Rais Dk. Samia Suluhu Hassan
Na Ibrahim Bakari
Mwaka mpya 2024 umeanza kwa staili ya aina yake, maisha yanaendelea kama ilivyokuwa mwaka jana na kama inavyofahamika, huu ni mwaka wa uchaguzi.
Kweli ni mwaka wa siasa, maana Chadema wameuanza mwaka kwa maandamano waliyoyaita ya amani.
Mpango mzima ulikuwa kuwasilisha hisia zao kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa kupinga kuwasilishwa kwa Miswada ya Uchaguzi, lakini kile walichodai maisha magumu.
Kati ya vitu ambavyo nawapongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan na Jeshi la Polisi ni kuruhusu Chadema kufanya maandamano yao bila kuwa na mikwaruzo.
Wakati mwingine, mtu anajaza upepo kifuani na ukiendelea kumbana upepo unazidi kujaa na ukija kubutuka, athari zake zinakuwa kubwa.
Nakumbuka kuna kipindi Rais Jakaya Kikwete akiwa ofisini, aliwahi kunywa juisi na viongozi wa Chadema Ikulu, na presha yao ikaisha. Nini, wamekaa na Rais Kikwete wakafunguka yao ya moyoni. Ni kama mgonjwa amepata tiba.
Maandamano yale ya Januari 24, ni kama kielelezo kuwa sasa kumekucha na watu wakae mkao wa kula. Hata Rais Samia kwenye salamu zake za Mwaka Mpya alisema 2024 ni mwaka wa uchaguzi hivyo kila mmoja awe tayari na Chadema wanaonekana kuanza wanavyojua wao.
Wakati Chadema wakiendelea na hayo, CCM na wenyewe kupitia kwa mwenezi, Paul Makonda anaendelea na shughuli katika mikoa 20. Anachofanya ni kuwauliza wananchi, Serikali imefanya nini, mnataka nini na ifanye nini. Hayo ndiyo wananchi wanataka. Siyo kuandamana.
Nikija kwenye hoja yangu, ukiangalia utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa Mwenyekiti wetu wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, anastahili pongezi na si za kinafiki. Rais anapambana kila sekta anataka kuona inapiga hatua.
Kila ukisoma kwenye vyombo vya habari, ukiangalia TV, ukisikiliza redio na mitandao ya kijamii, Rais ametekeleza ilani ya CCM kwa eneo kubwa na ninathubutu kusema asilimia 90.
Nakumbuka asubuhi moja nilikuwa ninasikiliza Radio RFA kipindi cha Matukio, bahati mbaya sikukariri kile kijiji kilichopo mkoani Shinyanga, kina mama wanamshukuru Rais Samia kwa kuwaletea maji. Walisema walikuwa wanaamka saa 8 hadi 9 usiku na maji wanapata saa 10 jioni. Hapo ndipo palinipa hisia. Walisema wakati mwingine hawapati maji kabisa. Sasa wanasema maji yanapatikana, ahsante sana Rais Samia na ndoa zao zimeimarika.
Ukiangalia, mbali na maji ambayo maeneo mengi yanapatikana, kuna huduma za kijamii kama afya, elimu, haki, miundombinu ya barabara, uwekezaji, utalii na mengine mengi, Rais ametekeleza kikamilifu na anastahili kabisa kupewa mauwa yake.
Huo ni mwaka wa nne tu amefanya hayo na mengine yanaendelea, sasa akipewa mingine mitano na umeme wa Rufiji unakuja, hakika tutasahau.
Sasa, kitu ambacho ninakiona ni baadhi ya watendaji wake, wanamwangusha mno. Baadhi hawajitambui, hawajui wajibu wao, hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.
Mfano mzuri, watendaji wa Idara ya Maji Lindi, wameshindwa kutekeleza wajibu wao hadi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofika na kukuta hadi pikipiki zimefungiwa stoo na kumwagiza Waziri wa Maji Awesso Awesso kuzigawa kwa watendaji.
Sasa unajiuliza aliyeamrisha pikipiki kuwekwa stoo alikuwa anawaza nini kama si kumwangusha Rais?
Imekuwa jambo la kawaida kwamba kila Waziri Mkuu anapofanya ziara, Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko wanalia na baadhi ya watendaji wazembe.
Madudu mengine ya wachache wanaomwangusha Rais tunayaona katika ziara ya Mwenezi wa CCM Taifa, Paul Makonda.
Hawa hawako kabisa kwenye kasi ya Rais Samia, wanamchonganisha na wananchi. Kuna Mkurugenzi alishindwa kutoa maelezo ya matumizi ya Sh 500 milioni zilizotolewa na Rais Samia kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Burige hadi akaambiwa asitoe macho atoe maelezo. Anaulizwa maswali ya msingi, anashindwa kutoa maelezo.
Sasa, huyo ni mmoja, katika eneo moja, kuna wangapi wako huko kwenye mikoa mingine ambako hatujawaona kwenye mitandao wakiumbuliwa?
Kimsingi, sitaki kutaja nani na nani, lakini walioonekana wameonekana, sasa hakuna haja ya kuwashika mkono, hakuna haja ya kuwabembeleza kwani hawa ni wachonganishi wa Serikali na wananchi ilhali wao ndio wazembe.
Serikali inapeleka mamilioni kwenye halmashauri za ujenzi wa hospitali au vituo vya afya, watendaji hawajengi, wakijenga ni chini ya kiwango kama sio chini ya kiwango, thamani ya ulinganifu haifanani.
Kinachotakiwa ni kumsaidia Rais lakini inashangaza kila inapotokea ziara za viongozi wanakutana na madudu mengi ya watendaji, hawa ndio wanaomwangusha Rais.
Mbali na hao, hata baadhi ya mawaziri, manaibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya ni kama hawajitambui kutekeleza majukumu yao.
Huku mitandaoni wapo wanaosema kuna watu wanasubiri wakumbushwe, na kama ni hivyo basi panga liwapitie mapema kupitia wananchi. Malalamiko ya wananchi yapimwe, yaangaliwe na iwe kigezo cha panga kwa kushindwa kutekeleza wajibu.
Ibrahim Bakari ni mwandishi wa habari. Simu 0655 264003.
Your Ad Spot
Feb 5, 2024
Home
featured
siasa
MAKALA: RAIS DK, SAMIA 'HANA BAYA' ANASTAHILI MITANO TENA, WATENDAJI MSIMUAGUSHE
MAKALA: RAIS DK, SAMIA 'HANA BAYA' ANASTAHILI MITANO TENA, WATENDAJI MSIMUAGUSHE
Tags
featured#
siasa#
Share This
About Bashir Nkoromo
siasa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇