LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 2, 2024

MASHINDANO YA 'MISS TANZANIA' YALIANZA KWA RUKSA YA MZEE MWINYI

Na Ibrahim Bakari
Mwaka 1968, Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanu (Tanu Youth League - TYL) ulipiga marufuku maonyesho ya mitindo (fashion show), klabu za usiku na hata mashindano ya urembo.

TYL ilikuwa na kazi moja ya kuujenga Utamaduni wa Tanzania kwani uliathiriwa kwa kiasi kikubwa na utamadunia wa kikoloni.

Mambo hayo yalikuwa yakifanyika wakati huo kukiwa na vielelezo kadhaa vya utamaduni wa kikoloni, na TYL ilikuwa inataka kuusimamisha Utamaduni wa Mtanzania kama si utamaduni wa kiafrika. Wakati TYL ikiyafanya hayo, ilikuwa ni miaka saba tu tangu Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961.

Katika mahojiano ambayo niliwahi kuyafanya na aliyekuwa mwasisi wa mashindano hayo, Hashim Lundenga anasema lengo la TYL lilikuwa kutengeneza utamaduni halisi wa Mtanzania.

TYL iliamini kuwa kufanyika kwa mashindano ya mitindo, urembo na maonyesho ya mavazi si utamaduni wa Mtanzania asilia na kwamba kufanya hivyo ni kuendeleza mabaki ya ukoloni yenye utamaduni wa kigeni.

Lundenga anasema wakati huo, Waziri wa Utamaduni, Chadiel Mgonja naye alikuwa moto akisimamia kikamilifu ujenzi wa Utamaduni wa Mtanzania.

Lundenga anasema mwaka 1994 walianza mashindano baada ya Rais Ali Hassan Mwinyi ambaye amefariki Februari 29, 2024 kutoa ruksa kwa uchumi huria kwa kila Mtanzania kufanya kile anachodhani kinaweza kusogeza uchumi ukiwemo utamaduni bila kuleta athari katika mageuzi hayo.

Baada ya ruksa hiyo, ndipo kukafumuka klabu za usiku, kuanza kwa maonyesho ya mavazi , mitindo na hilo la urembo.

Lundenga anasema mwaka 1994, walianzisha mashindano ya urembo Tanzania na mshindi wake wa kwanza alikuwa Aina Maeda huku mashindano hayo yakidhaminiwa na Palmolive na Whitesands Hotel.

Anasema mashindano yalipokewa kwa kishindo na msisimko mkubwa kwa kuwa kwa siku nyingi Watanzania walikuwa wanakosa mashindano hayo.

Hata hivyo, Aina Maeda hakufanya vizuri kwenye mashindano ya Miss World yaliyofanyika kwenye mji wa Sun City, Afrika Kusini. Maeda alikuwa kati ya warembo 87 walioshiriki shindano hilo.

Mashindano ya urembo yaliendelea na mwaka uliofuata utaratibu ukawa huo huo, lakini safari hii pamoja na kuruhusiwa, lakini Serikali ilisema lazima mashindano kufuata mila na desturi za Watanzania.

Katazo la kwanza, Wizara ya Michezo na Utamaduni, ilipiga marufuku wanafunzi kushiriki lakini pia kufanya mashindano kwa warembo kuvaa nguo zinazoonyesha maumbile.

Mjadala mzito ulizuka mwaka 1995 kwa Emilly Adolph kushiriki mashindano hayo ilhali ni mwanafunzi. Emilly alikuwa Shule ya Sekondari ya Central Dodoma.

Sakata la Emily halikuwa la mzaha, kwani ilifika hatua alitaka kuvuliwa taji hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa mwanafunzi licha ya kuwa mwenyewe alikanusha. Hata hivyo, shule yake ilijitokeza na kumfuta kwenye vitabu vyake vya shule.

Tangu mwaka 1995 ikawa kila mwaka mashindano yaliboreshwa na hasa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Wizara Michezo na Utamaduni walikuwa wakali kuhakikisha masuala ya utamaduni na mila zetu   yanalindwa.

Itakumbukwa pia Utamaduni ulikuwa na eneo maalumu Wizara ya Elimu na Utamaduni chini ya Dk Daniel Ndagala ambaye kwa sasa amestaafu.

Miaka ya nyuma, Utamaduni wa Mtanzania au wa Kiafrika, ulikuwa ukienziwa kwelikweli, maadili na weledi vilikuwa kipaumbele kwani hata katika hotuba mbalimbali za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa akitilia mkazo utamaduni wa Mtanzania.

Kimsingi, Ruksa ya Rais Mwinyi wakati huo, ilichochea kushika kasi kwa mashindano ya urembo kwani mpaka leo ni miaka 30 tangu mashindano ya urembo yalipoanza mwaka 1994 yakiongozwa na Hashim Lundenga, Prashant Patel, Bosco Majaliwa na Albert Makoye. Pia walikuwemo Prakash Patni na Ramesh Shah.

Aina Maeda- Miss Tanzania 1994 ambaye alikuwa Miss Tanzania wa Kwanza baada ya mashindano kufungiwa na Serikali Kwa zaidi ya miaka 20. Kushoto mshindi wa Pili Lucy (Tabasamu) Ngongoseke na kulia Dotto Abuu mshindi wa tatu

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages