LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 29, 2024

MAONI: TRENI LA UMEME NI MAFANIKIO MAKUBWA LAKINI..

Niipongeze serikali kwa kuthubutu. Ni nchi chache Afrika hiki kitu kipo. Binafsi nimeona Morocco, South Africa, Algeria, Ethiopia na Tunisia. Bravo Tanzania.


Nakumbuka kulikuwepo na wapambe waliodai majaribio yalifanywa 2000. Nakumbuka niliwaambia haiwezekani. Na ndio ukweli. TRENI la umeme linahitaji mambo kadhaa: umeme usiokonyeza (achilia mbali wa mgao), uzio imara njia yote, elimu kwa watumiaji na wasio watumiaji, vituo vya kisasa, mifumo ya ki electronic ya kugundua majanga,  n.k. 


Ukifika eneo la EU utaona kampuni inaitwa IEE. Ndiyo inamiliki treni la umeme. TRENI linaloenda kasi mara 100 ya hili la kwetu. Umeme wa nyuklia. Njia zote zimewekewa uzio. Raia wana Elimu ya kutosha kuhusu matumizi. Pamoja na hayo yooote kunatokea ajali. Nyingine mbaya sana. Kuna mpaka ajali za kujitakia. Dereva tu anaamua kufa na watu! Hata kwenye ndege! Maana yake watu wanaajiriwa bila kupimwa vizuri akili. Kuna ajali zinazotokana mfano na tetemeko la ardhi au mafuriko. Kuna ajali tu za matatizo ya kiufundi na uzembe. 


Wakati tulifurahi ujio wa treni la umeme tusijisahau ili kufurahishana. 


Tujiandae vyema. Bado hakuna uzio wa kutosha. Sehemu kadhaa ya njia hazijakingwa. Bado hatujatoa elimu ya kutosha kwa wananchi haswa watumiao reli au waishio pembezoni. Kwa mfano treni la kasi halifai kwa wasafiri wanaobeba mizigo au mafurushi mengi. Halifai kama tutajaza watu kwenye mabehewa mpaka wasimame kama kwenye daladala. Halifai kama abiria wengi watakata tikiti saa ya safari. Je wafugaji wetu, watoto wetu n.k. tumewaelimisha vya kutosha? 


Bado tuna wanasiasa na wafanyabiashara uchwara ambao wako tayari kuhujumu miundombinu. 


Athari za mabadiliko tabia nchi zimeongezeka nchini. Tuna mfumo wa kutabiri au kugundua mfano mafuriko, tetemeko, kabla treni halijapita? 


Tusikimbilie kuanza kama umeme utakuwa wa mashtaka kama ulivyo sasa. Ajali hutokea pale treni liko spidi halafu umeme ukatike. Watu hukatika vipande vipande kutokana na msukumo. India ni maarufu kwa ajali za hivi.


Tusipojiandaa vyema tukaharakisha tunaweza kupata ajali itakayofanya tuchukie treni la umeme.


Lakini kwa sasa tunasema hongereni, it's a step in the right direction. 

Basi na iwe KHERI!


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages