Na Lydia Lugakila Karagwe,
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira BUWASA Kanda ya Karagwe imempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mbali mbali ndani ya Wilaya ya Karagwe, Mkoa na taifa kwa ujumla hasa katika kuhakikisha wanamtua Mama ndoo kichwani.
Uongozi wa Buwasa umetoa pongezi hizo baada ya kupokea mabomba mradi wa maji Rwakajunju uliopo katika kata ya Nyabiyonza Wilayani humo huku pia nao Wananchi wakimpongeza Rais Samia kwa kuwaona baada ya kuteseka kwa muda mrefu kupata huduma ya maji katika eneo hilo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji miji 28 Kayanga mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe baada ya kupokea mabomba hayo Meneja wa Buwasa Kanda ya Karagwe Mhandisi Magreth Nyange amesema kuwa mradi huo wa kimkakati wenye lengo la kuondoa tatizo la maji ndani ya Wilaya hiyo unatarajia kunufaisha Wananchi katika kata 12 za Wilaya hiyo.
"Bomba hizi tumezipokea zitalazwa kutoka kwenye chanzo cha maji kuelekea eneo la mitambo ya kutibu maji na baada ya hapo Bomba nyingine zitaelekea katika tanki kubwa la maji hivyo nimshukuru Rais Samia kwa kuwapambania wana Karagwe hasa katika utekelezaji wa miradi mbali mbali iliyomo Wilayani humu" alisema Mhandisi Magreth.
Mhandisi Magreth ameongeza kuwa mradi wa maji miji 28 Kayanga ulioanza utekelezaji wake mnamo mwezi April 2023 unatarajia kukamilika ifikapo Desemba 2025 huku ukigharimu zaidi ya shilingi Bilioni 64.
Amesema kuwa mabomba hayo ni hatua za kuendeleza atekelezaji mradi wa maji miji 28 Kayanga Wilayani humo huku Wananchi katika kata ya Nyabiyonza wakieleza furaha yao baada ya kuelekea kuondokana na tatizo la upatikanaji wa maji ndani ya Wilaya hiyo.
Wakizungumza katika eneo la mradi ikiwa ni baada ya kupokea mabomba hayo Wananchi hao akiwemo akiwemo Bi Reokadia Eustadi kutoka Kijiji cha Ahakishaka kata Nyabiyonza na Denice Jovin wamesema kuwa hatua hiyo ni ya kujivunua kwani inakwenda kuwanufaisha huku wakimshukuru Rais Samia Viongozi wa BUWASA kutokana na kuwaondolea changamoto iliyowatesa ya kufuata maji umbali mrefu na kupata maji huku maji waliyokuwa wakipata yalikuwa siyo safi na salama.
"Kwakweli tuna furaha sana tumeviona vifaa hivi na mradi tunajua mradi huu ukikamilika tutakuwa na utajiri mkubwa tunazidi kumshukuru Rais wetu"kwa kutuona walisema Wananchi hao.
Akieleza hatua na kazi iliyokwisha fanyika katika mradi huo Mhandisi Magreth amesema kuwa usanifu umeanza na katika tanki ujenzi na tayari umeanza ambapo wamemwaga zege la awali huku hatua ya usukaji wa nondo ukiendelea ili kuinua kuta za tanki la maji.
Aidha alishukuru Mbunge wa Jimbo la Karagwe na Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, pia Waziri wa maji na uongozi wa Wilaya hiyo katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maji ndani ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Kalanga Laizer alipongeza hatua hiyo na kuwaomba Wananchi kuweka jicho Katika mradi huo kwa kuutunza na kuulinda huku akiwasihi Viongozi kuweka juhudi katika uangalizi makini ili kufikia malengo kusudiwa
Hata hivyo naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Karagwe Paschale Rwamugata amesema mradi huo unahitaji uangalizi mkubwa kwani fedha hizo zinatolewa na Rais Samia kwa malengo ya kuwanufaisha Wananchi wake hivyo mradi huo ulindwe na kutunzwa kwa manufaa ya sasa na ya baadae.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇