LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 24, 2024

DK. MWINYI AMPONGEZA RAIS DK. SAMIA KUFUFUA MASHINDANO KOMBE LA MUUNGANO, ASEMA NI KUUTHAMINI MUUNGANO

Ibrahim Bakari, CCM Blog
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kurudisha mashindano ya Kombe la Muungano akisema hatua hiyo Itayafanya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano kuwa ya kipekee.

Amesema, pia uamuzi wa kuyarejesha mashindano hayo, ni alama ya Rais Dk. Samia kuuthamini Muungano na uamuzi huo umemjengea heshima kubwa.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo mjini Dodoma, wakati wa utoaji nishani, uzinduzi wa vitabu, Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais na kile cha picha ikiwa ni maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano.

Michuano ya Kombe la Muungano, iliyokuwa ikishirikisha timu tatu za juu katika Ligi Kuu na bingwa huiwakilisha Tanzania Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikoma miaka 20 iliyopita.

Simba ambayo inaanza michuano hiyo mwaka huu kwa kupambana na KVZ ya Zanzibar, ndiyo bingwa wa mwisho wa michuano hiyo.

Aidha Dk. Mwinyi amesema ni wazo zuri na kwamba tayari michuano inachezwa na amewakaribisha watu mbalimbali kufika Zanzibar  kushuhudia mashindano hayo.

Kwa upande mwingine, Dk.  Mwinyi amewapongeza walioandaa kitabu hicho kilichozinduliwa na kusema kwamba kitasaidia vizazi na vizazi kwani kutokufanya hivyo historia itapotea.

Amesema ni wajibu wetu kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wetu, na njia nzuri ni kuwaweka katika kumbukumbu ili isomwe na vijana wa sasa na kufahamu historia ya waasisi wetu na hata vizazi vijavyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, kwenye hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 60 ya Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Kitabu cha Safari za Picha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 60 uliofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024.
 

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages