Ibrahim Bakari
Machi 8 ya kila mwaka, ni siku maalumu kabisa, ya mwanamke duniani. Wapo wanaosema hata mwanaume awe na siku yake, lakini hilo kwa sababu mbalimbali limeshindikana. Halipo. Kilichopo ni siku ya Baba Duniani. Hii ipo lakini si Siku ya Mwanamme.
Niwakumbushe kidogo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, siku hii inayoadhimishwa kila mwaka Machi 8, ilianza kutokana na jitihada za wanawake wapatao 15,000 mwaka 1908 walipoandamana mjini New York, Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura.
Kilikuwa Chama cha Kisoshalisti cha Amerika kilichotangaza kuwa ni siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake, mwaka mmoja baadaye.
Wazo la kuwa Siku ya Kimataifa lilianzishwa na mwanaharakati wa masuala ya wanawake wa Ujerumani, Clara Zetkin ambaye alipendekeza wazo hilo mwaka 1910 katika mkutano wa Kimataifa wa Wafanyakazi Wanawake huko Copenhagen Denmark.
Katika mikutano ule, kulikuwa na wanawake wapatao 100 hapo kutoka nchi 17 na wakakubaliana kwa pamoja na kwa mara ya kwanza ilisherehekewa Machi 8, 1911 katika nchi za Austria, Denmark, Ujerumani na Switzerland.
Suala hilo likawa rasmi mwaka 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuanza kusherehekea siku hiyo na baadaye kubuni kauli mbiu ya kwanza mwaka 1996 ilikuwa ''Furahia yaliyopita, panga kwa ajili ya baadae''.
Kimsingi, Siku ya Kimataifa ya Wanawake duniani imekuwa siku ya kutathimini maendeleo ya wanawake katika jamii katika nyanja za siasa na uchumi na kubwa ni kusisitiza masuala ya usawa.
Kwa kifupi, hayo ndiyo ya huko enzi hizo katika harakati za kuifanya Siku ya Mwanamke duniani na zaidi Kuitambulisha ngazi ya kimataifa.
Nikimwangalia mwanamke, mara zote amekuwa kielelezo na alama kuu kwa maendeleo na ndiyo maana inasemwa kuwa palipo na maendeleo nyuma kuna mwanamke.
Mwaka 2021 baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akaapishwa kuiongoza Tanzania.
Katika moja ya mikutano na hutuba zake, aliwatoa wasiwasi Watanzania kuwa yuko imara, amepikwa na kupikika na watangulizi, ana uzoefu wa uongozi kitu anachokionyesha hadi sasa.
Lakini kikubwa ambacho tunakiona, Rais Samia akiwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameonyesha anaweza, anafanya uamuzi mgumu na kupigania haki kwa Watanzania.
Kitu kikubwa baada ya kujiamini katika nafasi yake, amewatengeneza wanawake wengi kwa kuwapa imani kwamba hata wanawake wanaweza.
Amewapa nafasi mbalimbali za uongozi na kufuta kabisa dhana iliyokuwa imejengeka kuwa nafasi kadhaa ni kwa ajili ya wanaume pekee.
Mfano mzuri ni Wizara ya Ulinzi, alipompeleka mwanamama, Dk Stigomena Tax kuongoza.
Alifanya kazi vizuri, lakini pia wapo wengi walioingia kwenye maeneo mbalimbali yaliyoaminika kuwa wanaume pekee wanaweza.
Nikianza kutaja mmoja mmoja hapa, nitajaza ukurasa, lakini itoshe kusema kuwa Rais Samia ameonyesha njia, amekuwa alama ya mwanamke shupavu na kuwapa nafasi wanawake mbalimbali ili wakunjue mbawa kuonyesha ushupavu wao.
Wapo ambao wameonyesha kweli mwanamke anaweza japokuwa si wote. Nakiri kusema hivyo. Kuna wakati Kampuni moja ya uchapishaji magazeti hapa nchini walikuwa wakiandaa mikutano ya Wakurugenzi na CEO vijana wanawake, inapendeza, hao ndio wanawake viongozi wa baadaye.
Nini nataka kusema. Kwa kuwa Rais Samia amewapa heshima wanawake, ametengeneza imani kwa Watanzania kuwa mwanamke anaweza, sasa na wenyewe waonyeshe wanaweza.
Wanawake kuteuliwa katika nafasi mbalimbali, kufanya kazi kwa kujituma ni wazi kutaingarisha alama ya ushupavu wa Rais Samia kuwa wanawake wanaweza.
Watanzania siku zote wanataka kuona matokeo ya utendaji kazi ya kiongozi bila kujali jinsia, lakini kwa kuwa nafasi iliyopo mbele ni mwanamke, wanatakiwa na wenyewe kupambana kuipigania nafasi lakini pia kuipigania jinsia na kufuta wazo la kusema ni nafasi za wanaume.
Wakati wanawake wanaadhimisha siku yao katika ngazi mbalimbali, kwa wanawake viongozi kwa nafasi kubwa na ndogo, ni vyema wakaendelea kupambana kuipamba alama ya mwanamke shupavu na hiyo pekee jamii itasema awepo mwanamke, awepo mwanaume hakuna kitakachoharibika.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan
Ibrahim Bakari ni mwandishi wa habari. MAONI 0754 264003, 0655 264003
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇