.
Akikazia kwenye uadilifu, Balozi Dk. Nchimbi amesema kuna haja ya kuanzishwa vyuo vingi kwa ajili ya kuibua uadilifu na si kuendelea kupanua Kivukoni (Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere).
Aidha ametaka mitaala ya uadilifu katika chuo hicho kuboreshwa na kufundisha watu wa vyama vyote kwa kuwa Tanzania inataka watu walioiva kuongoza taifa.
Balozi Dk. Nchimbi, amesema bila uadilifu, taifa linaweza kuandaa watu ambao wanajua mchezo wao unaweza kuwa mauti kwa taifa letu kwani wanaweza kuliingiza taifa katika vurugu, mauaji na vita kwa sababu tu hawakuandaliwa.
Akaasa kuwa, wakati umefika sasa kwa vyama vya siasa (CCM na wapinzani) kukaa pamoja na kuona namna ya kuwa na taasisi ya elimu kwa viongozi wao na wajipange kuongoza Watanzania kwa misingi ya amani, umoja na mshikamano na kujenga uadilifu miongoni mwa viongozi wa vyama vya siasa.
Katika hotuba yake hiyo iliyochukua dakika 34, Balozi Dk. Nchimbi amesema amani, umoja na mshikamano havikununuliwa au kuokotwa, vilitengenezwa na viongozi wa vyama na ndio maana leo hii Tanzania iko hapa.
Akifananisha 4R za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na kauli ya maendeleo kuletwa na Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora, amesema vyote vina nia ya kujenga taifa moja lenye mshikamano na kuleta maendeleo.
Amewataka Watanzania kutokuweka matabaka ya rangi, kabila, walionacho na wasionacho kwa kuwa hakuna Mtanzania bora kuliko mwingine.
Kwa upande mwingine, Balozi Dk. Nchimbi, amesema Mwalimu Nyerere alifundisha uwajibikaji kwa kila mmoja mahali alipo katika kazi na alihimiza uongozi wa pamoja.
Amemsifu Mwalimu kuwa alikuwa kiongozi ambaye huwezi kumtilia shaka kwani katika uadilifu aliusimamia na tunatakiwa kuuishi uadilifu wake.
Mapema Mwanasiasa Mkongwe, Steven Wassira alisoma kwa kifupi historia ya Mwalimu na kuelezea uadilifu wake katika utumishi wa taifa la Tanzania.
Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika kongamano hilo ambalo ujumbe wake ni Mchango wa Mwalimu Nyerere katika uongozi, amani, umoja na uwajibikaji kwenye ujenzi wa Taifa.
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi (Picha: Maktaba)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇